Advertisements

Saturday, October 25, 2014

UNAKULA UJANA, UZEE UTALIWA NA NANI?

BILA shaka wapenzi wasomaji wa safu hii mko vizuri na mko tayari kupokea mambo mapya baada ya wiki iliyopita kumaliza somo letu lililohusu mchepuko.

Tulijifunza kwamba mchepuko una madhara kwa pande zote mbili, mwanamke na mwanaume na kupata jibu la pamoja kwamba ni vyema wapendanao wakawa waaminifu kwani hakuna jipya katika mapenzi.

Wiki hii tunajadili mada mpya ambayo inahusu ujana. Ujana ni sehemu ambayo kimsingi ina changamoto nyingi tofauti na utoto na uzee. Ni ukweli usiopingika kwamba unapokuwa mtoto, ‘stress’ za maisha hauzioni kama vile unapokuwa mzee.

Ukiwa mzee, mambo mengi yanakuwa hayana nafasi kwako. Tamaa za kimwili zinakuwa hazina nafasi kubwa na badala yake unaongozwa na busara katika mambo ya msingi.
Ukijipanga na kuutumia vizuri ujana ndivyo ambavyo utaufaidi uzee wako ukiwa mzima na mwenye familia bora.

Wengi wamekuwa wakichanga karata vibaya katika eneo hili na kujikuta wakipoteza uelekeo uzeeni kwao.Tatizo la kuchanga karata vizuri ujanani, lina athari kubwa zaidi kwa wanawake. Kimsingi maumbile ndiyo yanayoonekana kuwaponza zaidi wanawake tofauti na wanaume.

Inaaminika kwamba wanawake wanapouchezea ujana athari zao zinakuwa kubwa zaidi tofauti na wanaume, kutokana na maumbile yao.Ni rahisi uzeeni wakakosa soko kwa sababu mazingira yanaonesha mwanaume ndiye mwenye fursa ya kumuanza mwanamke hivyo kujikuta amepoteza soko haraka.

Binti anatumika pasipo kujistiri heshima yake, anaishi katika maisha ya kutojali kesho yake na pindi atakapokuja kufikiria suala la heshima yake, umri tayari unakuwa umemtupa mkono na hakuna ambaye anataka kumuoa.

Hapo ndipo unawasikia waoaji wakitoa kauli za kukudharau kama: “kashatumika sana.” Kauli hizo ndizo zinazokuwa mwiba kwa mabinti na kuona soko lao limefika ukingoni.
Mabinti wengi wanapofika katika steji hiyo ndipo pale wanapokuwa hodari wa misemo mingi ya kutiana moyo. Utasikia “kuolewa ni bahati mwaya, ukipangiwa kuolewa, utaolewa na kama hujapangiwa basi hautaolewa ng’o.”

Hapo anasahau kabisa kwamba safari ya kuelekea kwenye ndoa inahitaji maandalizi na misingi thabiti ili aweze kufikia kwenye kilele cha kuishi na familia; baba mama na watoto.
Ujana anautumia wee kama alivyoimba msanii wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’. Fasheni zote za mjini unazijua wewe, haupitwi na kitu kipya.

Kwenye kipindi hicho binti anakutana na changamoto nyingi ambazo kimsingi huchangia kumfanya azeeke kabla ya umri. Hapo ndipo zinapoibuka mimba kibao zisizotarajiwa. Kwa kupenda starehe za ujana, hawezi kuzaa, anaichoropoa mimba. Yawezekana pia akapata nyingine, nayo akaitoa.
Itakuwa ni mwendo wa kutoa ili aonekane msichana kila siku. Kumbe anazeeka hajijui.

Mwili wake ni rahisi sana kuchoka kutokana na vitendo hivyo. Nguvu ya ujana inamfanya leo awe na mwanaume huyu kwa kigezo fulani kesho anahamia kwa mwingine kwa kufuata kitu fulani ambacho wa awali hakuwa nacho.

Atahama kutoka kwa asiyekuwa na gari, atakwenda kwa mwenye gari ili aweze kutanua naye katika sehemu mbalimbali za starehe mwisho wa siku anaambulia maumivu maana huyo mwenye gari naye anakuwa anaona na kutamani wengi wa barabarani.

Itaendelea wiki ijayo.

GPL

No comments: