Advertisements

Saturday, October 25, 2014

Wabunge wamtia moyo Nyalandu kuhusu shutuma

Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu akizungumza na Mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki ,Joshua Nassar walipokutana katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha

Wabunge wa Kanda ya Kaskazini wamemtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, kutovunjika moyo kutokana na kauli za baadhi ya watu wanaoushutumu utendaji wake.

Wakizungumza katika mkutano wa viongozi wa mikoa ya Arusha na Kilimanajaro, wabunge hao wamesema wanaomuandama wana kinyongo na utendaji wake.

Wabunge hao ni Aggrey Mwanri wa Siha na Joshua Nassari wa Arumeru Mashariki, ambao walimpongeza kwa hatua anazochukua kwa kulinda maliasili na kupambana na ujangili na kumtaka aongeze bidiii. “Usife moyo kwa kuwa tunajua unafanya kazi zako vizuri kwa manufaa ya taifa, ukiona wanakurushia mawe, usifadhaike.Ndiyo wanakuongezea nguvu za kuweza kuongoza,” alisema Mwanri.

Alimpongeza kwa kuja na wazo la kuundwa kwa mfuko wa Uhifadhi wa Milima Kilimanjaro na Meru na kusema kuwa hiyo itasaidia wananchi kwani utalii utaongezeka na uhifadhi wa mazingira utakuwa bora zaidi.

“Nazungumza hivi sio kwamba nataka kujipendekeza kwako, kwani hapa nilipo ninahitaji nini zaidi? Lazima kusema ukweli na sio kuzushiana,” alisema.

Mbunge wa Arumeru Mashariki, Nassari alisema amekuwa akifuatilia utendaji wa waziri huyo na kupata faraja jinsi anavyoshughulikia masuala ya maliasili.

“Naomba kukutia moyo kwani anayefanya kazi ya Mungu atapata nguvu, nikisikia mtu bungeni anasema wewe ni waziri mzigo, mimi nitaruka juu na kumwangukia vibaya,” alisema.

Alisema kwa waziri kuchukua uzito wa kuanzisha mfuko wa kuhifadhi milima hiyo ni hatua muhimu kwa wananchi wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ambao wamekuwa wakitegemea milima hiyo kwa ajili ya utalii.

Kwa upande wake Nyalandu alisema kwa kasi iliyopo sasa watu kutumia vibaya bidhaa zitokanazo na misitu, baada ya miaka 15 kuna wasiwasi nchi ikawa jangwa kama hatua za haraka hazijachukuliwa.

“Milima hii ndio imekuwa chanzo cha maji kwa wananchi wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro lakini kwa kasi ya ukataji miti kwa matumizi ya nyumbani imekuwa trishio kwani hadi sasa hivi barafu katika mlima Kilimanjaro imepungua kwa kiasi kikubwa” alisema Nyalandu.

Nyalandu alisema kasi ya ukataji miti nchini imekuwa kubwa kwa sasa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na kuwa kwa mwaka mmoja pekee hekta 350,000 hukatwa huku kikiwa hakuna jitihada za kurejesha iliyoondolewa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: