Dar es Salaam. Mvua kubwa isiyotabirika inatarajiwa kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini hasa katika ukanda wa Pwani ya Kaskazini, maeneo ya Dar es Salaam, Tanga, Unguja na Pemba; pia katika ukanda wa Kaskazini Mashariki kwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Akitoa taarifa ya hali ya hewa jana kwa Januari na Februari mwaka ujao, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Agness Kijazi alisema mvua ya msimu katika maeneo hayo inatarajiwa kwisha leo.
Hata hivyo, alisema mvua kubwa ya nje ya msimu inatarajiwa katika kipindi cha Januari, 2015. Dk Kijazi alisema hali kama hiyo pia itaikumba mikoa ya Kagera, Mwanza, Shinyanga na Geita.
“Maeneo mengine yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka yatakuwa na mvua ya wastani. Maeneo hayo ni Mbeya, Rukwa, Katavi, Iringa, Lindi, Dodoma na Mtwara.
Dk Kijazi alisema mvua hiyo inasababishwa na ongezeko la joto linalolifanya anga kushindwa kutengeneza unyevunyevu ambao hugeuka kuwa mvua. “Ninawashauri wananchi kuchukua hatua ya kujikinga na athari za kiafya na mazingira zinazoweza kusababishwa na ongezeko la joto linaloendelea sambamba na mvua kubwa inayonyesha,” alisema Dk Kijazi.
Juzi, mvua kubwa ilinyesha jijini Dar es Salaam kwa saa mbili na kusababisha vifo vya watu wawili katika Wilaya ya Kinondoni kuleta kero kwa wasafiri wanaotumia vyombo vya moto na watembea kwa miguu.
Mitaa ya Azikiwe, Bibi Titi na Morogoro ambayo juzi ilijaa maji, jana ilionekana kuwa mikavu baada ya maji yote kukauka.
huku watumiaji wa barabara wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.
Yusuph Said, mmoja wa wafanyabiashara wa magezeti Mtaa wa Azikiwe, alisema eneo hilo hujaa maji kila mvua inaponyesha na kuwasababishi kufanya kazi yao katika mazingira magumu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura aliliambia gazeti hili jana kuwa hakuna madhara zaidi yaliyotokea ukiacha matukio ya watu wawili kufariki dunia kutokana na mvua hiyo.
Naye Kamanda wa Polisi Ilala, Mary Nzuki alisema: “Mkoani kwangu sijapokea taarifa yoyote ya maafa yaliyosababishwa na mvua mpaka sasa.” Kamanda Kihenya Kihenya wa Mkoa wa Kipolisi Temeke naye alisema hajapokea taarifa yoyote ya maafa.
Akizungumzia matukio ya mvua kipindi cha Oktoba – Disemba, 2014, Dk Kijazi alisema maeneo mengi ya nchi yalipata mvua za wastani hadi juu ya wastani isipokuwa maeneo machache ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Dodoma (Hombolo), Kilimanjaro (Same), Njombe, Mtwara na Lindi ambayo yalipata mvua za chini ya wastani.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa matukio ya mvua hizo ambayo yaliambatana na vipindi vifupi vya upepo mkali, yalisababishwa na kuimarika kwa ukandawa mvua magharibi mwa nchi ambao uliambatana na kuwepo kwa makutano ya upepo.
“Wananchi wajenge pia utamaduni wa kupanda miti ili kusaidia kupunguza kasi ya upepo unaombatana na mvua kubwa ambazo zinaweza kusababisha uharibifu wa mali na madhara kwao,” alisisitiza Dk Kijazi.
Peter Elias, Bakari kiango na Hadija Salum wa Mwananchi
No comments:
Post a Comment