Advertisements

Monday, October 20, 2014

TANZANIA INATAKA MABADILIKO UCHAGUZI 2015

Wananchi wakiwa wamefurika katika kituo cha kupiga kura cha Shule ya Mtoni, wilaya ya Mjini mwaka 2010.
Ilikuwa asiye na mwana abebe jiwe, kama Zainabu Ngwadani mkazi wa Mtoni Kidalu, wilaya ya Magharibi, akipiga kura huku akiwa na mtoto wake mwenye umri wa miezi mitano, katika kituo cha shule ya Mtoni mwaka 2010 Picha zote na The Nkoromo Blog.

Na Emmanuel Muganda, Washington, DC
Tanzania itafanya uchaguzi mkuu wa rais na bunge mwaka ujao 2015. Huu utakuwa uchaguzi wenye changamoto kubwa kwa chama tawala tangu kuanzishwe mfumo wa vyama vingi vya siasa.
   Tanzania ilifanya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi vya siasa mwaka 1995 na kwa sababu vyama vya siasa vilikuwa vichanga wakati huo, chama tawala, CCM kiliibuka na ushindi ingawa kulikuwa na ushindani mkubwa uliotolewa na Augustine Mrema, waziri wa zamani wa ulinzi na naibu waziri mkuu chini ya utawala wa CCM. CCM pia kilishinda uchaguzi uliofuata 2000, na uchaguzi wa 2005 kwa asilimia kubwa. Lakini katika uchaguzi wa 2010 asilimia ya ushindi wa CCM ilianza kuporomoka na chama cha ushindani, Chadema, kikaibuka na idadi iliyoongezeka ya wabunge na asilimia iliyopanda ya kura alizopata mgombea wa chama hicho.
  Katika chaguzi zote zilizotangulia CCM ilikuwa na uhakika wa kushinda kwa sababu moja kubwa ya udhaifu wa vyama vya upinzani. Sababu nyingine ilikuwa ni miundombinu za kisiasa zilizojengwa na chama tawala tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake mwaka 1961. CCM imejenga matawi na ofisi kila sehemu nchini kukiwa na vijijini. Kwa sababu hiyo, wagombea wa CCM hawakuona lazima ya kujadilia masuala yaliyoikabili nchi, badala yake wakitoa ahadi za kuboresha miundombinu, na kuleta maisha bora kwa Watanzania wote. Na kwa sababu hiyo pia, imejengeka dhana ndani ya chama kwamba yeyote atakayeteuliwa na chama hicho kuwa mgombea ndiye atakayekuwa rais wa Tanzania. Lakini uchaguzi wa 2015 utakuwa ni uchaguzi wa “issues,” masuala. Na dhana hiyo imeanza kukabiliwa na changamoto.

   Suala moja kubwa katika uchaguzi ujao litakuwa ni katiba mpya. Rasimu ya katiba iliyopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba ilibadilishwa na Bunge la katiba, baada ya vyama vya upinzani kujiondoa kwenye mchakato huo na kuunda kundi la UKAWA. UKAWA inashirikisha vyama vikuu vya upinzani, CHADEMA, CUF NA NCCFR-Mageuzi. Vyama hivi viliunga mkono muundo wa serikali tatu kama ilivyopendekezwa na tume ya Jaji Warioba. CCM inapinga muundo wa serikali tatu. Mbali na hayo, katiba iliyopitishwa na Bunge la katiba ambalo wengi ni wafuasi wa CCM, imefuta pia tunu za taifa ambazo ni pamoja na maadili ya uongozi na raia kuwa na mamlaka ya kuwaachisha kazi wabunge wao kama hawataridhika na uongozi wao. Hii ndiyo katiba, ambayo baadhi wameipachika jina, katiba ya Sitta na Chenge, ambayo CCM hivi sasa inaipigia chepuo. Na katiba hii itakayokuwa suala kubwa katika uchaguzi wa mwaka 2015.
   Licha ya shamrashamra na mayenu yaliyokatwa bungeni baada ya kupitishwa kwa katiba hii, mwenyekiti wa CCM, rais Jakaya Kikwete, ameanza kutambua kwamba muitikio wa wananchi kwa katiba hii ni mdogo sana katika maeneo aliyoyatembelea. Akizungumza hivi karibuni katika sherehe ya kumbukumbu ya kifo cha hayati Mwalimu Julius Nyerere, rais Kikwete alikiri wazi kwamba kunahitajika muda mrefu wa kujipanga kabla ya kutangaza kura ya maoni na kuonyesha kuwa huenda kura ya maoni isipigwe mpaka baada ya uchaguzi wa 2015.
“Juzi nilikuwa Mwanza nikawaeleza ila hata hawakuonyesha kuwa kuna jambo jipya na la muhimu linawajia. Walibaki kimya. Leo pale uwanjani nyote mumeshuhudia tukilisema na kulitilia mkazo ila wananchi walibaki kimya, wakituangalia. Hii siyo kawaida kwa jambo nyeti kama hilo. Hata wewe mzee, (akimtaja Sitta aliyekuwa amekaa pembeni yake) ulipotajwa na huku ni kwenu nilitarajia shangwe za hali ya juu kutokana na kazi uliyofanya lakini ndo wamebaki kimya. Lazima tufanye kazi ya ziada.” Alisema Kikwete.
   Lakini kazi ya ziada haitakuwa rahisi kwa CCM na viongozi wake. Tayari viongozi wa upinzani chini ya UKAWA wameshatangaza kuanzisha kampeni za kuipinga tafsiri ya rasimu iliyotolewa na Sitta na Chenge na kupitishwa na wabunge wa CCM. Mbali na UKAWA, mwenyekiti wa tume iliyoandika rasimu ya katiba, Jaji Joseph Warioba, naye ametangaza kuanzisha kampeni ya kupinga kupitishwa kwa rasimu hiyo iliyopitishwa na bunge. Akizungumza mjini Bunda hivi karibuni, Jaji Warioba alisema kuwa katiba hiyo haina maoni yote ya wananchi kama inavyodaiwa na Bunge maalumu. Alitaja mfano wa pendekezo la kuwepo kwa kipengele cha maadili ya viongozi ili kuwadhibiti dhidi ya vitendo viovu kama vile ufisadi, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. Lakini, alisema Warioba, wajumbe wa Bunge walirekebisha kifungu hicho hadi kikapoteza maana. Warioba alizungumzia pia mfumo wa serikali tatu uliokuwa umependekezwa katika mkusanyo wa maoni wa rasimu aliyopeleka bungeni, pia kuwapa raia madaraka ya kuwawajibisha wabunge wao na rais kupunguziwa madaraka, mambo ambayo yameondolewa na Bunge maalumu. Aliwashauri wananchi waisome katiba iliyopendekezwa kwa makini kabla ya kuipigia kura.
  Upinzani mwingine kwa katiba hiyo unatoka kwa baadhi ya viongozi wa kidini. Kwa hiyo, kwa pamoja, kampeni za Jaji Warioba, viongozi wa UKAWA na viongozi wa kidini zitakuwa na athari kubwa katika matokeo ya kura ya maoni ya kukubali au kuikataa katiba iliyopitishwa na Bunge maalum. Na kama katiba hii itapigiwa kura na kukataliwa kabla ya uchaguzi wa 2015 hilo litakuwa doa kubwa kwa chama tawala ambacho kimewekeza katika katiba ya Sitta na Chenge.
    Suala jingine litakalofanya uchaguzi wa 2015 kuwa uchaguzi tofauti na wenye msisimko, ni uamuzi wa vyama vikubwa vya upinzani, chini ya mwavuli wa UKAWA, kusimamisha mgombea mmoja wa urais, na kutosimamisha wagombea watakaoshindania nafasi moja katika uchaguzi mkuu. Ikiwa uamuzi huu utazingatiwa na kutekelezwa utatoa changamoto kubwa kwa CCM ambayo imekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka hamsini. Upinzani nchini Kenya uliweza tu kuindoa KANU madarakani baada ya kukubaliana kuungana. Katika uchaguzi wa 2005 mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete alishinda kwa asilimia 80. Katika uchaguzi wa 2010 ushindi wa Kikwete ulikuwa wa asilimia 60 wakati ambapo idadi ya wapiga kura walioshiriki katika uchaguzi kwa mara ya kwanza ilishuka kuwa chini ya asilimia 50 ya wapiga kura waliojiandikisha.
    Suala la katiba litawezesha mjadala kuhusu mwelekeo wa nchi. Mwaka 1995 alipokuwa akimnadi Benjamin Mkapa kuwa rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere alisema kuwa Tanzania inataka mabadiliko, Watanzania wanataka mabadiliko. Lakini wakati huo Mwalimu hakusema ni mabadiliko ya aina gani wanayoyataka Watanzania. Na kwa sababu upinzani ulikuwa bado mchanga, ilionekana kuwa kwa CCM kubadilisha viongozi, mathalan, kutoka kwa Mwinyi hadi Mkapa, na kutoka kwa Mkapa hadi Kikwete, CCM ilikuwa inaleta au inafanya mabadiliko. Lakini hayo yalikuwa ni mabadiliko ya personalities tu na si mabadiliko ya kimsingi.
Hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanyika kisera kati ya utawala wa Mwinyi na Mkapa, ila kulikuwa na mabadiliko tu ya “style” au mtindo wa kutawala. Vivyo hivyo Kikwete hakubadilisha lolote la maana kutoka utawala wa Mkapa. Katika masuala kama vile raslimali za nchi, uwekezaji, na uwezeshaji wa Watanzania kumiliki maliasili zao hakuna mabadiliko yoyote kati ya utawala wa Mkapa na Kikwete. Kwa kulifanya suala la katiba kuwa suala la uchaguzi upinzani pia utaweza kuzusha mjadala kuhusu mwelekeo wa Tanzania hasa katika uwekezaji, maliasili, na nafasi ya Mtanzania katika mchakato mzima wa uwekezaji. Haitakuwa rahisi kwa mgombea wa CCM katika uchaguzi wa 2015 kutoa ahadi tu za ujenzi wa miundombinu kama alivyofanya Kikwete katika uchaguzi wa 2010. Upinzani ulioungana utalazimika kuhakikisha kuwa CCM haitumii tena ajenda ya ujenzi wa miundombinu kama ajenda ya uchaguzi mkuu 2015.
   Tanzania inahitaji mjadala kuhusu mwelekeo wa nchi katika uchaguzi mkuu. Raslimali za nchi zimekuwa zinapotea kutokana na mikataba mibovu iliyowekwa na watawala. Tangu iachane na sera za ujamaa na kujitegemea Tanzania imekuwa kama meli inayoyumbishwa baharini na pepo za wenye nguvu duniani, si kwa kupenda, bali kwa utashi wa viongozi wa nchi.
Mwalimu Nyerere aliposema 1995 kuwa Watanzania wanataka mabadiliko, hakumaanisha mabadiliko ya kiongozi kumpisha mwingine. Ni mabadiliko ya kimfumo, ambayo kama hayatafanyika, Tanzania itaendelea kulemewa na ufisadi. Ni mabadiliko ya ruuya( vision) ambayo bila kufanyika Tanzania itaendelea kulemewa na wimbi la matajiri wachache wakati mamilioni wakikosa huduma za kimsingi. Na kwa hapa tulipo, ni wazi kuwa bila mjadala wa mabadiliko haya katika uchaguzi wa 2015, Tanzania itaendelea kushuhudia wachache wakijichotea keki ya taifa wakati walio wengi wanashindwa hata kupata mlo mmoja kwa siku.

Tanzania inataka mabadiliko.

5 comments:

Anonymous said...

๐Ÿ‘๐Ÿ‘๐Ÿ‘๐Ÿ‘๐Ÿ‘๐Ÿ‘๐Ÿ‘๐Ÿ‘ sagi sana hongera brother umenena ๐Ÿ‘Œ๐Ÿ‘Œ๐Ÿ‘Œ๐Ÿ‘Œ๐Ÿ™๐Ÿ‘

Anonymous said...

Asante sana mdau. Kuubwa la msingi tu pamoja na vyama vya vitakavyoshiriki uchaguzi, CCM kusema ukweli ni wezi wakubwa wa kura nakumbuka kabisa mwaka 2010 waliwekwa watu kule Bagamoyo hotelini kwa maandalizi ya kura za wizi na kweli ilifanikiwa. Tuache kuwalaghai wananchi na kugawa pesa ambazo ni zile zile tupatazo benki na kodi za wananchi. Kugungua matawi na mashina sio tija yanafunguliwa kwa gharama yeyote ile kitu ambachjo hata vyama vinginevyo wanayo. Tumeona hata kule Amerika kuna dada mmoja anajulikana kupewa fedha ili afungue mashina ya CCM Je kweli huko ughaibuni mnafungua mashina yanasaidiaje uchaguzi wa Tanzania?? Au hamna kazi za kufanya huko America? Tafuteni huduma za kuikomboa jamii ya WaTanzania maswala ya CCM na vyma waachieni waTanzania tulioko huku nyumbani, tunaelewa ziaidi na tunapata shida sana na hivi vyama ninyi hamana mnalokwazika nalo! Huyu dada anawadanganyeni na si ajabu ameahidiwa nafasi ya vitu wanavyoita maalumu !! Mhusika wa hii blog DJ LK usibane iweke ndio siasa hizo. Boreka na vijimambo..

Anonymous said...

Asante sana mdau. Kuubwa la msingi tu pamoja na vyama vya vitakavyoshiriki uchaguzi, CCM kusema ukweli ni wezi wakubwa wa kura nakumbuka kabisa mwaka 2010 waliwekwa watu kule Bagamoyo hotelini kwa maandalizi ya kura za wizi na kweli ilifanikiwa. Tuache kuwalaghai wananchi na kugawa pesa ambazo ni zile zile tupatazo benki na kodi za wananchi. Kugungua matawi na mashina sio tija yanafunguliwa kwa gharama yeyote ile kitu ambachjo hata vyama vinginevyo wanayo. Tumeona hata kule Amerika kuna dada mmoja anajulikana kupewa fedha ili afungue mashina ya CCM Je kweli huko ughaibuni mnafungua mashina yanasaidiaje uchaguzi wa Tanzania?? Au hamna kazi za kufanya huko America? Tafuteni huduma za kuikomboa jamii ya WaTanzania maswala ya CCM na vyma waachieni waTanzania tulioko huku nyumbani, tunaelewa ziaidi na tunapata shida sana na hivi vyama ninyi hamana mnalokwazika nalo! Huyu dada anawadanganyeni na si ajabu ameahidiwa nafasi ya vitu wanavyoita maalumu !! Mhusika wa hii blog DJ LK usibane iweke ndio siasa hizo. Boreka na vijimambo..

Anonymous said...

Hiyo yote ni propaganda ya UKAWA. China inayo chama kimoja na wanasonga mbele. Unless tunataka kurudia enzi za ujamaa, In Capitalist society wachache wanakuwa Matajiri na wengi wanabaki fukara. This is true in รกll developed countries; hata marafikit zetu wa jadi WACHINA! Mr. Muganda has failed to spell out that changes from Socialism to Capiatalism to which Tanzanians so much aspire can take decades. Even then, wealth distribution will remain unequal. CCM ล‘r CHADEMA won't change that simple economic fact petaining to capitalism. The late Pres. Mwalimu Nyerere knew that fact, and that is why he stuck with Socialism till he retired and handed over the tough task to Pres. Mkapa. Unfortunately, the so-called opposition are more interested in advancing their egos than the people wishes. With รกll due respect, CCM has some short-comings but is the only proven party which can deliver and capable to positively develop Tanzania.

Jay said...

Kiukweli CCM as the sole engine of moving this country to peosperity has failed watanzania big time. Hakika kama kwelu kuna mtu yeyote mwenye akili timamu anatetea upuuzi wa CCM basi huyo mtu atakuwa ana agenda zake za kubebwa ili atafune hela za walipa kodi. Nani anaweza kuniambia mazuri ya CCM toka huko tulikotoka mpaka hapa tulipofika? Truth be told, there's nothing positive to be said. Nchi inaibiwa hivi hivi, na rais wetu anaweka viongozi wasio na uwezo (incompetent) ili wamlindie maslahi yake. CCM imeshindwa kuongoza nchi, we need a change for real.