.Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akilizungumza Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hapo siku ya Alhamis kabla Baraza hilo halijapigia kura Azimio linalotaka kuwapo kwa siku ya Kimataifa ya kuwatambua watu wenye ulemavu wa ngozi. Kulia kwa Balozi ni Bi. Ellen Maduhu Afisa wa Uwakilishi anayeshughulika Kamati ya Tatu inayohusika na masuala ya Haki za Binadamu, Utamaduni na Masuala ya Jamii na alishiriki kikamilifu katika majadiliano ya kwanza kuhusu Azimio hilo ambapo alihakikisha Azimio limetambua juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi pamoja na kuzikabili changamoto wanazokumbana nazo.
Sehemu ya Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakiwa katika mkutano ambao ulipitisha maazimio mbalimbali yaliyowasilishwa mbele ya Baraza hiyo na Kamati ya Tatu. Baadhi ya Maazimio yaliyopitishwa katika mkutano huo uliofanyika siku ya Alhamis lilikuwapo linalopendekeza kuwapo wa siku ya Kimataifa ya watu wenye ulemavu wa ngozi ( Albino).
Na Mwandishi Maalum, New York
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza kwamba haitoshi kuwa na siku ya
kimataifa ya kuwatambua watu wenye ulemavu wa ngozi ( Albino) pasipo
kuwa na mikakati madhubuti inayolenga
katika kuwawezesha.
Hayo yameelezwa
na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi alipokuwa akizungumza muda mfupi
kabla ya Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa halijapigia kura Azimio linalotaka kuwepo kwa Siku ya
Kimataifa ya Kuwatambua watu wenye
Ulemavu wa ngozi.
Leo ( Alhamsi) Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipokea mapendekezo ya maazimio mbali mbali yaliyowasilishwa
mbele ya Baraza hilo yakitokea
Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Kamati inayohusika na
masuala ya Haki za Binadamu, Utamaduni
na Maendeleo ya Jamii.
Miongoni mwa Maazimio hayo lipo lililohusiana na Haki za
Binadamu ambapo ndani ya maazimio ya eneo hilo kuna azimio linalopendekea kuwa
wa siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Balozi Manongi
amelieleza Baraza hilo kuwa, kimsingi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
haipingi kuwapo kwa siku ya kimataita ya
kuwatambua watu wenye ulemavu wa ngozi .
Lakini inapata shida pale azimio
hilo linaposhindwa kuainisha mchango na mikakati ya kimataifa ya kuwezesha
jamii hiyo kukabiliana na
changamoto mbalimbali.
Akiongea kwa
msisitizo, Balozi Tuvako Manongi ameeleza
kuwa Tanzania ni nchi ambayo inaidadi kubwa ya watu wenye
ulemavu wa ngozia na pamoja na
changamoto na matatizo wanayokumbana nayo.
Amezitaja baadi ya changamoto
hizo na ambazo pia zimeainishwa katika Tume ya Haki za Binadamu kuwa ni pamoja na kutopata huduma
kamilifu za kiafya, elimu, kunyanyapaliwa na madhira mengine.
“Kuna changamoto
mbalimbali zinazowakabili, Changamoto ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi
na kutafutiwa ufumbuzi. Kama nchi yenye
idadi kubwa ya watu wenye ulemavu wa
ngozi, Ujumbe wangu ulijjitahidi katika
kuhakikisha kuwa pendekezo la Azimio
hili ambalo leo limeletwa mbele ya Baraza hili linakuwa lenye tija na manufaa
zaidi kwa walengwa kuliko lilivyo hivi sasa” amesema Balozi Manongi
Amesema kuwa pamoja na
kwamba pendekezo hilo la kuwa na siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu
wa ngozi ni hatua muafaka, lakini halitoi mwelekeo wa namna ya kushughulikia matatizo yao
pamoja na uwezeshwaji wao.
Ni kwa sababu
hiyo na kutokana na mapungufu
hayo ambayo yalikuwa hayatoi nafasi wa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na
Juhudi za Tanzania katika kuzikabili
changamoto zinazowakabili watu wenye ulamemavu wa ngozi.Ndiyo maana Tanzania
kwa nia njema kabisa iliomba azimio
hilo lipigiwe kura si kwa maana ya kulipinga azimio lakini
kupinga azimio hilo kutokuwa na maslahi mapana kwa watu wenye ulemavu wa ngozi.
Mwakilishi huyo wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,
amekwenda mbali zaidi kwa kusema
kuwa Tanzania na kama ilivyokuwa kwa wanachama wengine, imekuwa ikiaamini kuwa Chombo hicho kwa maana
ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Mataifa kwa ujumla wake
vinapashwa kupitisha maamuzi na maazimio yenye tija zaidi.
Azimio hilo limepitishwa kwa kupigiwa kura ambapo licha ya mapungufu yake, inatambua kuwa June 16 ya kila mwaka itakuwa ni
siku ya Kimataifa ya kuwatambua watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino)
No comments:
Post a Comment