ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 2, 2014

Mwanasheria Mkuu Z’bar azikataa ibara 22 Katiba

Dodoma.Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman amezua kizaazaa bungeni baada ya jana kupiga kura ya ‘hapana’ katika ibara 22 kwenye Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa.
Akipiga kura hiyo, Othman ambaye hivi karibuni alijiondoa katika Kamati ya Uandishi kwa kutoridhika na baadhi ya mambo, alieleza kutokubaliana na ibara ya pili, tisa, 86, 37, 70 hadi 75 na Sura ya 11 ambayo ina ibara ya 158, 159, 160 na 161 pamoja na Sura ya 16 yenye ibara za 243 hadi 251 na Nyongeza ya Kwanza inayozungumzia mambo ya Muungano.
Hatua hiyo ilionekana kuwaudhi baadhi ya wajumbe kiasi cha kumzomea, hivyo baada ya Bunge kuahirishwa alilazimika kutolewa mlango wa nyuma wa Ukumbi wa Bunge ambao hutumiwa na Waziri Mkuu huku akiwa amesindikizwa na wanausalama kwa kuhofia vurugu.
Wakati akisindikizwa, alikuwa ameongozana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho.
Kwanza alipelekwa kwenye chumba kimojawapo katika jengo la Bunge ambako alikaa kwa nusu saa kabla ya kutolewa nje ya eneo la Bunge ambako alipanda gari alilokuwamo Kificho na kuondoka.
Hatua hiyo ya Othman imekuja wakati Waziri wa Sheria wa Zanzibar, Abubakary Khamis Bakary (CUF) akiwa hayumo bungeni baada ya kususia vikao hivyo pamoja na wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa).
Baadaye Othman aliliambia gazeti hili kwamba licha ya kuwa yeye ni Mwanasheria Mkuu wa SMZ alitumia utashi wake wa kidemokrasia kupiga kura kuzikataa ibara hizo, kutokana na kutoridhishwa na jinsi zilivyoandikwa.
“Katika suala la Katiba, Serikali ilishatamka kwenye Baraza la Wawakilishi na hata nje ya Baraza kwamba haina msimamo. Ndiyo maana uliona misimamo ilikuwa imeachwa kwenye vyama vya siasa, sasa mimi siyo Mwanasheria Mkuu wa chama chochote.
“Kwa hiyo kama Serikali haikuwa na msimamo kwa maana ya upande, maana yake ni ipi pengine unisadie… nilipiga kura kwa kuzingatia utashi wangu na maoni yangu.”
Alisema awali, alikuwa ameamua kutopiga kura lakini baadhi ya watu wenye busara walimshauri kutumia demokrasia yake kuonyesha yale anayokubaliana nayo na yale asiyoyakubali… “Mtu unaweza kuwa na msimamo fulani, lakini kwa jinsi binadamu tulivyo, siyo lazima msimamo wako uwe sahihi, kwa hivyo na mimi niliwasikiliza watu wenye busara nikaona ushauri wao unafaa ndiyo maana nilikwenda kupiga kura.”
Ashambuliwa bungeni
Baada ya Othman kupiga kura hiyo, Mbunge wa Chwaka, Yahya Kassimu Issa, aliomba mwongozo wa mwenyekiti na kumshambulia kwa hatua hiyo.
“Muda wote huo hakuwapo na siyo kama anaumwa, mzima lakini kwa kejeli tu kuonyesha kwamba yeye kasoma. Sasa sisi tumemaliza anakuja hapa, tulitegemea awepo katika wale wenzake na kutoa hoja zake. Hivyo mwanasheria kama huyu ana masilahi na nchi huyu?”
Hali hiyo iliibua hisia za baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar wakisema; “Hafai, hafai.” Issa aliendelea huku akikatishwa na sauti za wajumbe zilizokuwa zikisema hafai, “Rais amemteua amsaidie ili kazi yake iwe rahisi. Kazi inayotukabili ni hii ya hivi sasa (mchakato wa Katiba).”
Akijibu mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alisema wakati wanapopiga kura wajumbe hawapigi kwa vyeo. “Kura tunazopiga kila mtu zinatokana na dhamiri yake. Kwa hiyo, tusimhukumu mtu yeyote kwa cheo chake.”
Hata baada ya Sitta kutamka kufunga mjadala huo, wajumbe waliendelea kurusha maneno bila kutumia vipaza sauti wengine wakisema kamanda anayekimbia vita hafai na wengine wakitaka Rais amwondoe.
Akizungumzia hali hiyo, Othman alisema alitarajia kushambuliwa kwani ni mambo ambayo hutokea hasa katika mikutano inayowahusisha wanasiasa.
“Nilitarajia litokee hilo, lakini Yahya mwenyewe hakusema ni wapi na lini waliniita ili kutaka ushauri wangu na mimi nikakataa, pengine hawakuwa wakifahamu kwamba mimi ni AG na kwa bahati mbaya huenda wametambua hilo baada ya mambo kuonekana kama yanaharibika,”alisema.
Ibara alizozikataa
Ibara ya 2. Hii inazungumzia eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, likiwamo la Tanzania Bara na la Zanzibar pamoja na madaraka ya rais wa Jamhuri kugawa eneo lolote la nchi katika mikoa au kukasimu madaraka.
Ibara ya 9 inayoeleza ukuu wa Katiba yenyewe na kuwa ndiyo sheria kuu. Inazuia kutungwa kwa sheria yoyote inayotofautiana nayo na inaelekeza wananchi na taasisi zote kuitii.
Sura ya Saba (Ibara 70-75). Hizi zinahusu muundo wa muungano na mgawanyo wa majukumu na mamlaka ya Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na SMZ.
Pia ibara hizo zinafafanua wajibu wa viongozi wakuu katika kuhakikisha kuwa wanatetea, wanalinda, wanaimarisha na kudumisha umoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ibara ya 86 na 87 inayofafanua utaratibu wa uchaguzi wa rais wa Muungano na taratibu za kisheria kwa mgombea asiyeridhika na matokeo ya uchaguzi mkuu kupinga uchaguzi huo mahakamani.
Ibara ya 128. Hii inahusu mamlaka ya Bunge la Muungano na Baraza la Wawakilishi katika kutunga sheria na kuzuia Baraza la Wawakilishi kutunga sheria kuhusu jambo lolote ambalo liko chini ya mamlaka ya Bunge na kulizuia Bunge kutunga sheria kuhusu jambo lililoko chini ya Baraza la Wawakilishi.
Ibara za 159, 160, 161 zinazozungumzia Rais wa Zanzibar na majukumu yake, Baraza la Mapinduzi Zanzibar na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar pamoja na majukumu yake.
Sura ya 16 (243-251). Hizo zinahusu Mfuko Mkuu wa Hazina na Fedha za Jamhuri ya Muungano. Misingi ya matumizi ya fedha za umma, misingi inayoongoza matumizi ya fedha za Muungano, akaunti ya fedha ya pamoja, mfuko wa hazina na masharti ya kutoa fedha za matumizi katika mfuko huo.
Pia sura hiyo inaweka utaratibu wa kuidhinisha matumizi ya fedha kabla ya sheria inayohusu matumizi ya fedha ya Serikali, mfuko wa matumizi ya dharura na ulipaji wa mishahara ya baadhi ya watumishi.
Nyongeza ya Kwanza. Hii ni orodha ya mambo ya Muungano ambayo yameongezwa kutoka saba ya Rasimu ya Warioba kuwa 14.
Mtazamo wa wajumbe
Mjumbe, Ezekiel Maige alisema kumhukumu mwanasheria huyo ni kutomtendea haki kwa sababu kwa dhamana yake, anaangalia masilahi ya watu mbalimbali na si ya CCM pekee.
“Huwezi kumhukumu kwa sababu amepiga kura ya kutokubaliana na vipengele katika Katiba, jambo la msingi ni kupeleka katika Kamati ya Maridhiano,” alisema.
Naye, Hamad Rashid Mohamed alisema: “Hakatazwi mtu kuwa na mawazo yake binafsi…tulitegemea haya mambo yote anayoyasema angekuwa ameshashauriana na Serikali na kama bado angewaambia wajumbe wengine tukajadiliana mapema.”
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Sio kila mtu mchumia tumbo