Advertisements

Sunday, November 23, 2014

TAMBUENI JUHUDI ZETU KUZUIA UKATILI DHIDI YA WALEMAVU WA NGOZI-TANZANIA

Na Mwandishi Maalum, New York

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  imesisitiza haja na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa ya kutambua mchango unaofanywa na serikali   wa kukabiliana na vitendo vya kikatili  dhidi ya  wananchi  wake  wenye  matatizo  ya   ulemavu wa ngozi ( albino)
Wito huo  wa Tanzania umetolewa  mapema  wiki hii ( Jumanne) wakati   Wajumbe wa Kamati ya Tatu ya  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  walipopitisha kwa  kupiga kura,  Azimio  linalotaka   Juni    13 ya  kila mwaka iwe ni   siku ya Kimataifa ya  kuwatambua watu wenye ulemavu wa ngozi.
 Balozi wa Somalia kutoka Geneva  ambako ndiko chimbuko la Azimio  hilo, ndiye aliyeongoza mchakato mzima wa uwasilishaji wa  azimio  katika Kamati ya Tatu   inayohusika na masuala ya Haki za Binadamu,  Jamii na  Utamaduni.
Tanzania  ikiwa  ni   mjumbe wa Kamati  hiyo ya Tatu, pamoja na kuunga mkono uwepo wa  siku ya Kimataifa kwaajili ya walemavu wa ngozi. Ilibani   mapungufu kadhaa  yakiwamo ya  kiufundi  katika eneo zima la uwasilishwaji wa   Azimio lenyewe na kubwa zaidi,  Azimio  halikuwa linatambua juhudi mbalimbali zinazofanywa na  serikali kulishughulikia tatizo hilo.
Kutokana na  mapungufu  hayo na namna azimio lilivyowasilishwa,  Tanzania  ilipendekeza  kwa wajumbe wa  Kamati  nyongeza   ya  vipengele   kikiwamo  kinachotambua   mchango na juhudi za serikali
Aidha  pamoja na pendekezo hilo, Tanzania pia ilishauri kuwa ili  Azimio hilo liwe na tija zaidi kwa walengwa,  lakini pia kama  sehemu ya  uelimishaji  jamii  juu ya    matatizo yanayowakibili watu wenye  ulemavu wa  ngozi,  ikataka  pawe pia na  kipengele  kinachoiagiza Jumuiya ya Kimataifa kuziwezesha na  kuzisadia  nchi ambazo zinakabiliwa na tatizo hilo.
“ Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  hatuna tatizo na  dhana  nzima ya  ujumbe na umuhimu wa Azimio hili. Nchi yetu ni kati ya nchi zenye  idadi kubwa ya watu  ambao  wana ulemavu   wa ngozi.  Ni   kundi hili la jamii  linakumbana na matatizo   mengi yakiwamo kufanyiwa vitendo vya  kikatili  na kunyanyapaliwa n ahata kupoteza maisha. Amesema  mwakilishi wa Tanzania
Na kuongeza kwamba,  pamoja na ukubwa wa tatizo na changamoto zake, Serikali ya Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania inajitahidi kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na  udhalimu na ukatiliwanaofanyiwa watu wenye  ulemavu wa ngozi.


 Tanzania  imesisitiza kwamba  haitoshi kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na siku ya Kimataifa ya watu wenye ulemavu wa ngozi  bila ya kuwa na mipango na mikakati madhubuti na yenye tija ambayo kwayo italenga zaidi kuwasaidia walengwa  na serikali.
Baada ya  majadiliano  na ushawishi mkubwa Tanzania imefanikiwa kuingiza katika Azimio hilo kipengele ambacho Jumuiya ya Kimataifa inatambua juhudi na mchango wa serikali katika eneo hilo.  
Azimio  limepitishwa  kwa kupigiwa kura  160 za  ndiyo,  na  16 hazikufungamana na upande wowote

No comments: