Advertisements

Monday, November 24, 2014

MACHUNGU YA UFISADI WA ESCROW YAANZA KUONEKANA ,SHILINGI YATANZANIA YASHUKA RASMI,SOMA HAPA KUJUA.


Dar es Salaam. Hatua ya wahisani kuzuia Sh1 trilioni za misaada ya kibajeti kwa Serikali kutokana na kashfa ya IPTL na wasiwasi wa Uchaguzi Mkuu mwakani, ni miongoni mwa sababu za kuporomoka kwa kasi thamani ya Shilingi nchini, imefahamika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wiki iliyopita, wasomi na wadau wa biashara nchini walisema sababu nyingine ni uagizaji na uuzaji bidhaa nje ya nchi.
Kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Januari 2, mwaka huu, Dola moja ya Marekani ilikuwa ikiuzwa kwa Sh1,586 lakini sasa imepanda hadi Sh1,745. Ikumbukwe kuwa katikati ya mwaka huu, Dola moja ilikuwa ikinunuliwa kwa hadi Sh1,800 katika baadhi ya benki na maduka ya kubadilishia fedha, jambo lililoongeza gharama za ufanyaji biashara na kuongeza bei ya bidhaa.
Escrow
Hivi karibuni, wahisani walitangaza kusimamisha misaada hadi Serikali itakapopitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow na kuchukua hatua.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Prosper Ngowi alisema hatua iliyochukuliwa na nchi wahisani ya kuzuia fedha za misaada hiyo ambazo zingeingia katika mzunguko wa fedha, imesababisha upungufu wa Dola katika soko la fedha, hivyo kuongezeka thamani.
Alisema iwapo fedha hizo zingekuwa kwenye mzunguko, zingesaidia kupunguza uhaba wa Dola uliopo ambao umesababisha kuuzwa kwa bei kubwa na hivyo kuchangia kupandisha thamani ya Shilingi.
“Hata kitendo cha Tanzania kuuza bidhaa chache nje ya nchi kimechangia mahitaji ya Dola kuongezeka kutokana na uhaba wa fedha hizo hapa nchini,” alisema Dk Ngowi akitaja sababu nyingine ya kuporomoka kwa Shilingi.
Hoja ya Dk Ngowi iliungwa mkono na Meneja wa Fedha wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Mshindo Ibrahim akisema kuzuiwa kwa fedha hizo za hisani, kumechangia kupaisha thamani ya Dola, licha ya kuwapo tatizo la kuuza bidhaa kidogo nje ya nchi.
“Sisi ni waagizaji wakubwa wa bidhaa kuliko kuuza nje, tunajikuta tunapata Dola kidogo kuliko mahitaji jambo linaloiongeza thamani yake, lakini hili la wahisani kushikilia fedha za bajeti kutokana na sakata la IPTL ni moja ya sababu kubwa kwa sasa,” alisema Ibrahim.
Iwapo wahisani ambao hutoa fedha zao kwa sarafu za kigeni wataziachia, mtaalamu huyo alisema zitasaidia kupunguza wingi wa Shilingi kwa kuwa Dola hizo zinatakiwa kubadilishwa kwa sarafu ya ndani ili zianze kutumika.
Alisema kuna wakati hali hiyo ni kawaida kibiashara.
atika hatua nyingine, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Dhamana na Uwekezaji ya Zan Securities, Raphael Masumbuko alisema safari hii Shilingi imeshuka thamani kwa kasi isiyo ya kawaida tofauti na miaka ya nyuma, jambo ambalo linaweza kuchangiwa na homa ya uchaguzi.
“Huenda imetokea kwa sababu tunaelekea katika kipindi cha uchaguzi. Katika kipindi kama hiki, wawekezaji wengi kutoka nje huwa wanahifadhi fedha zao katika Dola ili kujiokoa na hasara iwapo utatokea mfumuko wa bei wakati wa mchakato wa uchaguzi,” alisema Masumbuko.
Alisema Shilingi pia imeshuka thamani kutokana na Dola kutumika mno katika sekta ya nyumba na msimu huu ni wa kulipa kodi, hivyo Dola inahitajika zaidi kuliko Shilingi.
“Nyumba nyingi siku hizi zinakodishwa kwa Dola wanaita ‘mita ya mraba kwa Dola’ hadi majumba yanayomilikiwa na mifuko ya hifadhi za jamii… sasa kwa hali hii usitegemee Shilingi itapanda thamani,” alisema Masumbuko.
Hata hivyo, alisema hali hii haitakiwi kutia hofu Watanzania kwa kuwa inaweza kutengamaa baada ya msimu wa baridi kuanza Ulaya ambako watalii wengi watakuja na kuleta fedha za kigeni, pia juzi, BoT imeuza dhamana zitakazoipunguza Shilingi sokoni.
Mkuu wa Kitivo cha Biashara cha Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, Deogratius Massawe alisema kuongezeka kwa bidhaa mbalimbali nchini zinazonunuliwa kwa Dola pia kumechangia thamani ya fedha hiyo kuongezeka huku Shilingi ikishuka.
Massawe alisema mfumo huo unawalazimisha Watanzania kununua bidhaa hizo kwa bei ya juu zaidi tofauti na ile inayouzwa kwa Shilingi.
“Hata hivyo, ipo sheria inayomzuia mtu kumlazimisha mwingine kununua kitu chochote kwa Dola, ila mteja anaweza kununua bidhaa kwa Dola iwapo wamekubaliana na muuzaji.”
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Benjamin Mutagwaba alisema sera makini ndizo zinazoweza kuinusuru thamani ya Shilingi ya nchi hii.
“Kama kutakuwa na usimamizi mzuri, kilimo pekee kinaweza kuleta mapinduzi katika biashara na kubadili thamani ya kubadili fedha. Kama mazao yote yataongezwa thamani kabla hayajauzwa nje, nchi itapata fedha nyingi… unaweza ukaona hata madini tunayasafirisha yakiwa hayajaongezwa thamani, jambo ambalo si zuri kwa mustakabali wetu kiuchumi kama nchi,” alisema Profesa Mutagwaba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya KPMG, David Gachewa alisema hakuna njia ya mkato wa kuifanya Shilingi iwe na thamani kama si kuongeza uuzaji wa bidhaa nje ya nchi.

“Miaka 10 iliyopita thamani ya Dola moja ya Marekani ilikuwa Sh800 lakini leo hii ni Sh1,700 na bado tunaagiza bidhaa zilezile kwa sarafu hiyo. Hii inamaanisha kuwa gharama za bidhaa hizo zimeongezeka na mwananchi ndiye anayelipia. Hali hii itaendelea kama hakutakuwa na mabadiliko ya kiuchumi ili kuongeza uuzaji wa bidhaa nje ya nchi,” alisema Gachewa na kuongeza:
“Nadhani mafuta na gesi yatakapoanza kuzalishwa hapa nchini na kusafirishwa kwenda nje itasaidia kwa kiasi kwa kuwa Serikali itaokoa fedha zilizokuwa zinatumika kuagiza nishati hizo, pia kuna fedha zitakazoingia kutokana na mauzo ya bidhaa hizo.”

Kauli ya waziri
Akijibu swali la Cecilia Pareso (Chadema - Viti Maalumu) wiki iliyopita bungeni, kuhusu kuongezeka kwa matumizi ya fedha za kigeni nchini, Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima alisema linapunguza ufanisi wa sera za fedha na uwezo wa BoT kutimiza wajibu wake kuwa mkopeshaji wa mwisho katika uchumi.
Malima aliongeza kuwa endapo wananchi watalazimika kutumia fedha za kigeni, jambo hilo pia linaweza kuwa kero kwao kwa kuwasababishia usumbufu.
Hata hivyo, Malima alisema kiwango cha matumizi ya Dola nchini hakijafikia kiasi cha kuwa na madhara hayo.
Alisema uwiano wa amana za fedha za kigeni na ujazo wa fedha, ambao uliwahi kupanda hadi kufikia asilimia 34 mwaka 2003, kwa sasa umeshuka mpaka kufikia asilimia 27.2 mwaka 2013.
Alisema mwaka 2007, Serikali ilitoa tamko rasmi kuhusu matumizi ya fedha za kigeni katika kulipia huduma na bidhaa katika soko la ndani kuwa Mtanzania yeyote asilazimishwe kulipia huduma au bidhaa yoyote kwa fedha za kigeni.
Baada ya agizo hilo, Malima alisema fedha za kigeni zinazotunzwa na BoT ziliongezeka kutoka Dola 228.3 milioni mwaka 1993 sawa na asilimia sita ya Pato la Taifa hadi Dola 4 bilioni sawa na asilimia 14 ya Pato la Taifa mwaka 2012

1 comment:

Anonymous said...

Asante wadau hii ndio kazi na uongozi wa serikali ya CCM wa TANZANIA tujiandae kuwa na hali ngumu saaaaana kwa kuichagua CCM kuendelea madarakani tumekwisha!!Hakuna mjadala haya ndio wanayotaka fedha ziwepo mikononi ili wasambaze rushwa!! Achieni ngazi> Wapinzani mnazo sera za ukombozi UKAWA kazeni mwendo!