Advertisements

Friday, December 19, 2014

Sarakasi mpya ya Escrow

Dar es Salaam. Wakati Taifa likisubiri kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge ya kuwawajibisha mawaziri na watendaji wa Serikali waliohusishwa na kashfa ya Akaunti ya Escrow, Kampuni za IPTL na Pan Africa Power Solutions (PAP) zimekimbilia mahakamani kuzuia utekelezaji wa maazimio hayo.
Kampuni hizo kwa kushirikiana na Harbinder Singh Seth zimefungua kesi ya kikatiba Katika Mahakama Kuu ya Tanzania dhidi ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupinga utekelezaji wa maazimio hayo.
Kesi hiyo imefunguliwa siku mbili baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kujiuzulu wadhifa huo akisema ushauri wake wa kisheria kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow haukueleweka na hivyo kuchafua hali ya hewa.
Pia ni katika kipindi ambacho kuna taarifa zilizothibitishwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue kuwa Rais Kikwete atazungumzia suala hilo wakati wowote kabla ya kesho.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo zimesambaa katika mitandao ya kijamii Rais Kikwete atazungumza kupitia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam leo, lakini Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salva Rweyemamu alipoulizwa jana hakukanusha wala kukubali akisema ikitokea Rais anataka kuzungumza vyombo vya habari vitataarifiwa.
Tayari Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyekuwa ziarani Uarabuni amerejea nchini jana mchana baada ya ziara yake kukatishwa na Rais Kikwete kwa shughuli maalumu na anatarajiwa kurudi tena Falme za Kiarabu kesho kuendelea na ziara yake hadi Desemba 23, mwaka huu.
Kesi yenyewe
Katika kesi hiyo namba 59 ya mwaka 2014, iliyofunguliwa chini ya hati ya dharura jana, kampuni hizo zinawakilishwa na mawakili kutoka kampuni za uwakili za Bulwark Associates Advocates, Asyla Attorneys na Marando, Mnyele & Co. Advocates za Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo, kampuni hizo zinadai kuwa kile kilichofanyika ndani ya Bunge, kujadili na kupitisha maazimio dhidi ya watuhumiwa hao, ni kinyume cha Katiba na kwamba kina lengo la kugombanisha mihimili mitatu ya dola.
Kampuni hiyo zinadai kuwa kulikuwa na kesi ambazo zinaendelea mahakamani zinazohusu suala ambalo Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Takukuru walifanyia uchunguzi na hatimaye taarifa ya CAG kujadiliwa bungeni na kutolewa maazimio hayo.
Maazimio ya Bunge ni pamoja na kutaka waliohusika wawajibike kwa mujibu wa sheria, Serikali iangalie uwezekano wa kutaifisha na kuifanya mitambo ya IPTL imilikiwe na Serikali, ipitie upya mikataba yote na kuangalia kama ina masilahi na Taifa na iboreshwe.
IPTL na PAP zimesema kitendo hicho cha kujadili na kutoa maazimio kilipuuza amri ya Mahakama Kuu kwa kufuata tafsiri potofu iliyotolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha - Rose Migiro kuhusu amri ya Mahakama hiyo, ambayo ilizua mjadala wa escrow kujadiliwa bungeni.
Maombi
Mawakili hao wamewasilisha maombi likiwamo la Mahakama Kuu kutangaza kwamba maazimio hayo ya Bunge ya Novemba 29/2014 na uamuzi wa Spika wa kuyakubali maazimio hayo ni kinyume na Katiba kwa kuwa yanakiuka Ibara ya 13(1), 13(3), 13 (6)(a) (b)(e) na 24 na 26.
Ibara hizo zinataka haki za kila mtu au jumuiya, kulindwa na kuamriwa na Mahakama ya kisheria au chombo chochote ambacho kimeanzishwa kisheria, hivyo maazimio hayo ni batili.
Wanadai kuwa maazimio yaliyotolewa na Bunge yaliegemea upande mmoja kwa vile baadhi ya wahusika walioshiriki kuyapitisha wana kesi zinazohusiana na suala hilo na walishindwa kutangaza masilahi yao.
Pia wamewasilisha maombi ya amri ya zuio la muda la utekelezaji wa maazimio hayo, wakidai kufanya hivyo kutaathiri kesi ya msingi na nyingine zinazoendelea ambazo wadaiwa ni sehemu ya kesi hizo na kufanya hivyo ni kuifanya Mahakama kuegemea upande wa wadaiwa.
Katika maombi hayo ya zuio, kampuni hizo zinadai kuwa wadaiwa wanatarajia kutekeleza maazimio yaliyopitishwa na Bunge ambayo yapo kinyume na iwapo maombi hayo ya zuio hayatasikilizwa kama suala la dharura, itaathiri haki katika kesi zinazowahusisha wadai na kuonekana siyo wa muhimu.
Mwananchi

3 comments:

Anonymous said...

Pathetic,.Jambo hili limegeuzwa kuwa mipasho as if watu wako kwenye taratibu za kumtoa mwali..Where is the executive power in our country?

Anonymous said...

There is non excutive power in our country wote wamekalia kiusani sani tu na kifisadi fisadi tu na ndo maana na sisi huku tuko hivi kushabikia ujinga ujinga tu kisa tumepenyezewa vijisenti mbuzi.

tuko majuu but akili zetu ziko za mgando kama snow ya mount Kilimanjaro.

mipasho mipasho udaku udaku na kumtoa mwari kama ulivyosema ndo mpango mzima wa serikali hii na mijitu yenye kupewa vijisenti mbuzi.

luka wangu usibane comment big boy.

Anonymous said...

watz wenzangu siku ambayo tutakapo acha kuwa mashabiki wa wanasiasa na mambo ya kipuzi puzi mengine tunayoyafanya ndo siku ya hatua ya kwanza ya kujikomboa itakapo anza.

NY.