Wananchi wakiwa wamefurika katika kituo cha kupiga kura cha Shule ya Mtoni, wilaya ya Mjini mwaka 2010.
Ilikuwa asiye na mwana abebe jiwe, kama Zainabu Ngwadani mkazi wa Mtoni Kidalu, wilaya ya Magharibi, akipiga kura huku akiwa na mtoto wake mwenye umri wa miezi mitano, katika kituo cha shule ya Mtoni mwaka 2010 Picha zote na The Nkoromo Blog.
Na Emmanuel Muganda, Washington, DC
Tanzania itafanya uchaguzi mkuu wa rais na bunge mwaka ujao 2015. Huu
utakuwa uchaguzi wenye changamoto kubwa kwa chama tawala tangu kuanzishwe mfumo
wa vyama vingi vya siasa.
Tanzania ilifanya uchaguzi wa
kwanza wa vyama vingi vya siasa mwaka 1995 na kwa sababu vyama vya siasa
vilikuwa vichanga wakati huo, chama tawala, CCM kiliibuka na ushindi ingawa kulikuwa
na ushindani mkubwa uliotolewa na Augustine Mrema, waziri wa zamani wa ulinzi
na naibu waziri mkuu chini ya utawala wa CCM. CCM pia kilishinda uchaguzi
uliofuata 2000, na uchaguzi wa 2005 kwa asilimia kubwa. Lakini katika uchaguzi
wa 2010 asilimia ya ushindi wa CCM ilianza kuporomoka na chama cha ushindani,
Chadema, kikaibuka na idadi iliyoongezeka ya wabunge na asilimia iliyopanda ya
kura alizopata mgombea wa chama hicho.
Katika chaguzi zote zilizotangulia
CCM ilikuwa na uhakika wa kushinda kwa sababu moja kubwa ya udhaifu wa vyama
vya upinzani. Sababu nyingine ilikuwa ni miundombinu za kisiasa zilizojengwa na
chama tawala tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake mwaka 1961. CCM imejenga
matawi na ofisi kila sehemu nchini kukiwa na vijijini. Kwa sababu hiyo,
wagombea wa CCM hawakuona lazima ya kujadilia masuala yaliyoikabili nchi,
badala yake wakitoa ahadi za kuboresha miundombinu, na kuleta maisha bora kwa
Watanzania wote. Na kwa sababu hiyo pia, imejengeka dhana ndani ya chama kwamba
yeyote atakayeteuliwa na chama hicho kuwa mgombea ndiye atakayekuwa rais wa
Tanzania. Lakini uchaguzi wa 2015 utakuwa ni uchaguzi wa “issues,” masuala. Na
dhana hiyo imeanza kukabiliwa na changamoto.
Suala moja kubwa katika uchaguzi
ujao litakuwa ni katiba mpya. Rasimu ya katiba iliyopendekezwa na Tume ya Jaji
Warioba ilibadilishwa na Bunge la katiba, baada ya vyama vya upinzani kujiondoa
kwenye mchakato huo na kuunda kundi la UKAWA. UKAWA inashirikisha vyama vikuu
vya upinzani, CHADEMA, CUF NA NCCFR-Mageuzi. Vyama hivi viliunga mkono muundo
wa serikali tatu kama ilivyopendekezwa na tume ya Jaji Warioba. CCM inapinga
muundo wa serikali tatu. Mbali na hayo, katiba iliyopitishwa na Bunge la katiba
ambalo wengi ni wafuasi wa CCM, imefuta pia tunu za taifa ambazo ni pamoja na
maadili ya uongozi na raia kuwa na mamlaka ya kuwaachisha kazi wabunge wao kama
hawataridhika na uongozi wao. Hii ndiyo katiba, ambayo baadhi wameipachika
jina, katiba ya Sitta na Chenge, ambayo CCM hivi sasa inaipigia chepuo. Na
katiba hii itakayokuwa suala kubwa katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Licha ya shamrashamra na mayenu
yaliyokatwa bungeni baada ya kupitishwa kwa katiba hii, mwenyekiti wa CCM, rais
Jakaya Kikwete, ameanza kutambua kwamba muitikio wa wananchi kwa katiba hii ni
mdogo sana katika maeneo aliyoyatembelea. Akizungumza hivi karibuni katika
sherehe ya kumbukumbu ya kifo cha hayati Mwalimu Julius Nyerere, rais Kikwete
alikiri wazi kwamba kunahitajika muda mrefu wa kujipanga kabla ya kutangaza
kura ya maoni na kuonyesha kuwa huenda kura ya maoni isipigwe mpaka baada ya
uchaguzi wa 2015.
“Juzi nilikuwa Mwanza nikawaeleza ila hata hawakuonyesha kuwa kuna jambo
jipya na la muhimu linawajia. Walibaki kimya. Leo pale uwanjani nyote
mumeshuhudia tukilisema na kulitilia mkazo ila wananchi walibaki kimya,
wakituangalia. Hii siyo kawaida kwa jambo nyeti kama hilo. Hata wewe mzee,
(akimtaja Sitta aliyekuwa amekaa pembeni yake) ulipotajwa na huku ni kwenu
nilitarajia shangwe za hali ya juu kutokana na kazi uliyofanya lakini ndo
wamebaki kimya. Lazima tufanye kazi ya ziada.” Alisema Kikwete.
Lakini kazi ya ziada haitakuwa
rahisi kwa CCM na viongozi wake. Tayari viongozi wa upinzani chini ya UKAWA
wameshatangaza kuanzisha kampeni za kuipinga tafsiri ya rasimu iliyotolewa na
Sitta na Chenge na kupitishwa na wabunge wa CCM. Mbali na UKAWA, mwenyekiti wa
tume iliyoandika rasimu ya katiba, Jaji Joseph Warioba, naye ametangaza
kuanzisha kampeni ya kupinga kupitishwa kwa rasimu hiyo iliyopitishwa na bunge.
Akizungumza mjini Bunda hivi karibuni, Jaji Warioba alisema kuwa katiba hiyo
haina maoni yote ya wananchi kama inavyodaiwa na Bunge maalumu. Alitaja mfano
wa pendekezo la kuwepo kwa kipengele cha maadili ya viongozi ili kuwadhibiti
dhidi ya vitendo viovu kama vile ufisadi, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
Lakini, alisema Warioba, wajumbe wa Bunge walirekebisha kifungu hicho hadi
kikapoteza maana. Warioba alizungumzia pia mfumo wa serikali tatu uliokuwa
umependekezwa katika mkusanyo wa maoni wa rasimu aliyopeleka bungeni, pia kuwapa
raia madaraka ya kuwawajibisha wabunge wao na rais kupunguziwa madaraka, mambo
ambayo yameondolewa na Bunge maalumu. Aliwashauri wananchi waisome katiba
iliyopendekezwa kwa makini kabla ya kuipigia kura.
Upinzani mwingine kwa katiba hiyo
unatoka kwa baadhi ya viongozi wa kidini. Kwa hiyo, kwa pamoja, kampeni za Jaji
Warioba, viongozi wa UKAWA na viongozi wa kidini zitakuwa na athari kubwa
katika matokeo ya kura ya maoni ya kukubali au kuikataa katiba iliyopitishwa na
Bunge maalum. Na kama katiba hii itapigiwa kura na kukataliwa kabla ya uchaguzi
wa 2015 hilo litakuwa doa kubwa kwa chama tawala ambacho kimewekeza katika
katiba ya Sitta na Chenge.
Suala jingine litakalofanya
uchaguzi wa 2015 kuwa uchaguzi tofauti na wenye msisimko, ni uamuzi wa vyama
vikubwa vya upinzani, chini ya mwavuli wa UKAWA, kusimamisha mgombea mmoja wa
urais, na kutosimamisha wagombea watakaoshindania nafasi moja katika uchaguzi
mkuu. Ikiwa uamuzi huu utazingatiwa na kutekelezwa utatoa changamoto kubwa kwa
CCM ambayo imekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka hamsini. Upinzani nchini Kenya
uliweza tu kuindoa KANU madarakani baada ya kukubaliana kuungana. Katika
uchaguzi wa 2005 mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete alishinda kwa asilimia 80.
Katika uchaguzi wa 2010 ushindi wa Kikwete ulikuwa wa asilimia 60 wakati ambapo
idadi ya wapiga kura walioshiriki katika uchaguzi kwa mara ya kwanza ilishuka
kuwa chini ya asilimia 50 ya wapiga kura waliojiandikisha.
Suala la katiba litawezesha
mjadala kuhusu mwelekeo wa nchi. Mwaka 1995 alipokuwa akimnadi Benjamin Mkapa
kuwa rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere alisema kuwa Tanzania inataka
mabadiliko, Watanzania wanataka mabadiliko. Lakini wakati huo Mwalimu hakusema
ni mabadiliko ya aina gani wanayoyataka Watanzania. Na kwa sababu upinzani
ulikuwa bado mchanga, ilionekana kuwa kwa CCM kubadilisha viongozi, mathalan,
kutoka kwa Mwinyi hadi Mkapa, na kutoka kwa Mkapa hadi Kikwete, CCM ilikuwa
inaleta au inafanya mabadiliko. Lakini hayo yalikuwa ni mabadiliko ya
personalities tu na si mabadiliko ya kimsingi.
Hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanyika kisera kati ya utawala wa Mwinyi na
Mkapa, ila kulikuwa na mabadiliko tu ya “style” au mtindo wa kutawala. Vivyo
hivyo Kikwete hakubadilisha lolote la maana kutoka utawala wa Mkapa. Katika
masuala kama vile raslimali za nchi, uwekezaji, na uwezeshaji wa Watanzania
kumiliki maliasili zao hakuna mabadiliko yoyote kati ya utawala wa Mkapa na
Kikwete. Kwa kulifanya suala la katiba kuwa suala la uchaguzi upinzani pia
utaweza kuzusha mjadala kuhusu mwelekeo wa Tanzania hasa katika uwekezaji,
maliasili, na nafasi ya Mtanzania katika mchakato mzima wa uwekezaji. Haitakuwa
rahisi kwa mgombea wa CCM katika uchaguzi wa 2015 kutoa ahadi tu za ujenzi wa
miundombinu kama alivyofanya Kikwete katika uchaguzi wa 2010. Upinzani ulioungana
utalazimika kuhakikisha kuwa CCM haitumii tena ajenda ya ujenzi wa miundombinu
kama ajenda ya uchaguzi mkuu 2015.
Tanzania inahitaji mjadala kuhusu
mwelekeo wa nchi katika uchaguzi mkuu. Raslimali za nchi zimekuwa zinapotea
kutokana na mikataba mibovu iliyowekwa na watawala. Tangu iachane na sera za
ujamaa na kujitegemea Tanzania imekuwa kama meli inayoyumbishwa baharini na
pepo za wenye nguvu duniani, si kwa kupenda, bali kwa utashi wa viongozi wa
nchi.
Mwalimu Nyerere aliposema 1995 kuwa Watanzania wanataka mabadiliko,
hakumaanisha mabadiliko ya kiongozi kumpisha mwingine. Ni mabadiliko ya
kimfumo, ambayo kama hayatafanyika, Tanzania itaendelea kulemewa na ufisadi. Ni
mabadiliko ya ruuya( vision) ambayo bila kufanyika Tanzania itaendelea kulemewa
na wimbi la matajiri wachache wakati mamilioni wakikosa huduma za kimsingi. Na
kwa hapa tulipo, ni wazi kuwa bila mjadala wa mabadiliko haya katika uchaguzi
wa 2015, Tanzania itaendelea kushuhudia wachache wakijichotea keki ya taifa
wakati walio wengi wanashindwa hata kupata mlo mmoja kwa siku.
Tanzania inataka mabadiliko.
5 comments:
๐๐๐๐๐๐๐๐ sagi sana hongera brother umenena ๐๐๐๐๐๐
Asante sana mdau. Kuubwa la msingi tu pamoja na vyama vya vitakavyoshiriki uchaguzi, CCM kusema ukweli ni wezi wakubwa wa kura nakumbuka kabisa mwaka 2010 waliwekwa watu kule Bagamoyo hotelini kwa maandalizi ya kura za wizi na kweli ilifanikiwa. Tuache kuwalaghai wananchi na kugawa pesa ambazo ni zile zile tupatazo benki na kodi za wananchi. Kugungua matawi na mashina sio tija yanafunguliwa kwa gharama yeyote ile kitu ambachjo hata vyama vinginevyo wanayo. Tumeona hata kule Amerika kuna dada mmoja anajulikana kupewa fedha ili afungue mashina ya CCM Je kweli huko ughaibuni mnafungua mashina yanasaidiaje uchaguzi wa Tanzania?? Au hamna kazi za kufanya huko America? Tafuteni huduma za kuikomboa jamii ya WaTanzania maswala ya CCM na vyma waachieni waTanzania tulioko huku nyumbani, tunaelewa ziaidi na tunapata shida sana na hivi vyama ninyi hamana mnalokwazika nalo! Huyu dada anawadanganyeni na si ajabu ameahidiwa nafasi ya vitu wanavyoita maalumu !! Mhusika wa hii blog DJ LK usibane iweke ndio siasa hizo. Boreka na vijimambo..
Asante sana mdau. Kuubwa la msingi tu pamoja na vyama vya vitakavyoshiriki uchaguzi, CCM kusema ukweli ni wezi wakubwa wa kura nakumbuka kabisa mwaka 2010 waliwekwa watu kule Bagamoyo hotelini kwa maandalizi ya kura za wizi na kweli ilifanikiwa. Tuache kuwalaghai wananchi na kugawa pesa ambazo ni zile zile tupatazo benki na kodi za wananchi. Kugungua matawi na mashina sio tija yanafunguliwa kwa gharama yeyote ile kitu ambachjo hata vyama vinginevyo wanayo. Tumeona hata kule Amerika kuna dada mmoja anajulikana kupewa fedha ili afungue mashina ya CCM Je kweli huko ughaibuni mnafungua mashina yanasaidiaje uchaguzi wa Tanzania?? Au hamna kazi za kufanya huko America? Tafuteni huduma za kuikomboa jamii ya WaTanzania maswala ya CCM na vyma waachieni waTanzania tulioko huku nyumbani, tunaelewa ziaidi na tunapata shida sana na hivi vyama ninyi hamana mnalokwazika nalo! Huyu dada anawadanganyeni na si ajabu ameahidiwa nafasi ya vitu wanavyoita maalumu !! Mhusika wa hii blog DJ LK usibane iweke ndio siasa hizo. Boreka na vijimambo..
Hiyo yote ni propaganda ya UKAWA. China inayo chama kimoja na wanasonga mbele. Unless tunataka kurudia enzi za ujamaa, In Capitalist society wachache wanakuwa Matajiri na wengi wanabaki fukara. This is true in รกll developed countries; hata marafikit zetu wa jadi WACHINA! Mr. Muganda has failed to spell out that changes from Socialism to Capiatalism to which Tanzanians so much aspire can take decades. Even then, wealth distribution will remain unequal. CCM ลr CHADEMA won't change that simple economic fact petaining to capitalism. The late Pres. Mwalimu Nyerere knew that fact, and that is why he stuck with Socialism till he retired and handed over the tough task to Pres. Mkapa. Unfortunately, the so-called opposition are more interested in advancing their egos than the people wishes. With รกll due respect, CCM has some short-comings but is the only proven party which can deliver and capable to positively develop Tanzania.
Kiukweli CCM as the sole engine of moving this country to peosperity has failed watanzania big time. Hakika kama kwelu kuna mtu yeyote mwenye akili timamu anatetea upuuzi wa CCM basi huyo mtu atakuwa ana agenda zake za kubebwa ili atafune hela za walipa kodi. Nani anaweza kuniambia mazuri ya CCM toka huko tulikotoka mpaka hapa tulipofika? Truth be told, there's nothing positive to be said. Nchi inaibiwa hivi hivi, na rais wetu anaweka viongozi wasio na uwezo (incompetent) ili wamlindie maslahi yake. CCM imeshindwa kuongoza nchi, we need a change for real.
Post a Comment