Advertisements

Friday, December 12, 2014

VYOMBO VYA HABARI VINAWEZA KUZUIA AU KUWA CHANZO CHA MACHAFUKO

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Jan Eliasson akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo mpya wa thathmini na utambuzi wa viashiria vinavyoweza kama visipodhibitiwa mapema kuleta uhalifu, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita. uzinduzi huo umefanyika siku ya Alhamisi hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa
Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Ramadhan Mwinyi akizungumza wakati wa hafla hiyo ambayo iliandaliwa kwa pamoja na Wakilishi za Kudumu za Tanzania na Italia katika Umoja wa Mataifa pamoja na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuzuia mauaji ya Kimbari na Wajibu wa Kulinda Raia
Sehemu ya Washiriki wa uzinduzi huo ambapo mkazo mkubwa ulikuwa ni ushiriki wa wadau wengine kama vile vyombo vya habari na asasi zisizo za kiserikali na wajibu wao katika utambuzi wa viashiria vya uvunjifu wa amani na hatua mbalimbali ambazo vyombo hiyo vinaweza kusaidia kuzuia uvunjifu huo

Na Mwandishi Maalum, New York

Imeelezwa kuwa waandishi wa habari pamoja na vyombo wanavyofanyia  kazi wana  nafasi kubwa ya ama kuchochea  uibukaji wa  machafuko   katika nchi zao au  kuyazuia  kwa kutumia kalamu  zao.
Hayo yameelezwa  siku ya  Alhamis  hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa wakati wa   hafla ya   uzinduzi wa   mfumo mpya  wa uchambuzi unaolenga kutathmini  viashiria  hatarishi vya uhalifu, mauaji ya  kimbari ,uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita
Hafla ya uzinduzi  wa mfumo huo ambao umeandaliwa kwa ushirikiano baina ya  Ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Mauaji ya kimbari na Ofisi ya Umoja wa  Mataifa kuhusu wajibu wa kuwalinda raia (R2P) iliandaliwa  kwa ushirikiano wa Wakilishi za  Kudumu za  Tanzania  na Italia katika Umoja wa Mataifa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu uzuiaji wa mauaji ya Kimbari na ulinzi wa Raia. Uzinduzi uliohudhuriwa  na  Naibu Katibu  Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Jan Eliasson.
Mfumo huo( framework of  Analysis for Atrocity Crimes, a tool for prevention) pamoja na mambo mengine licha ya  kutoa ufafanuzi, tafsri  na maelezo ya kina kuhusu viashiria na mazingira ambayo yanaweza kupelekea  au  kusababisha mauaji ya  halaiki au kimbari,   uhalifu dhidi ya binadamu  na uhalifu wa makosa ya kivita  unapanua wigo wa kuvishirikisha vyombo vya habari na asasi za kiraia kama wadau  muhimu  wa si tu   kufanya tathmini ya awari ya viashiria hivyo  lakini ikiwa ni pamoja na kuchukua  hatua za mapema za kuuzia kuibuka kwa matatizo hayo katika jamii.
Vyombo vya habari na Asasi za kiraia vinaelezwa kama wadau muhimu licha ya   ukweli kwamba wajibu wa kwanza wa kuzuia machafuko ya aina yoyote ile pamoja na  kutoa  ulinzi wa raia ni wa serikali kuu.

 Na kwa sababu hiyo imeshauriwa kuwa waandishi wa habari wanapashwa   kwanza  kutambua vyema  viashiria hatarishi dhidi ya Amani na usalama na kuwa nyenzo muhimu ya kuzuia kuibuka kwa  uhalifu huo badala ya  kuwa sehemu ya   uhalifu huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo huo, Naibu  Katibu Mkuu wa Umoja wa  Mataifa, Bw. Jan Eliasson  amesema ,  mwaka 2014  umeshuhudia umwagaji mkubwa wa damu kuliko miaka mingine yoyote.
Amesema hali  hiyo inatoka na  ama kwa Jumuiya ya Kimataifa kutotambua mapema na katika hatua za awali  za dalili ya kutokea  uhalifu na uhalifu dhidi ya binadamu au ni kwa jumuiya  ya kimataifa kutofautiana kimtazamo na kimaslahi kuhusu njia muafaka za kuzuia  uhalifu huo.
Akasema  uzinduzi wa mfumo huo unatoa fursa kwa  serikali na wadau wengine  ya kutambua mapema viashiria vya uwepo wa mazingira hatarishi yanayoweza kusababisha mauaji ya kimbari, uhalifu  dhidi ya binafamu na uhalifu wa kivita. Lakini kubwa na la msingi anasema ni  kuzuia uhalifu huo kabla  haujatokea.
Amesisisitiza kuwa  uhalifu dhidi ya binadamu  hauibuki mara moja, bali ni jambo linalokuwa limepangwa  na kuandaliwa  kwa muda mrefu ukiwashirikisha wadau mbalimbali.
Amesema   hali ilivyo  hivi sasa ni kwamba jumuiya ya kimataifa imejikuta   ikijikita zaidi  katik a kushughulikia matatizo ambayo tayari yameshajitokeza badala ya  kuyazuia katika  hatua za awali hali inayosabibisha kutumia gharama kubwa zaidi.
Kwa upande wake Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan Mwinyi, pamoja na kuelezea umuhimu  na manufaa ya mfumo huo wa  tathmini ya  viashiria  vya   uwepo wa  mazingira hatarishi. Amesema Tanzania inaunga mkono ushirikishwaji wa wadau mbalimbali  kama  sehemu  muhimu  katika eneo zima la  Amani, usalama na  ulinzi wa raia.
Hata hivyo ametahadharisha kuwa pamoja na kutambua mchango wa wadau  wengine, ni vema basi pawepo na utaratibu wa uwajibikaji wa wadau hao ikiwa ni pamoja  usimamizi lengo likiwa ni  uwajibikani kama  baadhi ya wadau hao wanakuwa chanzo au chachu cha machafuko hayo.
Aidha  Balozi Mwinyi  amesema Tanzania ni  rafiki wa  mchakato huo  wa  wajibu wa kuwalida raia (R2P). Lakini  ni ukweli usionpingika kuwa  dhana hiyo ya  wajibu wa kuwalinda raia bado  imegubikwa na utatamwingi na kwamba kwa nchi nyingi hususani za afrika bado dhana hiyo haijakubalika au haijapokelewa vema.
Amesema sababu ya kutopokelewa vema kwa dhana hiyo na waafrika kunatokana na ukweli kuwa dhana hiyo inalenga zaidi katika kuingilia masualaya ndani ya  nchi husika na pia ni dhana inayolenga katika kuleta mabadiliko ya kiuongozi katika  nchi husika ( regime change).
Na kwa sababu hiyo, Mwakilishi huyo wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa amesisitiza haja na umuhimu wa kuwapo na usimamizi na utambuzi maalumu kuhusu dhana  hiyo ya  wajibu wa kulinda raia bila ya kuingilia uhuru wa nchi husika.
Katika uzinduzi huo, baadhi ya wachangiaji wa  mfumo huo  wa thathmini pamoja na dhana ya R2P   akiwamo  Katibu Mkuu  Msaidizi Mwandamizi anayehusika  na  masuala ya  uzuiaji wa mauaji ya kimbari, Bw. Adama Dieng  wameielezea Tanzania kama nchi ambayo ni kielelezo halisi cha Amani, usalama na utulivu ikilinganishwa na  mataifa mengine Barani Afrika.
Akizungumzia wajibu wa vyombo vya habari katika kuzuia machafuko ambayo  yanaweza kupelekea kutoka kwa matukio ya uhalifu na makosa ya jinai dhidi ya binadamu. Bi, Agnes kut Callamard kutoka Chuo Kikuu cha Columbia. Amesisitiza haja na umuhimu  kwa waandishi wa habari  kuzingatia maadili ya kazi zao  huku akitilia mkazo   utendaji kazi huru wa vyombo hivyo  ikiwa ni pamoja na  haki ya kupata habari na kusambaza habari.
Amesisitiza kuwa  uzoefu  umeonyesa kuwa  sehemu  nyingi  ambapo kumetokea machafuko, vyombo vya habari  vimebainika kuchangia kwa asilimia kubwa  uwepo wa hali  hiyo.
Naye B.i Peggy Hicks kutoka Human Rights Watch  akizungumzia kuhusu nafasi ya asasi zisizo  za kiserikali  pamoja na mambo mengine amesema kuwa   Tanzania ina mfumo mzuri  unaoziwezesha asasi zisizo za kiserikali kutekeleza majukumu yao pasipo kuingiliwa sana na serikali kuu.  Na kusisitiza  asasi hizo za tanzania  hazihitaji kujifunza kutoka nje juu ya utekelezaji wa majukumu yao.

Aidha  katika uzinduzi huo   Tanzania  imeelezwa pia kuwa  Taifa ambalo   kumekuwapo na  ustawi, maridhiano  na  kuvumiliana kwa hali ya juu  baina ya  madhehebu mbalimba ya dini. 

No comments: