ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 16, 2014

Ukawa watikisa kwa Wasira, Sitta, Membe


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetamba kutwaa vijiji na vitongoji wanavyotoka mawaziri, akiwamo Stephen Wassira (Ofisi ya Rais-Mahusiano na Uratibu);Samuel Sitta (Ushirikiano wa Afrika Mashariki) na Bernard Membe (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), katika matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa, yaliyotangazwa jana.

Maeneo mengine, ambayo Chadema wametamba kuyatwaa na kuwa chini ya himaya yao, ni anakotoka Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba; Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi na Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja.

Uchaguzi huo uliohusisha wagombea nafasi ya uenyekiti, ujumbe na makundi katika serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, ulifanyika nchini kote, Jumapili wiki iliyopita.

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu, alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari, katika mkutano ulioitishwa jijini Dar es Salaam jana kwa lengo la kuelezea yaliyojiri katika uchaguzi huo na hatua, ambazo chama hicho kinatarajia kuchukua.


Mwalimu alisema wanaendelea kupokea matokeo ya uchaguzi huo, kazi ambayo ilianza kufanywa na vijana 50 wa Chadema, kuanzia juzi usiku, kutoka sehemu mbalimbali nchini.Alisema pamoja na kwamba, bado hawajawa na matokeo kamili kwa asilimia 100, matokeo waliyonayo yanaonyesha kuwa wamefanya vizuri.

Hata hivyo, alisema hiyo haimaanishi kwamba, wamefanya vizuri kwa uchaguzi mzima na kwamba, bado wanaendelea kupokea matokeo.Alisema ikilinganishwa Chadema iliko na ilikotokea, chama hicho kiko mbali sana kwa mafanikio ya kisiasa kwa sasa tangu uchaguzi kama huo uliofanyika nchini kote mwaka 2009 na ule uliofanyika juzi.
Alitoa mfano wa Dar es Salaam, ambako alisema huko nyuma Chadema ilikuwa na mitaa saba.

Lakini akasema hadi kufikia jana, mitaa ambayo ilikuwa imekwisha kuhesabiwa na matokeo rasmi yaliyokwishatoka kwenye jimbo moja pekee la Ubungo, ilikuwa ni zaidi ya 23.

“Ukienda Kawe tuna mitaa mingi tumeshinda, ukienda Segerea tuna mitaa mingi tumeshinda, ukienda Ukonga ni hivyo hivyo, ukienda Kigamboni nafikiri waandishi wa habari mmeshanusa, tumesomba kweli kweli ule upande wa Kigamboni,” alisema Mwalimu.

Alisema hadi kufikia jana, walikuwa wanakadiria kuvuna mitaa zaidi ya kati ya 45 hadi 50 katika jiji la Dar es Salaam kutoka mitaa saba waliyokuwa wakiiongoza tangu mwaka 2009.

Hata hivyo, alisema idadi hiyo haiishii Dar es Salaam tu, bali hadi vijijini, ambako kuna maeneo Chadema haikuwa na kijiji wala kitongoji, kikiwamo kijiji cha Boma cha Waziri Sitta, kilichokuwa kikiongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Leo Sitta anapokuwa na matatizo yake, yatatatuliwa na Chadema, hakuna matatizo yatakayokwenda kutatuliwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba wala Bunge la Jamhuri, hapana. Matatizo ya familia yake tutayatatua sisi. Na tutatumia hekima na busara kubwa kuhakikisha kwamba, matatizo yake tunayamaliza,” alisema Mwalimu.
Aliongeza: “Lakini siyo hivyo tu, kuna maeneo mengi ya mawaziri.”

Alisema katika uchaguzi huo, Chadema pia imefanikiwa kutwaa Kijiji cha Kidundwe, kilichopo Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, anakotoka Naibu Waziri wa Maji, Makalla, ambacho awali kilikuwa kikiongozwa na CCM.

Pia alisema katika Wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya, anakotoka Waziri wa Uchukuzi, Dk. Mwakyembe, mwaka 2009 Chadema ilikuwa na mitaa miwili pekee, lakini katika uchaguzi wa juzi, wamefanikiwa kushinda mitaa 28, CCM ikiwa na mitaa saba, huku Halmashauri ya Mji Mdogo wa Kyela ikiwa chini ya Chadema kutoka CCM.

Alisema katika kijiji cha Kisangwe, kilichopo Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, anakotoka Waziri Wassira, kimetwaliwa na Chadema, pia kijiji cha Nyangao, kilichopo Wilaya ya Lindi Vijijini, anakotoka Waziri Membe, nacho pia kimetwaliwa na Chadema.

Mwalimu alisema pia kitongoji anachotoka Makamba na mji mdogo wa Sengerema anaotoka Ngeleja, umechukuliwa na Chadema.Alisema zimekuwa zikisikika propaganda dhidi ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, kwamba hatorudi kuliwakilisha jimbo hilo kwa madai kwamba, anadhibitiwa.

“Sisi hapa hatuna idara ya propaganda, tuna idara ya utafiti na mipango, wenzetu wana idara ya propaganda, wabaki na propaganda,” alisema Mwalimu.
Hata hivyo, alisema kati ya vijiji 43 vilivyoko katika jimbo la Singida Mashariki linalowakilishwa na Lissu, 41 vimechukuliwa na Chadema, huku CCM ikiambulia viwili.

DAR
CCM kimeibuka mshindi katika Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, kwa kujinyakulia viti vya uenyekiti 133 kati ya 195 huku Chadema kikijishindia viti 34 na Chama cha Wananchi (CUF), viti 15.

Hata hivyo, jumla ya vituo 13 havikuweza kufanikiwa kufanya uchaguzi katika manispaa hiyo kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za ukosefu wa vifaa vya kupigia kura kama vile wino wa kuwekea alama za vidole, karatasi za kura na vurugu zilizosababisha kuchanwa na kuchomwa moto kwa karatasi za kura na hivyo kuahirishwa.

Vituo vilivyoahirishwa katika Jimbo la Kinondoni ni Kinondoni Mjini, Mwenge, Alimaua A, Mwinyimkuu, Mtambani, Bwawani huku Ubungo ni King’azi B, Kibwegere, Jitegemee, Mabibo na Kawe kituo cha Tegeta.

Katika Jimbo la Ubungo, Chadema kimejinyakulia viti hivyo katika vituo vya Stopover, Michungwani, Farasi, Golani, Mavulunza, Kilungule A, Kimarabaruti, Baruti, Makoka, Marambamawili, Temboni, Kwa Yusufu, Msewe, Msakuzi Kusini, Mshikamano, Msakuzi, Makabe, Luis, Mji Mpya, Kinzudi na Kunguru.

Jimbo la Kawe, chama hicho kimetwaa mitaa ya Basihaya, Mbezi Kati, Ndumbwi, Mbezi Jogoo, Changanyikeni, Mlalakuwa, Makongo Juu, Mbuyuni, Mbopo, Salasala, Wazo, Malindi Estate, Kondo, Pwani na Nzasa kwa Jimbo la Kinondoni.

CUF kimejinyakulia viti hivyo katika vituo vya Bonde la Mpunga (Kawe), Matokeo, Sisikwasisi (Ubungo), Mpakani, Idrisa, Msisiri A, Msisiri B, Mchangani, Kisiwani, Makumbusho, Mkunduge, Kwa Tumbo, Sokoni, Mkwajuni na Kigogo Kati (Kinondoni).

Jimbo la Kawe, CCM kimejishindia viti 38, Chadema 12, CUF 1; Kinondoni CCM 33, Chadema 1, CUF 12 na Ubungo CCM 62, Chadema 21 na CUF 2.
CCM pia iliongoza katika wilaya ya Ilala. Mkurugenzi wa wilaya ya Ilala, Issa Mngurumi, alisema wilaya hiyo ina mitaa 153, iliyositishwa ni 27 na iliyokamilika kupiga na kuwasilisha matokeo ni 95.

Mngurumi alisema katika mitaa hiyo CCM wameshinda mitaa 71, CUF mitaa mitano ,Chadema 16 nafasi za wajumbe ni CCM imeshinda mitaa 225, Chadema 35 na CUF mitaa saba.
Mkurugenzi Manispaa ya Temeke, Fatuma Mwafujo, alitangaza matokeo ya awali yakionyesha kuwa kati a Kata ya Changombe kituo A, Mgombea wa CCM, alishinda kwa akura 313 na kufuatiwa na mgombea wa CUF kura 88.

Mwafujo alisema CCM pia ilikuwa imeshinda katika vituo vya Chang’ombe B, Yombo Dovya na Uwanja wa Taifa.CUF kilikuwa kimeshinda mitaa 33 na kati ya hiyo mitaa 10 ni katika jimbo la Temeke na mitaa 23 jimbo la Kigamboni.

Temeke, Bernard Mwakyembe, alisema wamefanikiwa kupata mitaa 32 kutoka mtaa mmoja waliokuwa nao baada ya uchaguzi wa mwaka 2009.Alisema kati ya mitaa hiyo, jimbo la Kigamboni wamepata mitaa 24 na jimbo la Temeke wamepata mitaa nane.

MBEYA
Licha ya CCM Mkoa wa Mbeya kikiendelea kupata ushindi katika matokeo ya awali katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vyama vinavyounda Ukawa navyo vimeonyesha ushindani mkubwa huku vikifanikiwa kushindana kuunda serikali katika mamlaka mbili za mji.

Kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyotelewa na Katibu wa CCM wa Mkoa huo, Mwangi Kundya, yanaonyesha kuwa, chama hicho kimefanikiwa kuzoa idadi kubwa ya vijiji hadi sasa.

Kundya alisema matokeo ya awali katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya lenye mitaa 181, CCM imepata mitaa 106, Chadema 71, NCCR-Mageuzi mmoja.Halmashauri ya Wilaya ya Chunya yenye vijiji 86, vijiji vilivyokamilisha hesabu ni 74, CCM ilipata vijiji 67 , Chadema saba, wakati kwa upande wa vitongoji, CCM 270 huku Chadema ikiambulia 18.

Halmashauri ya Wilaya ya Ileje ina vijiji 71 kati ya hivyo 32 vimekamilisha matokeo. CCM imepata vijiji 23, Chadema tisa.Halmashauri ya Wilaya ya Kyela vijiji vyote 93 vimekamilisha matokeo, CCM imepata 79, Chadema 13, huku uchaguzi wa kijiji kimoja ukiahirishwa.

Kwa upande wa vitongoji 469, CCM imepata vitongoji 377, Chadema 88, wakati vitongoji vinne uchaguzi utarudiwa.Mbarali yenye vijiji 102, CCM imeshinda 81, Chadema 16 na sita vitafanya uchaguzi wa marudio.

Kwa upande wa vitongoji 713, CCM imeshinda 570 , Chadema 79 na vitongoji 36 matokeo yake bado.Wilaya ya Mbozi, vijiji vilivyopo ni 125, kati ya hivyo 92 matokeo yake yalikuwa tayari, CCM kimepata viti 84 na Chadema vinane, huku 33 matokeo bado.Kwa upande wa vitongoji 664, CCM imepata 557, Chadema 110, CUF viwili, TLP ikiambulia kimoja.

Rungwe yenye vijiji 155 , CCM imepata 132, Chadema 22, CUF kimoja na vijiji vitano vitarudia. Kwa vitongoji 694 vilivyopo, CCM ilipata 578, Chadema 111, CUF viwili na TLP viwili.

Momba matokeo yake yamegawanywa katika sehemu mbili kutokana na wilaya kuwa na Halmashauri ya mji wa Tunduma.Kwa upande wa vijiji 72, CCM imepata 43, Chadema 24 na vijiji vitano vitarudia uchaguzi.

Kwa vitongoji 302, CCM 189, Chadema 53 na vitongoji 60 matokeo yake bado.Kwa upande wa mitaa katika Halmashauri ya mji wa Tunduma yenye mitaa 71, CCM imechukua 25, wakati Chadema imeongoza kwa kupata mitaa 46, hivyo kuunda Halmashauri ya mji.Wilaya ya MbeyaVijijini matokeo yalikuwa bado kutangazwa.

ARUSHA
Chadema Mkoa wa Arusha, ambacho mwaka 2009 kilishinda viti saba katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mwaka huu kimefanya vizuri na kushinda viti 75.Kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Juma Iddi, CCM imepata viti 78.

Alisema viti sita kati ya 78 ambavyo CCM imepata, wagombea wake walipita bila kupingwa.Alisema matokeo aliyoyatangaza ni ya nafasi za wenyeviti tu kwa sababu matokeo ya wajumbe bado yanafanyiwa uchambuzi.

Alifafanua kuwa kuna baadhi ya vituo wenyeviti wameshinda chama kimoja, lakini kwa nafasi za wajumbe wameshinda kwa vyama tofauti.Alisema vyama vingine vya ACT, NCCR Mageuzi, CUF na TLP vilipata kura sifuri katika vituo vyote.

TANGA
Kwa Halmashauri ya Jiji la Tanga CCM kimeongoza katika nafasi ya uenyekiti kwa kupata mitaa 118 huku CUF kikipata 60 na Chadema miwili.Mkurugenzi wa Jiji hilo, Juliana Mallange, alisema kwa upande wa wajumbe mchanganyiko CCM imepata 356 na viti maalum 230, CUF 117 na viti maalum 62 wakati Chadema watatu na viti maalum viwili.

Katika Halmashauri ya Kilindi, CCM imepita bila kupingwa katika vijiji 102 vya kata 20 imepita bila kupingwa kutokana na vyama vingine vya upinzani kushindwa kusimamisha wagombea.

Katika Halmshauri ya Mji Handeni katika mitaa 60, mitaa 50 CCM ilipita bila kupingwa na mitaa 10 iliyofanya uchaguzi CCM ilipata mitaa 57 na CUF mitaa mitatu.

MWANZA
Katika halmashauri ya Jiji la Mwanza yenye kata 18 yenye mitaa 175, vituo 279 na 329 vya kupigia kura, CCM pamoja na kupata ushindi wa ‘bure’ kwa baadhi ya mitaa, imenyakua mitaa 96 sawa na asilimia 54.86, Chadema 70 (40%), Cuf (7 sawa na 4%) na ACT mtaa mmoja (0.57%).

Mkurugenzi wa jiji la Mwanza, Hassan Hida, alisema mitaa waliyonyakua CCM ni pamoja na ile ambayo haikuwa na ushindani katika nafasi ya uenyekiti kutokana na wagombea wa Chadema kuwekewa pingamizi.

Alisema wapigakura 123,549 (asilimia 62) walijiandikisha ingawa lengo lilikuwa kujiandikisha watu 199,347, walifanikiwa kujitokeza na kupiga kura.

BUKOBA
Katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera matokeo ya 66 yametangazwa mpaka sasa, kati ya hiyo CCM imeshinda 35, Chadema 35 na CUF miwili huku katika nafasi ya wajumbe Chadema kimezoa 200, CCM 125 na CUF watano.

Aidha, wilaya ya Muleba yenye vitongoji 752 matokeo ya awali katika vituo 82 kati ya 166, CCM imezoa viti 50, Chadema 32 ikiwa ni wentyeviti wa vijiji.

CHATO
Mjumbe wa Bunge la Katiba kupitia tiketi ya wavuvi, Tulutoza Bagambisa (CCM), alibwagwa na mgombea Chadema baada ya kupata kura 91 dhidi ya 167 za Fares Kabunazya.
Kati ya vitongoji 20 vya kata ya Chato, CCM imeambulia vitongoji vitano tu ambavyo ni Chato Kati, Msikitini, Uswahilini, Simu na Ushirika huku Chadema wakiibuka kidedea kwa vitongoji 15.

Hali hiyo ni tofauti na uchaguzi huo wa miaka mitano iliyopita, wakati Chadema walipata kitongoji kimoja tu cha Elimu na vingine vyote kuchukuliwa na CCM katika jimbo hilo linaloongozwa na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli.

SHINYANGA
Msimamizi wa uchaguzi ambaye ni mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Festo Kang’ombe, alisema matokeo ya viongozi wa mitaa 55 mjini Shinyanga, Chadema wamechukua 29, CCM 26.

Kang’ombe alisema katika vijiji 17, CCM wamechukua 14, Chadema viwili na CUF kimoja, na upande wa vitongoji 84, CCM wamepata 65, Chadema 18 kitongoji kimoja cha Katunda hakijapiga kura.

IRINGA
Katika Halmashauri ya Iringa, nafasi za uenyekiti wa mitaa CCM imepata 126, Chadema 54 na CUF moja.Wajumbe wa serikali za mitaa CCM 389, Chadema 160, CUF wawili , NCCR mageuzi moja.Wajumbe wa viti maalum CCM kura 253 na Chadema 104.

KILIMANJARO
Manispaa ya MOshi CCM imepata mitaa 28 54 huku Chadema ikipata mitaa 26.Katika Mji mdogo wa Himo CCM vitongoji 11, NCCR-Mageuzi vine na Chadema mitatu.Katika jimbo la Hai, CCM imeshinda vijiji 29, Chadema vijiji 23, huku uchaguzi katika vijiji vitano jimboni humo ukitarajiwa kurudiwa.

DODOMA
Katika Halmashauri ya Kondoa yenye kata 28, CCM kimeshinda uenyekiti wa vijiji katika kata 12, CUF viwili na Chadema viwili.Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa halmashauri ya Kondoa, Isdory Mwalongo , alisema kwa vitongoji, CCM imeshinda viti 89, CUF 13 naChadema viwili.Wajumbe wa serikali ya kijiji CCM 97, CUF 15 na viti maalum CCM 83 na CUF 14.

SINGIDA
Manispaa ya Singida CCM, kimeshinda nafasi zote 50 za uenyekiti wa mitaa sawa na asilimia 100..
Kwa mujibu wa Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Joseph Mchina chama hicho kimeshinda kwenye vijiji 19 kati ya 20 vya Manispaa yao sawa wa aslimia 95.

"CUF ilishinda nafasi moja ya kijiji sawa na asilimia tano, Chadema na ACT havikuambulia kitu, " alisema. Katika vitongoji 90, CCM imetwaa 81 sawa na aslimia 90, CUF nane (asilimia 8.9) na Chadema kimoja ( aslimia 1.1).

CCM imepita bila kupigwa kwenye nafasi za uenyeviti wa vijiji sita (aslimia 30), vitongoji 37 ( 41.1), mitaa 13 ( 26) na CUF vitongoji viwili.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Msimamizi wa uchaguzi , Mohamedi Nnkya, alisema bado wanaendelea kuhesabu kura na matokeo kamili yatatangazwa leo.

Imeandikwa na Muhibu Said, Thobias Mwanakatwe, Isaya Kisimbilu, Christina Mwakangale, Kamili Mmbando, John Ngunge, George Tarimo, Lulu George, Kamili Mmbando, Leonce Zimbandu na Enles Mbegalo, Daniel Mkate na Rose Jacob, Lilian Lugakingira, Daniel Limbe) na Marco Maduhu, Godfrey Mushi, Charles Lyimo, Agusta Njoji na Ismailly Jumbe.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: