Advertisements

Sunday, October 19, 2014

TUMEWAKOSA BAHATI YAO

Kiungo wa timu ya Simba,Amri Kiemba akuchuana vikali na Mshambuliaji wa timu ya Yanga,Andrey Coutinho wakati wa mtanange wa watani wa Jadi Yanga na Simba uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.Timu hizo zimetoka sare ya bila kufungana.PICHA ZOTE NA OTHMAN MICHUZI.
Mtanange ukiendelea...
Dogo akiwachambua wana Yanga...
Jaja hakuweza fua dafu.

Dar es Salaam. Si Yanga wala Simba. Hicho ndicho unachoweza kusema baada ya miamba hiyo ya soka nchini kutoka sare ya 0-0 jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kuendeleza rekodi yake ya kutoka sare nne msimu huu, wakati Yanga wakipata sare ya kwanza.
Mchezo huo uliokuwa na ushindani na ufundi mkubwa katika muda wote ulimshuhudia kipa chipukizi wa Simba, Manyika Peter akifanya kazi kubwa kuizuia Yanga.
Manyika ambaye alichukua nafasi ya wazoefu Ivo Mapunda na Hussein Sharif ‘Cassillas’ walio majeruhi, akicheza kwa utulivu katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, alionekana muda mwingi akiwa mapumziko kutokana na mpira kuchezewa zaidi katikati ya uwanja.
Simba wakicheza kwa tahadhari na umakini walitawala sehemu kubwa ya mchezo, kipindi cha kwanza kwa kupiga pasi fupi fupi, lakini washambuliaji wake, Emmanuel Okwi na Elias Maguli walikosa umakini kwenye umaliziaji.
Yanga walionekana kujibu mapigo zaidi kwa mashambulizi ya kushtukiza kwa kutumia kasi ya Mrisho Ngassa na Andrey Coutinho kupitisha krosi kwa Jaja.
Katika mojawapo ya nafasi chache, Coutinho alipokea pasi nzuri ya Haruna Niyonzima na kupiga shuti lililodakwa na Manyika dakika ya 17.
Nusura Okwi aifungie timu yake bao katika dakika ya 30, baada ya kuwalamba chenga mabeki wa Yanga na kupiga shuti lililompita kipa Dida kabla ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kuokoa hatari hiyo.
Kocha wa Simba, Patrick Phiri alifanya mabadiliko ya mapema kwa kumtoa Said Ndemla na kumwingiza Shaban Kisiga, dakika ya 38.
Simba walirudi kipindi cha pili kwa kasi zaidi na kulishambulia lango la Yanga kama nyuki, lakini mashuti yao yalishindwa kulenga lango.
Simba walipata pigo dakika ya 59, baada ya kiungo wao, Jonas Mkude kuumia bega na kulazimika kutolewa nje na nafasi yake kuchukuliwa na Pierre Kwizera.
Hata hivyo, maumivu kwa Mkude yalionyesha udhaifu kwa upande wa watoa huduma ya kwanza ambao hawakuwa na vifaa vya kumbebea mchezaji huyo na badala yake kumlazimisha kusimama, kutembea.
Nafasi nyingine ya Simba kufunga bao ilipotea baada ya Haruna Chanongo kupokea pasi ya Okwi na kupiga shuti lililogonga mwamba, ingawa tayari mwamuzi msaidizi alishaonyesha kibendera cha kuotea kwa Chanongo.
Kocha Marcio Maximo alifanya mabadilko kipindi cha pili kwa kuwatoa Niyonzima, Jaja, Juma Abdul na kuwaingiza Simon Msuva, Hamis Kiiza na Salum Telela katika kutafuta bao.
Manyika alifanya kazi ya ziada dakika ya 76 kwa kuokoa kwa miguu shuti lililopigwa na Coutinho.
Hofu yamwingia Manyika
Mwishoni mwa mchezo huo, Manyika alisema katika mahojiano kuwa ulikuwa mtihani mkubwa kwake kucheza mechi hiyo, kiasi kwamba awali aliingiwa hofu, lakini baba yake, Peter Manyika kipa wa zamani wa Yanga alimtia nguvu.
“Nilikuwa na hofu, namshukuru baba alinitia moyo, alinituliza, ndiyo nimefanya vyema katika mchezo,” alisema.
Mashabiki wafurika U/Taifa
Nje ya dakika 90 za mchezo huo, mashabiki wengi walijitokeza mapema uwanjani hapo na kupanga mistari mirefu ili kuingia uwanjani kwa kutumia tiketi zao za kielektroniki kwa mara ya kwanza.
Jinsi timu zilivyowasili
Simba ndiyo waliotangulia kuingia uwanjani saa 9.19 alasiri, huku Yanga wakifuata wakiingia saa 9.25 na kuanza mazoezi.
Wachezaji 13 kati 18 wa Simba walikuwa wamevaa viatu vya rangi ya chungwa, wakati Owino, Kisiga na Tambwe wakivaa viatu vya njano, Singano alivaa vya bluu na Mohamed Hussein pekee akiwa navyo vyeupe.
Yanga kwa upande wao walikuwa kivutio kwa unyoaji wa nywele, hasa Mbuyu, Ngassa na Juma Abdul.
Awali, timu ya vijana ya Yanga B ilichapa Simba B kwa mabao 2-1 na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa Yanga waliofika mapema uwanjani hapo.
Yanga: Deogratius Munishi, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Genilson Santos ‘Jaja’, Mrisho Ngasa, Andrey Coutinho.
Simba: Manyika Peter, William Lucian, Mohamed Hussein, Hassan Isihaka, Joseph Owino, Jonas Mkude, Haruna Chanongo, Said Ndemla, Elias Maguli, Amri Kiemba na Emmanuel Okwi.
Mwananchi

No comments: