Advertisements

Thursday, November 27, 2014

EMERSON AANZA KUJIFUA YANGA

Kiungo Mbrazil Emerson de Oliveira (wa pili kutoka kulia) akiwa mazoezini leo asubuhi katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola, Dar. Wengine ni Hamis Kiiza, Hussein Javu na Coutinho. (Picha na Yanga SC)

BAADA ya kuwasili jana kutoka nchini Brazil, kiungo mkabaji Emerson de Oliveira Neves Roque leo ameanza mazoezi mepesi asubuhi katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola jijini Dar es Salaam kufuatia kusaifri kwa zaidi ya masaa 11 kutoka jijini Rio de Janeiro.

Emerson ameungana na wachezaji wengine wa Yanga katika mazoezi ya leo asubuhi ikiwa ni siku yake ya kwanza katika ardhi ya Tanzania na kufanya mazoezi mepesi mepesi chini ya kocha msaidizi Leonardo Neiva kuijiweka fit na kutoa uchovu wa safari.

Kiungo huyo mwenye umbo lililonyumbulika ambae alikuwa akichezea timu ya Bonsucesso FC iliyopo ligi daraja la pili nchini Brazi katika jiji la Rio de Janeiro pia msimu uliopita alikuwa akicheza soka la kulipwa katika nchi ya Poland kwenye klabu ya Piotrkow Trybunalski FC.

Kocha Mkuu wa Yanga, Marcio Maximo amesema mchezaji huyo leo alikuwa na programu ya mazoezi mepesi tu kutokana na uchovu wa safari na kesho anatarajiwa kuendelea na mazoezi na wenzake kulingana na ratiba iliyopo.

Endapo Emerson atafanikiwa kulishawishi benchi la ufundi kumsajili basi moja kwa moja ataingia makubaliano na klabu hiyo kwa ajili ya kuitumikia kwenye michuano ya kimataifa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

No comments: