Advertisements

Thursday, December 25, 2014

Daktari mmoja Tanzania huhudumia watu 30,000

Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa.

Daktari mmoja nchini Tanzania, anahudumia watu 30,000 (1:30,000), utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO), umeonyesha.

Hata hivyo, takwimu hizo zipo mbali mno na uwiano uliopendekezwa na WHO wa daktari maalum mmoja kuhudumia watu 1,000.

Taarifa ya Hospitali ya Apollo jana ilisema kutokana na ukuaji wa haraka wa idadi ya watu nchini, kwa ujumla uwiano huo haujabadilika katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Kutokana na uhaba huo unaojionyesha, ufumbuzi ni kuongeza idadi ya madaktari katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Hata hivyo, taarifa ilisema jambo hilo linaonekana kama litakuwa mkakati wa muda mrefu nchini na hivyo ufumbuzi wa haraka ni wa kutumia teknolojia kama vile telemedicine katika maeneo hayo.

Ilifafanua kuwa hatua ya kutumia teknolojia ya telemedicine, itaruhusu maeneo ya mbali zaidi kama vile vijijini kuwa na upatikanaji wa mtaalam katika hospitali atakayetoa ushauri na matibabu kwenye hospitali na kliniki hizo bila kusafiri umbali mrefu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, teknolojia ya telemedicine, bado ni changa nchini Tanzania.

Moja ya nchi zilizofanikiwa kwa kutumia teknolojia hiyo ni India ambayo hutumia kutoa matibabu nchini humo pamoja na nchi nyingine duniani, ilisema.

Kwa jinsi teknolojia inavyoendelea kutafsiri upya utoaji wa huduma za afya, Tanzania inatakiwa kuanza matumizi ya telemedicine kwa kiwango kikubwa, taarifa ilifafanua.

Kwa kutumia teknolojia hii, ilisema upatikanaji na utoaji wa huduma maalum za matibabu utakuwa rahisi kwa wananchi wote.

"Madaktari bingwa waliopo katika hospitali muhimu na kubwa kama Muhimbili au KCMC, wana uwezo wa kubofya kitufe mara moja na kuhudumia wagonjwa au kutoa msaada wa kitaalam kwa madaktari wenzao waliopo katika maeneo ya mbali zaidi hususan vijijini," taarifa ilisema.

Wakati wa mkutano wa siku mbili wa telemedicine uliofanyika Septemba, mwaka huu mjini Bagamoyo ambao uliandaliwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Universal Communications Service Access Fund (UCSAF).


Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, alionyesha matatizo mbalimbali yanayoikabili sekta ya afya nchini na pia alielezea umuhimu wa teknolojia hiyo ili kukabiliana na changamoto zilizopo.

Profesa Mbarawa alisema kuwa kwa sasa Tanzania ina watu binafsi na wataalam ambao wanapaswa kuwa sehemu ya mapinduzi katika sekta ya afya.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, wakati wa mkutano huo, alitoa wito wa kujifunza kutoka kwa hospitali na taasisi zenye uzoefu zaidi.

Kiungo muhimu katika teknolojia ya telemedicine, Profesa K. Ganapathy, amenukuliwa akisema kwamba kupitia teknolojia hiyo, kuna uwezo wa kufanya jiografia kuwa historia kwa kufanya umbali kutokuwa na maana na hivyo kurahisisha gharama za upatikanaji wa huduma bora za afya kwa kila mtu wakati wowote na mahali popote.
CHANZO: NIPASHE

No comments: