Advertisements

Friday, December 19, 2014

BVR ‘zachemsha’ uandikishaji Dar

Dar es Salaam. Uandikishaji wa wapigakura kwa kutumia mfumo mpya wa BVR unaoendelea katika kata tatu za Jiji la Dar es Salaam umeanza kusuasua kutokana na matatizo ya watendaji na mashine zinazotumika kwenye uandikishaji huo.
Uandikishaji huo unaofanyika kwa majaribio kwenye Kata za Bunju, Mabwepande na Mbweni ulianza Jumatatu wiki hii na unatarajiwa kumalizika Jumatatu wiki ijayo.
Akizungumzia uandikishaji huo jana, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bunju yenye vituo 13, Emmanuel Riwa alisema wamekuwa wakikabiliwa na matatizo makubwa yanayotokana na ufanisi mdogo wa mashine za kutoa vitambulisho, hivyo kuchukua muda mrefu tofauti na ilivyotarajiwa.
Alisema matatizo makubwa yanayojitokeza kwenye maeneo mengi ni mashine hizo kuzimika na kushindwa kuendelea kuzitumia kama ilivyopangwa huku idadi ya watu wanaojitokeza ikizidi kuongezeka.
“Mashine tatu unazoziona hapo nje zimezimika na imewalazimu watendaji wetu kuzirudisha na nyingine zinazoendelea kutumika kasi yake ya kutoa vitambulisho ni ndogo sana. Kwa hiyo watu wanaendelea kujaa vituoni huku wakisubiri huduma bila mafanikio,” alisema Riwa.
Alieleza kwamba japokuwa wamekuwa wakiandikisha hadi watu 800 kwa siku, itakuwa si rahisi kufikia lengo ndani ya siku saba zilizopangwa hivyo kushauri kuongeza siku zaidi kwa ajili ya kutoa nafasi pana zaidi kwa watu wengi kujiandikisha.
Riwa alisisitiza kamba japokuwa watu wanajitokeza kwa wingi sasa, hali inatarajiwa kuwa ngumu zaidi katika siku za mwisho wa wiki ambazo wengi waliopo katika kazi zisizowaruhusu kurudi nyumbani mapema watakuwa mapumziko na kutumia nafasi hiyo kujiandikisha.
“Kwa kweli, wakati tunaendelea kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayojitokeza kutokana na mashine hizi, bado tunaona changamoto zaidi katika siku hizi za mwisho wa wiki. Ndiyo maana tunaomba ikiwezekana siku ziongezwe,” alisema.
Baadhi ya wananchi waliotokeza kujiandikisha walieleza kwamba wapo waliojitokeza juzi wakashindwa kujiandikisha hadi jioni kutokana na wingi wa watu na hata walipofika jana walikuwa wakiendelea kupoteza muda mwingi kusubiri kuandikishwa.
Mmoja wa wananchi hao, Peter Stephano alisema katika kituo alichokuwa akisubiri kujiandikisha, watendaji walichelewa na kufungua kituo saa nne badala ya saa mbili asubuhi wakati wananchi wakiwa tayari wameshajipanga kwenye foleni tangu saa 12 asubuhi.
“Wengi tunajitokeza lakini tunapofika vituoni matatizo yanayojitokeza yanasababisha tupoteze muda mwingi. Wengine wanaamua kurudi nyumbani na kuendelea na shughuli zao kwa sababu hawawezi kupoteza siku nzima hadi siku mbili kwa ajili ya kujiandikisha tu,” alisema.
Katika kituo cha Shule ya Sekondari Mbweni, wananchi walikuwa wamefurika kujiandikisha huku wakilalamikia ubovu wa mashine moja kati ya mbili, hivyo kutumia mashine moja na kuchelewesha uandikishaji.
Mwandishi wetu alishuhudia watu wawili wakiandikishwa kwa nusu saa katika kituo hicho, kutokana na mashine moja iliyobaki kuwa na kasi ndogo ya kukusanya maelezo na kutoa kitambulisho.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mbweni yenye vituo 15, Sylvester Nchonja alisema wanaendelea kukabiliana matatizo madogomadogo yanayojitokeza na uandikishaji unaendelea kama ulivyopangwa.
Alipoulizwa kuhusu matatizo hayo, Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Julius Malaba alisema bado wanasubiri taarifa kutoka kwa msimamizi ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, ambaye hata hivyo, hakupatikana baada ya simu yake kuita bila kupokewa.
Mwananchi

No comments: