Advertisements

Friday, December 19, 2014

Ligi ya soka Somalia kutimua vumbi leo

Sasa tunaelekea Somalia ambako wakati mwingi habari zinazosikika ni ghasia, ukame na mifarakano miongoni mwa koo. Lakini sasa tunapata habari nzuri. Baadaye leo, ligi ya kandanda nchini humo inatarajiwa kutimua vumbi. Mashindano ya mwaka huu yatashuhudia idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni.

Kuongezeka kwa hali ya utulivu katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu kumevutia kiasi cha wachezaji ishirini wa soka kutoka Nigeria, Kenya, Uganda na nchi nyingine za Kiafrika.

Pia kuna kocha wa kigeni. Ni John Maura ambaye anakuwa kocha wa kwanza wa kigeni kuongoza klabu kubwa nchini Somalia kwa karibu miaka thelathini. Ameingia mkataba wa mwaka mmoja kufundisha timu ya Banadir Sports Club, ambao ni mabingwa wa ligi ya Somalia.

Timu kumi zitakuwa zikiwania ubingwa mwaka huu, zikiwa zimeongezeka timu mbili kutoka nane za mwaka jana.

Kwa mji mkuu Mogadishu kuwa na kipindi kirefu cha utulivu katika zaidi ya miongo miwili, Mamlaka ya michezo nchini humo wnataka askari wa Umoja wa Afrika, AMISOM, nchini humo kuondoka katika uwanja wa mpira, eneo ambalo ni kubwa kuliko yote ya michezo nchini Somalia, ili michezo ianze kufanyika katika uwanja huo.

Lakini majeshi ya Amisom, ambayo yamekuwa katika uwanja huo tangu mwaka 2011, wakati kundi la wapiganaji wa Kiislam la al-Shabaab liliporudishwa nyuma, bado majeshi ya Amisom hayajaondoka katika uwanja huo.

Badala yake uwanja wa Banadir, uliofanyiwa matengenezo na shirikisho la soka duniani, FIFA mwaka jana, utatumika kwa michezo ya mwaka huu.-BBC

No comments: