Advertisements

Sunday, January 25, 2015

Rais Kikwete awasili Saudi Arabia kuhani msiba wa Mfalme

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili katika Uwanja wa Ndege wan Kijeshi mjini Riyadh, Saudi Arabia, asubuhi ya Jumapili, Januari 25, kuhani kifo cha Mfalme Abdullah bin Abdul Aziz al Saud aliyefariki Alhamisi na kuzikwa Ijumaa ya wiki iliyopita.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili mjini Riyadh, Saudi Arabia,asubuhi ya Jumapili, Januari 25, 2015, kuhani kifo cha Mfalme Abdullah bin Abdul Aziz al Saud aliyefariki Alhamisi na kuzikwa Ijumaa ya wiki iliyopita.

Baada ya kuhani msiba wa Mfalme Abdullah, Rais Kikwete ataendelea na safari yake kwenda nchi za Ujerumani na Ufaransa kwa ziara za kikazi.

Mjini Berlin, Ujerumani ambako Rais Kikwete alitarajiwa kuwasili kesho, Jumatatu, Januari Ishirini na Sita, akitokea Riyadh, Saudi Arabia, anatarajiwa kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Global Alliance for Vaccines and Immunization (GAVI Alliance) ambako viongozi mbali mbali duniani watajadili jinsi ya kuboresha mipango ya utoaji chanjo kwa watoto wadogo hasa katika nchi zinazoendelea.


Baada ya kumaliza ziara yake Ujerumani, Rais Kikwete atakwenda Ufaransa ambako miongoni mwa mambo mengine atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Ufaransa.

Aidha, Rais Kikwete atafungua jengo jipya la Ubalozi wa Tanzania katika Ufaransa na pia nyumba ya balozi.

Rais Kikwete baada ya kumaliza ziara zake za kikazi katika Ujerumani na Ufaransa atakwenda Addis Ababa, Ethiopia, kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).


Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
25 Januari, 2015

1 comment:

Anonymous said...

hebu tuambiyeni toka ashike hatamu raisi wetu amesafiri na kuwa angani mika mingapi. na kuna nchi raisi wetu hajatia mguu wake?