ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 7, 2014

Chadema sasa yajipanga kupiga kambi jimbo la Sitta

Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Baraza lake la Vijana Taifa (Bavicha), kimetangaza mkakati wa kwenda kuweka kambi kwenye Jimbo la Urambo Mashariki linaloongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta.

Lengo la chama hicho ni kuwaeleza namna kiongozi huyo alivyochakachua Rasimu ya maoni ya Watanzania.

Mkakati huo ulitangazwa jana na Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Patrobas Katambi na Katibu wa Baraza hilo, Julius Mwita, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Shule ya Sekondari Mwisenge mjini Musoma.


Katika mkutano huo ambapo baadaye ulifuatiwa na maandamano makubwa ya amani kuwasindikiza viongozi hao hadi Makao Makuu ya Chadema mjini Musoma, Mwenyekiti Patrobas, Katibu wake Mwita pamoja na Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere, walisema wamedhamiria kufanya hivyo ili kuueleza umma jinsi Bunge la Katiba lilivyotumia vibaya fedha za wananchi na kushindwa kuwapatia haki wananchi.

Katambi alisema Rasimu ya Katiba iliyopitishwa bungeni imewanyima haki za msingi wananchi wakiwamo wa Jimbo la Urambo, kinyume cha sheria na mkataba wa Baraza la Umoja wa Mataifa (UN) la mwaka 1948 pamoja na mkataba wa Afrika wa mwaka 1981.

“Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na kupitishwa na Bunge la Katiba kinyume cha matakwa ya wananchi wenye nchi, ni kiini macho na ni changa la macho. Tunahitaji wananchi waikatae hii Rasimu ya Katiba iliyochakachuliwa," alisema.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: