ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 20, 2014

UNAJENGA UKARIBU NA MKE, MPENZI WA MTU ILI IWEJE?


Ni wiki nyingine tulivu kabisa tunakutana kupitia safu hii nikiamini umzima bukheri wa afya. Mimi namshukuru Mungu kwa kunipa nguvu na uwezo wa kuandika hiki nilichodhamiria kukufikishia siku ya leo.
Nazungumzia ukaribu ambao baadhi ya watu wamekuwa wakiujenga kwa wake au waume za watu bila hofu yoyote na kuona ni jambo la kawaida tu.

Katabia hako kamechipukia huko mtaani ambapo unakuta mtu yuko kwenye ndoa au uhusiano wa kawaida lakini eti anafagilia kuwa na ukaribu uliopitiliza na watu wa jinsia nyingine, tena wanaoonesha wazi kuwatamani kingono.

Yaani mke wa mtu anaona si jambo baya kuchati na mwanaume mwingine au kuonana na kupiga naye stori bila mume wake kujua chochote. Mume wa mtu kujenga mazoea na mwanamke mwingine kiasi cha kufikia hatua ya kuona siyo mbaya kupeana fedha na kushirikishana kwenye mambo kadha wa kadha kwa siri eti ni sawa.

Najua kwenye hili wapo watu ambao hawajali, wenyewe wanajiita ‘disminders’. Kwa msaada tu kwa wale ambao kimombo kimewapiga chenga ‘disminder’ ni mtu ambaye hata akimuona mpenzi wake ana ukaribu uliopitiliza na mtu mwingine hajali, anachukulia poa.

Mke anamuona kabisa mumewe kakaa baa na wanawake kibao huku akiwapa ofa lakini anachukulia poa, hataki kujipa ‘hedeki’. Ananyamaza eti kuepusha shari. Mimi nadhani kama kweli unajali uhusiano wako, huwezi kuwa ‘disminder’ kwa vitu ambavyo vinaweza kuja kukuharibia. Mtu makini hawezi kuona mpenzi wake anachekacheka na mtu wa jinsia nyingine, wanapigiana simu mara kwa mara, wanachati usiku na mchana halafu yeye anaona ni poa tu.

Ukiwa mtu wa sampuli hiyo utakuwa na matatizo ya akili.
Lakini wakati hilo likiwa hivyo, wapo baadhi ya wanawake wanajua kabisa f’lani ni mume au mpenzi wa f’lani lakini bila soni wanatengeneza ukaribu uliopitiliza bila kufikiria madhara yanayoweza kutokea.
Mwanaume naye utashangaa anamganda mke wa mtu, akiuliza eti ni urafiki wa kawaida tu, urafiki wa kawaida kwa mke wa mtu? Hivi mwenye mali zake akigundua unadhani atalielewa jibu la kwamba ni marafiki tu?

Hujaona watu wengine ambao unaweza kutengeneza nao urafiki wa kutaniana, kuchati, kupigiana simu mpaka ukamgande mke wa mtu?

Najua haikatazwi kuongea na mke wa mtu, swali ni je mnaongea nini? Siyo tatizo kumpigia simu au kumtumia sms mke wa mtu lakini pia watu watataka kujua sms kwa mke wa mtu inahusu nini au umeamua kumpigia simu mke wa mtu usiku kwa lipi?

Utakuwa ni mtu wa ajabu kama utamtumia sms mke wa mtu na kumuuliza; mambo vipi? Kufanya hivyo utakuwa unatafuta matatizo kwani mume wake akiiona hiyo sms hawezi kukuelewa. Hatakuelewa kama ulikuwa unamsalimia tu, atakuweka kwenye kundi la watu wanaotaka kuiharibu ndoa yake.
Cha msingi hapa ni watu kujiheshimu na kuziheshimu ndoa na mahusiano ya wenzao. Ukiona mtu ana mpenzi wake, utani wa kujinga, mazoea yasiyo na maana yasipewe nafasi.

Hata kama mwanamke atakuwa mcharuko na kutaka kukutengenezea mazingira ya wewe kumzoea, muogope kama ukoma na mwambie amheshimu mpenzi wake.
Ukichukulia kwa kuwa kaanza kukupigia simu wewe usiku na wewe ukawa unafanya hivyo, ipo siku yatakukuta ya kukukuta.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine. GPL

3 comments:

Anonymous said...

Natamani mume wangu asome maana kutwa kuongea na wake za watu halafu akirudi nyumbani anajifanya malaika. Nimechoka

Anonymous said...

Ambae ajakuelewa apo tumchape na viboko kabsa....

Anonymous said...

😂😂Anaitaj viboko uyoo