Advertisements

Friday, December 12, 2014

UFANYEJE MWENZI WAKO ANAPOKOSA HAMU YA TENDO?- 4

Ni Ijumaa nyingine nzuri tunapokutana katika busati letu la mahaba. Uhali gani msomaji wangu? Bila shaka uko poa. Leo tunamalizia kujadili mada yetu kama inavyojieleza hapo juu.

Wiki iliyopita tuliishia kuangalia jinsi rafiki yetu Jackob alivyokuwa akitoa ushuhuda wa namna mke wake anavyosababisha akose hamu ya tendo la ndoa kutokana na uchafu uliokithiri, sababu kubwa ikiwa ni malezi ya mtoto wao mdogo. Niwashukuru wote ambao mlitoa michango yenu kumshauri Jackob na mkewe.

Nilichokigundua ni kwamba kumbe malezi ya mtoto mchanga hayawezi kuwa sababu ya kumfanya mwanamke awe mchafu. Akina mama wengi wameeleza kwamba uchafu ni hulka ya mtu, kama wewe ni msafi hata uwe unalea kachanga bado utaendelea kuwa msafi.

Jambo la kujifunza hapa kwa wale wanawake wanaojisahau, ni kwamba malezi ya mtoto yasikufanye ukajisahau. Mumeo naye ni muhimu na ili udumishe ndoa yako, unapaswa kujigawa vizuri kuwahudumia wote, mtoto na baba yake. Wanaume wengi huchepuka wakati wake zao wakiwa wananyonyesha kwa sababu ya kukimbia uchafu, jitahidi na wewe mwenzi wako asichepuke kwa kujiweka safi muda wote.

UPUNGUFU WA NGUVU ZA KIUME
Miongoni mwa sababu nyingine zinazosababisha wanaume wapoteze hamu ya tendo na wenzi wao, ni tatizo la upungufu wa nguvu za kiume na jinsi mwenzi wake anavyolichukulia. Utafiti unaonesha kwamba wanaume wengi waliopo ndani ya ndoa na wale ambao bado hawajaingia, wanasumbuliwa na tatizo la upungufu wa nguvu za kiume.

Lakini je, ni wanawake wangapi wanaojua kuwasaidia wenzi wao wenye tatizo hili ili wasizidi kuathirika kisaikolojia? Nimewahi pia kukutana na mwanaume aliyekuwa anaomba ushauri. Ndugu yetu huyu ambaye sitapenda kumtaja jina, alikuwa akilalamika kwamba yeye ana tatizo la upungufu wa nguvu za kiume na anaishi ndani ya ndoa.

Kilichomfanya aje kuomba ushauri, ni jinsi mkewe alivyokuwa ‘aki-mtreat’ anaposhindwa kukidhi haja zake wawapo faragha. Kwa masikitiko alisema mke wake amekuwa akimtolea maneno ya kejeli kwamba yeye si lolote kwa sababu hana uwezo wa kumfikisha faragha na amekuwa akimuita majina mengi mabaya kwa sababu hiyo.

Akaenda mbele zaidi kwa kueleza kuwa mkewe amemtishia kwamba endapo ataendelea kumuacha njiani, atadai talaka yake kwani haoni umuhimu wa kuishi kwenye ndoa. Akaendelea kulalamika kwamba hali hiyo imesababisha akose kujiamini na kupoteza kabisa hamu ya kushiriki tendo na mwenzi wake.

Najua huyu ni mmoja lakini wapo wengi wanaokutana na hali kama hii kwenye ndoa. Jambo ambalo ningependa wanawake wote walijue, ukosefu wa nguvu za kiume ni ugonjwa kama yalivyo magonjwa mengine. Hivi mumeo kama anaumwa malaria utakuwa unamsimanga na kumbeza au utamsaidia kumpeleka hospitali akatibiwe?

Kama mumeo hakidhi haja zako, usimchukie, elewa kwamba ana tatizo na mtu pekee anayeweza kumsaidia kupona tatizo hilo ni wewe. Mpe moyo, mfariji, muoneshe kwamba anao uwezo wa kupona tatizo lake kisha kwa pamoja saidianeni kutafuta tiba kwani zipo na upo ushahidi wa wanaume wengi ambao walikuwa na tatizo hilo lakini hivi sasa wamepona kabisa.

MATATIZO YA KIFEDHA
Tatizo lingine linalosababisha wanaume wengi wapoteze hamu ya kushiriki tendo la ndoa ni matatizo ya kifedha. Upo usemi uliozagaa kwenye jamii kwamba pesa ndiyo kila kitu. Kwa bahati mbaya wengi wanauamini usemi huu na matokeo yake unawasababishia matatizo makubwa ya kisaikolojia.

Wanawake wengi siku hizi wamekuwa na kasumba ya kuwapeleka puta wenzi wao katika suala zima la pesa. Kwamba mwanamke anajua kabisa kipato chako jinsi kilivyo lakini anakuwa anafosi umtimizie mahitaji yake hata yale ambayo yapo nje ya uwezo wa mwanaume.

Matokeo yake, mwanaume anapatwa na msongo wa mawazo na kupoteza kabisa hamu ya kushiriki tendo la ndoa. Hivyo ni vyema wanawake wakawasoma wenzi wao na kuepuka kuwapa presha inayohusu masuala ya fedha.

Mpaka hapo tumefikia mwisho, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Kwa maoni, ushauri, nicheki kwa namba ya hapo juu.

GPL

No comments: