ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 6, 2014

Mke wa Pinda azungumzia urais wa mumewe 2015

Mke wa Waziri Mkuu, Tunu Pinda

Mke wa Waziri Mkuu, Tunu Pinda, amesema bado hajashirikishwa na mume wake Mizengo Pinda, kuhusu nia ya kiongozi huyo wa serikali kutaka kuwania nafasi ya urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu ujao mwakani.

Akizungumza katika mahojiano maalum na NIPASHE jijini Dar es Salaam, Tunu alisema mume wake bado hajatangaza rasmi nia yake ya kugombea nafasi hiyo kubwa nchini mwakani.

Alisema Pinda hajawahi kukaa na familia yake na kuwaeleza kama ana mpango wa kujitosa katika kinyang'anyiro cha nafasi ya urais au la.

“Mume wangu bado hajatangaza rasmi nia ya kugombea urais, hata yule mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza –BBC (Salim Kikeke), alimlazimisha tu, akasema yumo katika mbio hizo kimyakimya, lakini hakuweka wazi suala hilo, hivyo bado halijawa rasmi,” alisema Mama Pinda.

"Familia kwa maana ya mimi ‘baby’ (mke) wake na watoto bado hajatuambia lolote kwa sasa kuhusu suala hilo.

“Lakini kama Watanzania na wanadamu, lazima tufahamu kwamba urais wa nchi ni baraka kutoka kwa Mungu. Familia yangu ni waumini wazuri wa dini, Biblia inaeleza namna wafalme walivyokuwa wanaoongoza. Kama mfalme hajapata thawabu kutoka kwa Mungu, ilikuwa ngumu kuongoza. Ndivyo ilivyo kwa nafasi ya urais wa nchi.

“Kama ‘baby’ (Pinda), ataamua kutangaza rasmi nia ya kuwania urais, ni jambo jema kwani mwisho wa stori maamuzi ya Mungu ndiyo yatakayotoa Rais wa Tanzania,” alisema Tunu na kuongeza:

"Na hata asipofanikiwa kupata fursa hiyo, sitalalamika kwa nini Sanula amepata, mume wangu amekosa. Ninaamini watajitokeza zaidi ya 50 kuwania nafasi hiyo, lakini Mungu ndiye atatuchagulia kiongozi.”

Oktoba 21, mwaka huu akiwa katika ziara ya kikazi jijini London, Uingereza, Waziri Pinda katika mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya BBC, alisema yumo katika mbio za kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu mwakani ingawa mbio zake ni za kimyakimya.

Kauli hiyo ya Pinda iliondoa uvumi ambao ulikuwapo kwa takriban miezi mitatu iliyopita kwamba naye ameingia katika kinyang’anyiro hicho.

Pinda aliweka wazi nia ya kuelekea Ikulu, lakini akasisitiza kuwa hajatangaza rasmi ingawa ameanza harakati hizo ‘kimyakimya’.

“Mikoba ya Rais (Jakaya) Kikwete inaweza kuchukuliwa na yeyote atakayeonekana mwisho wa safari kwa utaratibu wa chama na ndani ya Serikali yenyewe, kwamba anafaa. Waliojitokeza sasa ni wengi … basi tukubali hilo na yeye (Pinda) yumo,” alisema Pinda baada ya kuulizwa kama ni miongoni mwa wanaotaka kurithi mikoba JK mwakani.

KAULI YA PINDA JIJINI MWANZA
Agosti 24, mwaka huu, magazeti mengi ya kila siku yaliripoti kuhusu nia ya Pinda kutaka kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Magazeti hayo yalimkariri Pinda akitangaza nia hiyo usiku Agosti 22, mwaka huu Ikulu ndogo ya Jiji la Mwanza, wakati wa kikao alichowaalika wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM toka mikoa sita ya Kanda ya Ziwa.

Habari hizo zilieleza kuwa Waziri Mkuu aliwaalika wajumbe tisa kutoka katika wilaya zote za mikoa ya Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita na Kagera.

Pinda aliyekuwa jijini Mwanza kwa ajili ya kuendesha harambee ya Mfuko wa Taasisi ya Benjamin Mkapa iliyofanyika usiku wa Agosti 23, mwaka huu, alikutana kwa ‘mafungu’ na wajumbe zaidi ya 50 kutoka Mara, baadhi toka Mwanza, Geita na Kagera.

Habari hizo zilieleza kwamba miongoni mwa sababu zilizomfanya Pinda ajiitose katika kinyang'anyiro cha urais, ni kutokana na ushawishi mkubwa kutoka kwa maaskofu, masheikh, baadhi ya wabunge na watu maarufu.

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, alikuwa wa kwanza kutangaza nia ya kuwania urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwa Uingereza kabla ya Pinda kufanya hivyo.

Makamba alitangaza nia ya kuwania nafasi hiyo kupitia CCM hiyo Julai 2, mwaka huu alipokuwa Uingereza katika mkutano wa sekta ya mawasiliano baada ya kuhojiwa kwenye kipindi hicho hicho cha Dira ya Dunia cha BBC.

Weingine waliokwishatangaza nia hiyo ni Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangallah na Naibu waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya, wameshasema kuwa watakuwa tayari kujitosa kuomba uteuzi wa chama tawala kuwania nafasi hiyo ikiwa wataombwa na wananchi kufanya hivyo.

Makada wengine wa CCM ambao wanatajwa kuwa watagombea nafasi hiyo ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta; Mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Mahusiano), Stephen Wassira na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Hata hivyo, Sumaye, Lowassa, Wassira, Membe, Makamba na Ngeleja Februari mwaka huu walihojiwa na kupewa adhabu ya miezi sita kutogombea nafasi yoyote ndani ya chama tawala kutokana na kubainika kuanza kampeni kabla ya wakati kinyume cha kanuni na taratibu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: