Balozi Irene Kasyanju, Mkurugenzi wa Idara ya Masuala ya Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akizungumza wakati wa Mkutano wa Kumi na Tatu wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC). Mkutano huo wa wiki mbili unafanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Sehemu ya wajumbe wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai wakimsikiliza Mwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano huo, Balozi Irene Kasyanju ambaye katika hotuba yake pamoja na mambo mengine ameishauri Mahakama hiyo kuimarisha uhusiano wake na Afrika.
.
Na Mwandishi Maalum, New York
Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, imesema, mafanikio ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya
Jinai (ICC) yatategemea uimarishishwaji
wa ushirikiano kati ya Makahama hiyo na
Afrika.
Na kwa sababu hiyo, Tanzania imeshauri
kuwa Rais Mpya wa Mkutano wa Nchi wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa
ya Jinai hana budi kuhakikisha kuwa moja ya vipaumbele vyake vijielekeze katika
kuimarisha uhusiano wa Makahama hiyo na Afrika.
Ushauri huo umetolewa na Balozi
Irene Kasyanju, Mkurugenzi wa Idara ya
Masuala ya Sheria, Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati akizungumza katika mkutano wa kumi na tatu wa Nchi
wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai.
Amesema Tanzania ina imani kubwa
na Rais mpya wa Mkutano wa Nchi wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya
Jinai, Bw. Sidiki Kaba, kutoka Senegal, kuwa afanye kila awezalo katika
kuimarisha uhusiano huo ambao kwa sasa
umezorota.
Vile vile Balozi Kasyanju amesema
Rais huyo anashika uongozi katika kipindi ambacho, Mahakama inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na mwenendo mzima wa mahakama
na hasa uhusiano wake na Afrika.
Amebainisha kuwa, changamoto hiyo
ya mahusiano na nyinginezo zinahitaji majadiliano ya uwazi yatakayowashirikisha
wadau wote, na kwamba Tanzania inaamini kuwa
anao uwezo huo.
Akizungumzia zaidi kuhusu ushirikiano kati ya Mahakama na Afrika,
Tanzania imeeleza kuwa namna ICC ilivyoshughulia shauri la Kenya hakutafanya mambo yawe shwari, kutokana na
ukweli kuwa ICC ilishindwa kulifanyia kazi ombi la awali lililowasilishwa na
Afrika mbele ya chombo hicho la kutaka kuahirishwa kwa shauri hilo kumechangia katika kuongeza malumbano
kati ya ICC na Afrika.
Kwa mantiki hiyo Tanzania imesema
uamuzi wa hivi karibuni wa kumwondolea mashtaka Rais Uhuru Kenyata unapaswa kutoa fursa kwa mahakama hiyo kujitazama upya.
Vile vile Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imetumia fursa hiyo kumpongeza Rais Kenyatta kwa kuonyesha ushirikiano na ICC.
Katika hatua nyingine Tanzania
pia imeishauri ICC kuangalia namna
itakavyoweza kufanya kazi kwa
karibu na Baraza Kuu la Usalama la Umoja
wa Mataifa hasa katika kushughulikia makosa ya jinai yanayofanywa na Nchi ambazo si wanachama wa Mkataba wa Mahakama hiyo ili kuondoa dhana ya
undumilakuwili katika utendaji wa ICC.
Tanzania imeujulisha mkutano huu
kwamba ipo katika hatua yake ya awali ya
kuziingiza sheria zitokanazo na Mkataba wa ICC katika mfumo wa Kisheria wa
Nchi.
Balozi Kasyanju anaongoza Ujumbe
wa Tanzania katika Mkutano huo wa wiki mbili unaohusisha pia uchaguzi wa
majaji sita wa mahakama hiyo.

.jpg)
No comments:
Post a Comment