Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungungumza na Askofu Mpya wa Dayosisi ya Centra Tanganyika, Dk Dickson Chilongani (kulia) na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglican Tanzania , Dk Jacob Chimeledya baada ya kumalizika kwa ibada ya kumweka wakfu Askofu Chilongani iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Anglican mjini Dodoma, jana. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Dodoma. Serikali imeunda timu ya watu 10 kutoka kada tofauti wakiwamo viongozi wa dini ambao watapewa jukumu la kufanya kazi ya usuluhishi kwenye vijiji vyenye migogoro baina ya wafugaji na wakulima wilayani Kiteto mkoani Manyara.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema hayo jana wakati akiwasilisha salamu za Serikali kwenye ibada ya kumweka wakfu Askofu wa sita wa Dayosisi ya Central Tanganyika ya Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Dickson Chilongani iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu, mjini Dodoma.
Pinda ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete aliyeko nje ya nchi kwa matibabu, alisema, “Hali ya Kiteto ni changamoto kama alivyosema Askofu Mkuu, Dk Chimeledya lakini inahitaji ufumbuzi kutoka kwa wadau tofauti na siyo Serikali peke yake... inataka Serikali, wananchi, vyombo vya dola, pia na kanisa lazima lihusishwe ili kujenga upya maadili ya jamii.
“Ukiwa na kundi kubwa la watu ambao hawamwogopi Mungu ni tatizo. Hii ndiyo iliyoko kule. Watu wanauana kwa sababu ya hasira, ni hasira gani hiyo inayokufanya usiogope kutoa roho ya mwenzako,” alihoji.
Pinda alisema timu itakayoundwa itapewa jukumu la kufanya usuluhishi na kupata maridhiano kijiji kwa kijiji huku ikipeleka ujumbe wa amani.
“Tunataka kutumia Kiteto kama mradi wa majaribio kwenye suala la kutafuta amani kwenye maeneo kama haya,” alisema.
Wilaya ya Kiteto inaingiliana na mikoa mitano ambayo ni Tanga (Kilindi), Morogoro (Gairo); Dodoma (Kongwa) Manyara (Simanjiro) na Arusha (Monduli) hali ambayo inachangia kuwapo na mwingiliano mkubwa wa kijamii. Hatua nyingine zitakazochukuliwa na Serikali ni kupima ardhi inayogombewa yenye ukubwa wa hekta 133,000 na kuigawa kwa wafugaji ili wafuge kwa mtindo wa ranchi na inayobakia igawiwe kwa wakulima.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment