Advertisements

Friday, December 19, 2014

MWAKA 2014 UNAISHIA NA HUJAFANYA CHA MAANA, WHY? KWA NINI?

Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa upendo aliouonesha kwangu na kuniwezesha kuiona siku ya leo nikiwa mzima. Nadiriki kushukuru kwa sababu, wapo waliotamani kuiona wiki hii wakiwa wazima lakini baadhi wameshaondoka kwenye ardhi hii huku wengine wakiwa hoi mahospitalini na majumbani.

Ndugu zangu, mwaka ndiyo huo unakaribia kuisha. Najua wapo wanaoumaliza wakiwa wamefanya mambo makubwa lakini pia wapo ambao mioyo yao imesinyaa kwa kuwa, waliyopanga kuyafanikisha hayakutimia.

Mimi nataka kuwatia moyo wale ambao mwaka unaisha bila kufikia mafanikio waliyotarajia. Kumbuka kila jambo linapangwa na Mungu, yawezekana yeye kwa sababu anazojua kapanga ufanikiwe mwaka ujao na siyo huu.

Kikubwa ni kuamini kuwa hakuna linaloshindikana kwako. Wewe ni bilionea mtarajiwa! Wewe ni mmiliki wa makampuni makubwa mtarajiwa nk. Hizo ziwe ni kati ya ndoto zako kubwa kwenye maisha yako ya kesho na huna sababu ya kufa moyo.

Ukifuatilia historia za watu wenye mafanikio makubwa duniani utagundua miaka na miaka ilikatika wao wakiishi maisha magumu lakini hawakunyanyua mikono juu na kusema wameshindwa!Kadiri walivyokuwa wakikumbana na changamoto ndivyo walivyozidi kupambana wakiamini walikuwa wakiyakaribia mafanikio.

Kwa jitihada walizoonyesha kuna wakati Mungu akaamua kuwabandika mikono ya baraka na wakafanikiwa. Wewe pia amini mwaka ujao ni wako wa mafanikio, ongeza bidii.
Hata hivyo, yapo mambo ya msingi ya kuyazingatia ili mwaka ujao ujiweke kwenye nafasi nzuri ya kuingia kwenye historia ya watu waliofanikiwa.

Ni vyema ukajipanga upya
Waswahili wanasema, kuteleza si kuanguka, kama ulishindwa kufanikiwa mwaka huu, kaa chini tena na uorodheshe malengo yako. Unashauriwa kutafakari upya na kutafuta njia sahihi za kuweza kufanikisha malengo hayo.

Thubutu tena na tena
Maisha siku zote ni mapambano. Maisha ni kutoogopa kujaribu kwa kuhofia kushindwa. Kamwe usiogope kuthubutu tena na tena kwani hata ukishindwa itakuwa ni hatua ya kuelekea kwenye mafanikio.

Dadisi, ongea na waliofanikiwa
Kuwa tayari kujifunza kutoka kwa wengine ambao wamemaliza mwaka huu wakiwa wamefanikiwa katika mambo yao. Jaribu kudadisi na kung’amua ni kwa namna gani wameweza kufikia malengo yao ili na wewe ujifunze kitu kutoka kwao.

Kukata tamaa ni mwiko
Katika kujaribu kufikia malengo yako ni wazi umekutana na vikwazo vya hapa na pale na wakati mwingine kuhisi huwezi kuendelea tena.
Siku zote vikwazo unavyokutana navyo viwe ni changamoto kwako ya kujipanga upya na kuanzisha tena mapambano ya kufikia malengo yako.

Kukata tamaa ni mwiko kwani inaelezwa kuwa, idadi kubwa ya watu wanaoishi maisha yasiyokuwa na nyuma wala mbele wameathiriwa na tabia ya kukata tamaa.

Omba ushauri
Katika mbio za kufikia malengo yako, usiishi kama kisiwa, wakati mwingine omba ushauri wa kimawazo pale utakapokwama. Usikubali kubaki na msongo wa mawazo, jaribu kutafuta msaada na ushauri kwa watu unaowaamini.

Anasa ni sumu
Matumizi mabaya ya fedha na kupoteza muda mwingi katika mambo ya anasa kamwe haviwezi kukusaidia kutimiza ndoto zako. Daima kazi kwanza, starehe baadaye, ishi kama mtumwa leo, ili utimize ndoto ya kuishi kama mfalme kesho!

Jifanyie tathimini
Katika hatua nyingine ni vyema pia ukachukua muda wako kujitathimini kwa kudadisi sababu ambazo huenda zimekufanya usifanikiwe mwaka huu. Je, matumizi yako ya fedha yalikuwa mabaya kiasi cha kutokuwa makini na kila shilingi uliyokuwa ukiipata? Je, hukujituma sana na hukutumia akili na maarifa yako katika kiwango cha juu?

Je, ulitengeneza mazingira ya kuwapa mwanya maadui wakukatishe tamaa na kukufanya uhisi huwezi? Fanyia kazi maswali hayo!

GPL

2 comments:

Anonymous said...

Shukran kwa hii article.

Anonymous said...

ahsante kwa makala haya na nauliza kama sina rafiki mimi nifanyeje kwenda kumuliza mtu ushauri au maswali wote nawaona wakutoka katika nchi yangu wako na choyo cha roho.kila kukicha mimi nawasidia wao,wao hata siwaoni linaponipata janga mimi.so nifanyeje.si bora nibaki na msogo wa mawazo mwenyewe na kumuomba mungu wangu anisaidiye.ameen