ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 2, 2015

TAMBWE AISHITAKI SIMBA FIFA

Mshambuliaji wa Yanga Mrundi, Amissi Tambwe. 

Na Wilbert Molandi
MSHAMBULIAJI wa Yanga Mrundi, Amissi Tambwe ameiambia klabu yake ya zamani, Simba kuwa hadi kufikia leo Ijumaa akiwa hajalipwa fedha zake anazodai, basi atakwenda kushtaki kwenye Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Tambwe anaidai Simba dola 7,000 (zaidi ya Sh milioni 11) kutokana na klabu hiyo kusitisha mkataba wake hivi karibuni kiasi ambacho kinafanana na kile anachodai aliyekuwa kiungo wa timu hiyo Pierre Kwizera, ambaye naye alisitishiwa mkataba klabuni hapo.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Tambwe alisema kuwa hatakubali kuona haki yake inapotea kirahisi, hivyo atapambana hadi dakika za mwisho kuhakikisha anazipata fedha zake.“Mimi nilikubali kuondoka kwa amani Simba lakini nashangaa kuona hali hii inayoanza kutokea kwa viongozi. Tulikubaliana vizuri kabisa, wasitishe mikataba yetu kwa kutulipa dola 7,000 kila mmoja, lakini hadi leo hii bado hawajatulipa, tunaona siku zinazidi kwenda.

“Tumepanga kwenda kushtaki Fifa ikiwa kufikia Januari 2 (leo) tuliyokubaliana watakuwa hwajatulipa, ajabu wanafanya kitu ambacho siyo cha kiungwana kwa kutangaza kuwa wametulipa kitu ambacho siyo kweli,” alisema Tambwe.

Gazeti hili lilipowasiliana na Katibu Mkuu wa Simba, Stephene Ally na Ofisa Habari, Humphrey Nyasio ambao walisema kuwa wachezaji hao wameshawalipa.

Wakati huohuo, suala la wachezaji Waganda wa Simba, Juko Mushidi na Simon Sserunkuma kukosekana katika kambi ya klabu hiyo bado lina utata kutokana na kudaiwa kuwa wachezaji hao bado wanadai kila mmoja anadai dola 20,000 (zaidi ya shilingi milioni 34).

“Mchezaji mwenye taarifa ni (Emmanuel) Okwi pekee, hao akina Mushidi na Simon wanadai fedha za usajili ambazo hawajamaliziwa, kila mmoja anadai dola 20,000,” kilisema chanzo.
CREDIT:GPL

No comments: