Dodoma. Hali ni tete. Ndiyo neno ambalo unaweza kulizungumza kuhusu kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Mji wa Dodoma tangu juzi umejaa pilikapilika zikiambatana na mikutano iliyokuwa ikijadili kashfa hiyo.
Kamati ya Uongozi wa Bunge, Kamati ya Uongozi wa Wabunge wa CCM, Baraza la Mawaziri, kwa nyakati tofauti walikaa kujadili ripoti ya escrow ambayo inatarajiwa kujadiliwa na Bunge Jumatano na Alhamisi.
Leo kikao cha wabunge wa CCM kinatarajiwa kufanyika kujadili suala hilo. Wabunge walionekana kila kona ya Viwanja vya Bunge jana wakijadiliana katika vikundi kuhusu sakata la escrow, huku wengine wakitaka hata miswada yote iliyobaki isijadiliwe ili kutoa nafasi kuichambua kwa kina kashfa hiyo.
Wabunge wa kila vyama wamekuwa wakikutana kuweka misimamo yao kuhusu namna watakavyoshiriki kujadili ripoti hiyo.
Wabunge wa CCM wamegawanyika katika makundi matatu; linaloshinikiza waliohusika na wizi huo wajiuzulu, kundi la watu wasiokuwa na msimamo na kundi linalotaka ripoti isijadiliwe bungeni.
Kikao cha Kamati ya Uongozi kilichofanyika jana asubuhi kilikubaliana suala hilo la escrow lijadiliwe kwa siku mbili badala ya moja iliyokuwa imepangwa awali.
Kamati ya Uongozi CCM
Katika kikao cha Kamati ya Uongozi wa Wabunge wa CCM, wabunge wawili akiwemo Naibu Spika, Job Ndugai walipewa kibano kuhusiana na matamshi yao kuhusu sakata hilo.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zinaeleza kuwa waliokumbana na kibano hicho ni Mbunge wa Kahama, James Lembeli na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya, ambao waliambiwa kwamba matamshi yao wakati wakichangia yalilenga kukifanya chama hicho kuonekana kuwa ni cha wezi.
“Ndugai yeye walimbana kwa nini aliruhusu mjadala huo bungeni,” alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.
Aidha, baadhi ya wabunge wana hofu kuwa mjadala huo huenda usiende bungeni.
“Kuna taarifa kuwa Serikali bado haitaki mjadala huu uingie bungeni na wanamtumia Spika Anne Makinda kuukwamisha. Sisi hatuwezi kukubali uzuiwe kujadiliwa tutapiga kura za kutokuwa na imani naye iwapo atajaribu kufanya hivyo,” alisema mmoja wa wabunge kutoka Kanda ya Kati.
Alisema taarifa hizo zinakuja siku chache baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa mahakama inataka kuzuia mjadala huo usiingie bungeni.
Habari zaidi kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alitoa msimamo mkali kuhusu sakata hilo la escrow na kwamba ametaka hatua zichukuliwe kwa wahusika wote.
Katika kikao hicho inaelezwa kwamba Nchemba alionyesha msimamo wake waziwazi kuwa sakata hilo ni hujuma na kwamba haiwezekani walioiba fedha hizo wakaachiwa tu hivihivi.
Ndani ya kikao hicho imeelezwa kuwa Mwigulu alijitokeza na kusema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameshamaliza utata hivyo, mali zote, fedha zote za IPTL zikamatwe na wahusika wote wakamatwe.
Alisema haiwezekani watu wakawajibika tu kwa kujiuzulu kwa kuwa huko ni kutoa tu likizo mtu akale mabilioni yake, hivyo wachukuliwe hatua ipasavyo na kufilisiwa.
“CAG ameshasema pesa zile zilikuwa mali ya umma, sasa zikamatwe zote na wahusika wote wakamatwe,” alisema Mwigulu.
Chanzo chetu cha habari kilieleza kuwa Mwigulu alienda mbali zaidi na kusema hata ambao walishastaafu na wamehusika kulihujumu taifa wakamatwe na akaunti zao zikamatwe, zifilisiwe na fedha zirudishwe kwa wananchi.
Pia aliagiza mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambaye anatuhumiwa kuchota Sh1.6 bilioni za akaunti hiyo afukuzwe kazi, akamatwe na akaunti zake za fedha zifilisiwe ili fedha irudi serikalini.
Habari za uhakika kutoka kikao hicho zinaeleza kuwa Mwigulu aliongea kwa sauti ya mamlaka mbele ya Waziri Mkuu na kusema kuwa kujiuzulu siyo adhabu stahiki kwa wizi mkubwa kama huo.
Mwigulu alisema: “Tazama wanafunzi, watoto wa maskini zaidi ya elfu 40 wamekosa mikopo, madawa hospitalini hakuna, maskini wanakufa, watu wasio na hatia wanafungwa kwa kukosa michango ya maabara, walimu wanadai fedha zao, wazabuni wanauziwa nyumba zao na benki huku wakiidai Serikali kwa huduma walizotoa, leo wezi tuwape adhabu ya kujiuzulu? Tuwape likizo ya kwenda kutumia fedha walizo waibia maskini?”
Kwa mtumishi wa TRA aliyekula fedha za IPTL zaidi ya 1.6 bilioni Mwigulu akatoa agizo:
“Nimemwagiza Kamishna wa Kodi amfukuze kazi yule mtumishi wa TRA iliyoko chini ya wizara yangu na afilisiwe, pia mitambo na kodi vikamatwe na wahusika wakamatwe.
“Hatuwezi kuendeleza mazoea ya kufunga maskini na kuwapa likizo wezi wakatumie fedha. Walio serikalini na walioko kwenye siasa wakamatwe na tuwafilisi fedha irudi serikalini,” Mwigulu alisisitiza.
Wapinzani wadai ripoti imechakachuliwa
Kambi Rasmi ya Upinzan Bungeni, imedai kuwa watu wanaotuhumiwa kuhusika na uchotaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, wamenyofoa baadhi ya nyaraka katika ripoti ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Ofisi ya Katibu wa Bunge.
Wakizungumza mjini Dodoma jana, viongozi hao walisema watuhumiwa wamekuwa wakisambaza nyaraka hizo feki maeneo mbalimbali ili kuzima mjadala wa wizi huo usiingie bungeni.
“ Wanatoa nakala na kuzisambaza mtaani wakiwaaminisha watu kuwa ripoti haina kitu, hivyo hakuna haja ya kupeleka bungeni kujadiliwa,”alisema Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika.
Alisema kutokana na kubaini njama hizo, kambi ya upinzani imetoa taarifa kwa Katibu wa Bunge na tayari mtu mmoja amekamatwa akihusishwa na upatikanaji na usambazi wa ripoti hiyo.
“Sisi tumeshuhudia akikamatwa mtu huyo aliyekuwa na nyaraka hizo, tunaliomba Jeshi la Polisi kuchunguza kwa kina na kumhoji uhusiano wake na watu wanaotuhumiwa katika ripoti hiyo,”alisema Mnyika
Kwa upande wake, Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia alitaja kurasa zilizonyofolewa katika ripoti hiyo kuwa ni zilizobeba mambo ya msingi ambazo ni ukurasa wa 57, 58 na 59.
“Tutaitisha kikao cha dharura kabla ya Jumatatu ili kushinikiza mjadala huu ufanyike kabla ya mambo mengine kwanza,”alisema Mbatia.
Mbatia alimuonya Spika wa Bunge, Anne Makinda kutojaribu kuuzuia mjadala, ili kuepusha machafuko kama yaliyotokea katika nchi nyingine duniani.
Naye Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Rajab Mbarouk Mohamed, aliwataka wananchi watakaoziona ama kupewa nakala za ripoti hiyo kufikisha katika vyombo vya sheria.
“Wananchi wasiwe na wasiwasi sisi tuko imara katika kuhakikisha haki inatendeka, watuhumiwa wanakamatwa, wanafikishwa mahakamani na kurejesha fedha walizochukua,”alisema.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment