Advertisements

Tuesday, October 7, 2014

Taasisi zenye harufu ya ufisadi zatajwa

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA), Dk. Matern Lumbanga, akizungumza na waandishi wa habari

Taasisi 13 za serikali nchini, ikiwamo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, zimekumbwa na kashfa ya kuwa na viashiria vya rushwa, huku 19 zikiwa zimefanya malipo yenye shaka ya thamani ya Sh. bilioni 1.7 katika manunuzi ya umma kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

Pia, kampuni 19 zimefungiwa kushiriki katika zabuni kwenye taasisi za umma nchini kutokana na madai ya kushindwa kutekeleza kikamilifu mikataba iliyoingia, huku nne zikiwa zimesimamishwa.

Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA), wakati ikitoa taarifa kuhusu matokeo ya ukaguzi wa shughuli za ununuzi katika taasisi za umma kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30 mwaka huu.

Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Dk. Matern Lumbanga, alisema katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, mamlaka hiyo ilifanya ukaguzi wa shughuli za ununuzi kwa taasisi 76 za umma katika maeneo mawili ya ukaguzi wa taratibu za ununuzi, ambao ulihusisha taasisi 68 na uhakiki wa hoja za ukaguzi kwenye kaguzi zilizofanywa kipindi cha nyuma kwa kuhusisha taasisi nane.

Dk. Lumbanga alisema matokeo ya ukaguzi huo yalibaini uwapo wa viashiria vya rushwa kwa zaidi ya asilimia 20 kwa taasisi 13 za umma zikiwamo halmashauri za wilaya, majiji pamoja na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Alitaja baadhi ya halmashauri za wilaya na manispaa zilizobainika kuwa na harufu ya rushwa na kiwango chake katika mabano kuwa ni Kondoa (30), Kilwa (22.5), Kishapu (62.6), Monduli (21), Maswa (31), Kinondoni (22) na Musoma (27).

Nyingine ni halmashauri za majiji ya Dar es Salaam (33) na Mwanza (27.9), Mamlaka ya Maji na Mazingira Lindi (51), Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Lindi (28.9), Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii (33) na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (25.3).

KAMPUNI 19 ZAFUNGIWA
Dk. Lumbanga ambaye ni Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, alisema pia bodi ya wakurugenzi ya mamlaka hiyo imezifungia kampuni 19 kutoshiriki katika zabuni kwenye taasisi za serikali za umma nchini kutokana na kushindwa kutekeleza kikamilifu mikataba iliyoingia na taasisi hizo na hivyo kusababisha mikataba hiyo kuvunjika.

Bodi hiyo pia imezisimamisha kwa muda kampuni nne kutoshiriki katika zabuni za umma hadi pale mchakato wa kuzifungia au la utakapofikiwa.

“Kutokana na matakwa ya vifungu hivyo hapo juu, Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA katika kikao chake kilichofanyika leo (jana), imezifungia kampuni 19 kwa kushindwa kutekeleza kikamilifu mikataba iliyoingia,” alisema Dk. Lumbanga na kuongeza:

“Bodi pia imezisimamisha kampuni nne kushiriki katika zabuni za umma kwa muda hadi pale mchakato wa kuzifungia au la utakapokamilika. Uamuzi huu ni kwa mujibu wa kifungu cha 97 cha kanuni za ununuzi wa umma wa mwaka 2013.”

Aidha, matokeo ya ukaguzi huo katika eneo la thamani ya fedha, yalibaini taasisi 19 kufanya malipo yenye shaka ya Sh. bilioni 1.7, huku miradi 120 yenye jumla ya thamani ya Sh. bilioni 32 sawa na asilimia 58.5 ya miradi yote iliyokaguliwa utekelezaji wake ulikuwa wa wastani.

Mwenyekiti huyo wa bodi aliongeza kuwa, kati ya miradi 205 iliyokaguliwa, ni miradi 33 pekee yenye thamani ya Sh. bilioni 18.5, sawa na asilimia 16.1, ndiyo iliyotekelezwa kwa ukamilifu mbali na kuwa na mapungufu madogo madogo.

Kutokana na matokeo hayo, bodi ya wakurugenzi ya PPRA imeiagiza menejimenti yake kufanya uhakiki wa taarifa za kuwapo kwa malipo ya ziada kwa kazi ambazo hazikufanywa ili maamuzi stahiki yaweze kuchukuliwa.

Baadhi ya maamuzi mengine yaliyochukuliwa na bodi hiyo ni kupendekeza kwa mamlaka husika kuchukua hatua za kinidhamu kwa maofisa waliosimamia miradi 52 ambayo inadaiwa kutotekelezwa katika viwango vilivyoainishwa kwenye mikataba.

Alitaka pia kuundwa kwa mikakati ya pamoja kati ya PPRA, Tamisemi, Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na wadau wengine ili kuondoa tatizo la usimamizi wa mikataba lililoonekana kwenye serikali za mitaa.

Kadhalika, alitaka kutolewa taarifa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa ajili ya kufanya uchunguzi zaidi na kuzichukulia hatua taasisi na miradi yenye viwango vya zaidi ya asilimia 20 ya viashiria vya rushwa.

Sambamba na hilo, alitaka hatua za kinidhamu na kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya maofisa wote walioshiriki kuidhinisha malipo yenye shaka baada ya kufanya uhakiki wa kina wa malipo hayo ili kubaini kiasi halisi kilichofanywa na wahusika.

Bodi hiyo pia ilipendekeza kutolewa kwa taarifa kwa bodi ya wahandisi, wasanifu majengo na wakadiriaji majenzo, wakandarasi kuhusu ukikukwaji wa maadili ya kitaaluma kama ilivyoainishwa katika taarifa za ukaguzi.

Ukaguzi huo ulifanywa kwa ufadhili kutoka Public Finance Management Reform Programme (PFMRP), Belgium Technical Cooperation (BTC) na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) huku jumla ya mikataba 4, 532 yenye thamani ya Shilingi bilioni429.5 ikiwa imekaguliwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: