Advertisements

Wednesday, January 21, 2015

TFF yafagilia marefa kupigwa

Wakati beki wa zamani wa kushoto wa Yanga, Stephano Mwasika alifungiwa mwaka mzima kwa kumpiga refa, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetoa adhabu inayolea vurugu michezoni kwa kumfungia mechi tatu winga Haroun Chanongo wa Stand United kwa kumpiga mwamuzi.

Nahodha wa zamani wa Manchester United, Eric Cantona alifungiwa miezi nane na kutozwa faini ya paundi 30,000 (Sh. milioni 79) kwa kumpiga teke shabiki aliyekuwa jukwaani, lakini TFF jana ilitangaza kumfungia Chanongo mechi tatu tu na kumpiga faini ya Sh.500,000 kwa kumpiga teke refa wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Polisi Moro kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro Januari 3.

Katika kuhakikisha kwamba tukio hilo halijirudii, Cantona alivuliwa unahodha wa timu ya taifa ya Ufaransa na hakuitwa tena katika kikosi hicho hadi alipostaafu soka.

Adhabu ya Chanongo ambayo haimfanyi mtu kujutia alichokifanya, imekuja katika kipindi ambacho soka la Tanzania limetawaliwa na matukio mengi ya kupiga marefa viwanjani huku pia ikionyesha udhaifu mkubwa wa tofauti ya viwango vya adhabu vinavyotolewa na shirikisho hilo la soka nchini katika matukio yanayofanana.


Misimu miwili iliyopita, TFF ilimfungia Mwasika mwaka mmoja na kumpiga faini ya Sh. milioni moja kwa kumpiga refa Israel Nkongo katika mechi yao ya VPL waliyolala 3-1 dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam.

Akizungumza na wanahabari jana, Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Boniface Wambura, alisema kuwa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) imewapiga faini na kuwafungia wachezaji wawili huku baadhi ya makocha na viongozi ikiwafikisha kwenye Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya uchunguzi zaidi kabla ya kuadhibiwa.

Alisema adhabu ya Chanongo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu. Chanongo anaitumikia Stand United kwa mkopo akitokea Simba ambako alikuwa amefungiwa kutokana na kilichoelezwa kuwa utovu wa nidhamu katika mechi yao ya raundi ya tano ya VPL waliyotoka 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons mjini Mbeya Oktoba 25, mwaka jana.

Wambura alisema kipa Amani Simba wa Oljoro JKT amepigwa faini ya Sh. 300,000 kwa kukataa kupeana mkono na viongozi wakati wa kusalimia kabla ya kuanza kwa mechi yao dhidi ya Toto Africans iliyofanyika jijini Mwanza. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 14 ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Alisema timu ya Polisi Mara imepigwa faini ya Sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake wakati wa mechi ya FDL dhidi ya Mwadui ya Shinyanga iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma. Pia Polisi Tabora imepigwa faini ya Sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake kwenye mechi namba 40 dhidi ya Geita Gold, adhabu ambazo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 41.

12 WATINGA KAMATI YA NIDHAMU
Wambura alisema wachezaji Dihe Makonga, Swalehe Idd Hussein, Ramadhan Mwinyimbegu na Shaibu Nayopa wa Oljoro JKT, pamoja na Nassib Lugusha wa Polisi Dodoma wanalalamikiwa katika Kamati ya Nidhamu kwa kushambulia waamuzi na kufanya vurugu kwenye benchi la timu pinzani katika mechi zao za FDL.

Alisema Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa Polisi Mara, Clement Kajeri analalamikiwa kwa kuongoza mashambulizi dhidi ya waamuzi kwenye mechi kati ya timu yake na Mwadui iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.

Wambura alisema Mtunza Vifaa wa Rhino Rangers, Albert Mbunji naye anapelekwa katika Kamati hiyo kwa kupinga maamuzi na kuwatukana waamuzi kwenye mechi dhidi ya Polisi Dodoma iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Aliongeza kwamba pia Mtunza Vifaa wa Oljoro JKT, Eliud Mjarifu analalamikiwa kwa matukio mawili; alimpiga Kocha wa Burkina Faso, CR Mwakambaya kwenye mechi ya FDL iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Pia alimtukana mwamuzi wa akiba (fouth official) Mussa Magogo kwenye mechi dhidi ya Toto Africans iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Kocha wa Polisi Tabora, Kim Christopher analalamikiwa kwa kumtolea lugha chafu mwamuzi wa mechi kati ya timu yake na Panone FC iliyochezwa Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Alisema kuwa Msimamizi wa Kituo cha Musoma, Katibu wa Chama cha Soka Mara (FAM), Mugisha Galibona naye anapelekwa katika Kamati ya Nidhamu kwa tuhuma za kutotoa ushirikiano kwa maofisa wa mechi na kuchochea maofisa hao (waamuzi) kupigwa.

Wambura alisema Kamati ya Soka la Wanawake ya TFF imependekeza Katibu wa Chama cha Soka Simiyu, Emmanuel Sologo, na Kaimu Katibu wa Chama cha Soka Singida (SIREFA), Gabriel Gunda kupelekwa kwenye kamati ya Nidhamu kwa matukio mbalimbali yaliyojitokeza kwenye mechi za Kombe la Taifa la Wanawake.

Sologo anatuhumiwa kumpiga kibao mwamuzi wa mechi ya marudiano kati ya timu yake ya Simiyu na Shinyanga iliyochezwa mjini Shinyanga, tukio ambalo lilimfanya mwamuzi huyo avunje mchezo.

Naye Gunda analalamikiwa kwa kushindwa kuhakikisha timu yake ya Singida inaingia uwanjani kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Dodoma iliyokuwa ifanyike kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: