By EDO KUMWEMBE (email the author)
Lilikuwa bao muhimu. Dakika chache baada ya Didier Kavumbagu kuipatia Azam bao la kuongoza. Kwa wanaomfahamu Tambwe hawakushangazwa na bao lile.
KWA shabiki wa Simba kuna picha inayoudhi, kukera na kunyanyasa moyo kama ile ya juzi wakati Amiss Tambwe alipokuwa akishangilia bao lake la kwanza katika jezi ya Yanga, tena katika pambano dhidi ya Azam!
Lilikuwa bao muhimu. Dakika chache baada ya Didier Kavumbagu kuipatia Azam bao la kuongoza. Kwa wanaomfahamu Tambwe hawakushangazwa na bao lile.
Krosi ya Salum Telela ilikuwa inaelekea katika vidole kumi vya Mwadini Ally lakini Tambwe akaipitia kama umeme.
Hii ilikuwa sura ya kwanza ya maudhi katika pambano la Yanga na Azam juzi.
Bahati mbaya maudhi hayo yaliwasuta mabosi wa Simba waliokuwa wamekaa jukwaa kubwa pamoja na mashabiki wao pamoja na Kocha, Patrick Phiri kama alikuwepo uwanjani.
Unamuachaje mshambuliaji kama Tambwe kwa visingizio hafifu? Inadaiwa kuwa Phiri alikuwa hamtaki kwa sababu Tambwe hakuwa hodari katika kucheza kitimu nje ya boksi la adui.
Hata hivyo, kocha mwenye mipango angeweza kumtumia sana Tambwe katika mechi dhidi ya timu dhaifu ambazo kwa kweli ni nyingi sana Ligi Kuu yetu.
Kwa Simba kuna mechi mbili tatu tu ambazo inaweza kujihami zaidi. Nyingine nyingi inashambulia. Sasa kwa nini uachane na Tambwe?
Picha ya pili ya maudhi katika pambano la juzi ni usumbufu wa Didier Kavumbagu kwa Kevin Yondani na Mbuyu Twitte. Watu hawa wawili watakuwa wanaulizana ni kwa nini mabosi wao waliruhusu kumuacha Kavumbagu aondoke Yanga.
Yondani na Twitte ndiyo walioijua adha ya kucheza timu tofauti na Kavumbagu.
Mipira mingi ya hewani ilikuwa yake. Matumizi yake ya nguvu yaliwachosha. Lakini hapa unamzungumzia mchezaji ambaye Yanga walimuacha bure Julai mwaka huu kwa visingizio hafifu.
Alikuwa mshambuliaji mwenye tabia tofauti kwa Yanga. Kumuacha na kumnunua Geilson Santos ‘Jaja’ kulipunguza kwa kiasi kikubwa usumbufu wa Yanga katika safu ya ushambuliaji.Siyo Yondani tu, waulize mabeki wengi wa kati wa Ligi Kuu ya Tanzania watakwambia jinsi Kavumbagu alivyo msumbufu katika matumizi ya mwili.
Maudhi mengine yalikwenda kwa Wanayanga tena.
Hawakuhitaji kujilaumu sana kwa sababu hayakuwa maamuzi yao, lakini kiwango cha Salum Telela katika eneo la katikati ya uwanjani kiliwasuta kwa jinsi walivyopoteza pesa nyingi kwa wachezaji wa kigeni eneo hilo.
Telela huenda ndiye alikuwa mchezaji bora wa mechi.
Alimiliki mpira vizuri, aliisambaza vyema, alikuwa na hamu na mpira popote ulipokwenda, alikimbia vizuri na atakumbukwa kwa krosi yake ya bao la Tambwe.
Kwa nini ukimbilie kuwanunua wachezaji wa kigeni kwa pesa nyingi wakati una Telela?
Kama ni majeruhi, kwa nini usitumie pesa nyingi kumtibu ili kumrudisha uwanjani mapema kwa ajili ya kuisaidia timu?
Picha nyingine inayoshangaza sana ni ile ya Salum Abuubakar ‘Sure Boy’ wa Azam.
Mechi ya juzi haikumuendea vizuri sana. Lakini kwa nini mashabiki wa Simba na Azam wameanza kumkariri Sure Boy katika mechi dhidi ya Yanga?
Mashabiki wa Simba na Azam walimtoa mchezoni mapema Sure Boy. Hawakumwamini. mwishowe yeye mwenyewe hakujiamini.
Sababu ni moja tu kwamba baba yake Abuubakary Salum alikuwa mchezaji hodari wa Yanga.
Wanaamini kuwa watu wa Yanga wanamtumia Sure Boy kupitia kwa baba yake ili aihujumu Azam katika mechi dhidi ya Yanga.
Ni madai magumu kuyathibitisha lakini kwa kiasi kikubwa Sure Boy anaondoka mchezoni katika dakika tano tu za mwanzo za pambano lolote dhidi ya Yanga.
Hofu kubwa hapa ni kwamba huenda baada ya muda mfupi mashabiki wa Simba wakahamia kwa kipa wao, Manyika Peter. Baba yake, Peter Manyika alikuwa kipa mahiri wa Yanga. Kuna uwezekano baadaye ikadaiwa kuwa Manyika anamtumia mwanaye kuihujumu Simba.
Lakini pia suala hili litakuwa linawaweka katika wakati mgumu wachezaji chipukizi ambao baba zao walikuwa wanacheza Simba au Yanga, halafu wao wakaja kuibukia timu pinzani na zile ambazo baba zao walikuwa wanachezea.
Labda huu ni wakati mwafaka wa kuanza kuwaamini wachezaji walioangukia upande tofauti na ule ambao wazazi wao walicheza. Kama tutaendelea tuliloliona kwa Sure Boy, basi mwishowe tutazalisha wachezaji ambao lazima wachezee timu ambazo baba zao walichezea.
"CREDIT:MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment