Advertisements

Saturday, January 24, 2015

Diwani aidai CCM fidia ya bilioni nne

Diwani wa CCM kata ya Magomeni, Julian Bujugo

Diwani wa CCM kata ya Magomeni Dar es Salaam, Julian Bujugo, amekishtaki chama hicho akitaka kimlipe fidia ya Shilingi bilioni nne kwa kumsababishia hasara.

Bujugo, aliwaambia wanahabari kuwa amefungua shauri la madai na mlalamikiwa ni Jumuiya ya Wazazi ya CCM.

Alisema hatua hiyo inatokana na jumuiya hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Abdallah Bulembo, ‘kumpora’ Chuo cha Kilimo na Mifugo Kaole cha mjini Bagamoyo, ambacho ni mali ya jumuiya hiyo.

Hata hivyo, Bulembo amemkosoa Bujugo kwa hatua hiyo na kusema aliwahi kufungua kesi kama hiyo iliyotolewa hukumu na Jaji John Utamwa wa Mahakama Kuu na kutakiwa kulipa fidia ya Shilingi milioni 150.

Kwa upande wake, Bujugo alisema uporwaji wa chuo hicho ulifanywa hivi karibuni na Bulembo akishirikiana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, akiwamo Mkuu wa Wilaya, Ahmed Kipozi.

Hivi karibuni, Bulembo alitangaza kukisimamisha chuo hicho kwa madai kuwa mwendeshaji Bujugo, alibadili matumizi ya iliyokuwa shule ya sekondari Kaole na kuanzisha chuo hicho bila ridhaa ya jumuiya hiyo.

Lakini Bujugo alisema (huku akionyesha nakala vivuli vya makubaliano na malipo kati ya pande mbili hizo), kuwa jumuiya hiyo imeshindwa kumheshimu badala yake kumvua Umeneja na uendeshaji wa chuo hicho kwa mabavu.

Alisema katika hali iliyomstaajabisha, Bulembo akiwa na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani Bagamoyo, walimvua uendeshaji wa chuo hicho na kukisimamisha.

Alidai kuwa makubaliano waliyoyafikia kati yao, ikiwa ni pamoja na kuilipa jumuiya hiyo asilimia tano ya mapato yake, yalimuingizia gharama zikiwamo za ujenzi na ukarabati wa majengo, maabara, vifaa, mifugo na stahiki za wanafunzi na wafanyakazi ambavyo kiasi chake kinakadiriwa kuwa Shilingi bilioni nne.

Akizungumzia sakata hilo, Bulembo alisema chuo hicho hakiwezi kufunguliwa na badala yake kuwataka wazazi na wanafunzi kufuatilia madai yao katika mamlaka husika ikiwamo kupitia kwa Afisa Elimu wa mkoa wa Pwani.

“Bujugo ana majengo katika shule zake, anachapaswa kukifanya si kusababisha hasara kwa wanafunzi na kuendeleza malumbano, awachukue wanafunzi waliomlipa fedha awapeleke kwenye majengo yake ili wamalizie kozi zao huko,” alisema.

Pia, Bulembo alitoa wito kwa serikali kupitia wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi, kufuatilia kwa akribu uendeshaji wa taasisi za elimu nchini ili kuabaini na kudhibiti kasoro zinazochangia kuwaathiri wanafunzi, walimu na wazazi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: