ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 19, 2014

Kibadeni astaafu rasmi ukocha

Kocha wa zamani wa Simba na Ashanti United, zote za jijini Dar es Salaam, Abdallah 'King' Kibadeni, ametangaza kuachana rasmi na kazi hiyo na kuamua kuanzisha kituo cha kulelea vijana wenye vipaji vya michezo 'spoti akademi'.

Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Kibadeni mwenye rekodi pekee ya kufunga mabao matatu katika mechi moja (hat-trick) inayohusisha watani wa jadi, Simba na Yanga, alisema amechukua uamuzi wa kuachana na ukocha ili kuepuka malumbano na kuzongwa na viongozi pindi timu inapokuwa na matokeo yasiyoridhisha.

"Nipo hapa Sinza (Dar es Salaam), nilifanyiwa 'operation' (upasuaji) ya jicho tarehe 6 mwezi huu (Novemba). Nina mipango maalum ya kujenga akademi Chanika. Akademi hiyo itaitwa KISA yaani Kibadeni Soccer Academy ambayo pia itakuwa na michezo mingine mbali na soka.

"Itakuwa na vijana wenye umri kuanzia miaka 12 hadi 18 na nitaiendesha pamoja na watu wengine akiwamo kaka yangu. Tutakuwa na timu pia yenye vijana wenye umri usiozidi miaka 23," Kibadeni alisema.


"Nitakuwa ninasaka vijana wenye vipaji na kulea wale ambao nitaletewa na klabu. Kwa elimu yangu ninaona kuna umuhimu wa kufanya hivyo maana Taifa limenisaidia kusoma sehemu mbalimbali, nina elimu ya kutosha kwa sasa. Ninaona sihitaji kulumbana na viongozi wa timu nikiwa kama kocha. Bora nifanye shughuli nyingine.

"Eneo nililonalo linatosha kujenga hata viwanja viwili vikubwa kwa ajili ya soka, mpira wa kikapu na michezo mingine. Ninamuomba Mungu anijalie nipone haraka niendeleze mpango huu."

Kabla ya kutua Ashanti United mzunguko wa pili msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Kibadeni aliiongoza Simba mzunguko wa kwanza akiwa kocha mkuu lakini akatimuliwa kibabe pamoja na aliyekuwa msaidizi wake, Jamhuri Kihwelu 'Julio', timu hiyo ya Msimbazi ikiwa nafasi ya nne katika msimamo wa VPL ikizidiwa pointi nne tu na waliokuwa vinara wa msimamo, Yanga.

Baadaye aliletwa kocha Mcroatia Zdravko Logarusic ambaye alishinda mechi tatu tu mzunguko wa pili huku timu ikifungwa na JKT Ruvu, Azam, Mgambo Shooting, Coastal na Ashanti United kabla ya kutimuliwa Agosti 10, mwaka huu ikiwa ni saa chache baada ya Simba kulala 3-0 nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya Zesco ya Ligi Kuu ya Zambia.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: