ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 8, 2015

Tibaijuka, Chenge watumiwa ankara kodi ya Escrow

Naibu waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba

Serikali imesema imeshachukua hatua za kulipwa kodi kutoka kwa watu walionufaika na mgawo wa fedha zilizochotwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, amesema wizara yake imeshawaandikia ankara za malipo ya kodi wadaiwa wote waliopokea mgawo huo.

Nchemba, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), alisema serikali imewapatia siku 30 watu hao ili kuhakiki ankara hizo na kulipa madeni hayo ambayo yalitokana na mgawo wa fedha hizo.

Nchemba aliyabainisha hayo jana jijini Dar es Salaam alipotembelea wodi ya watoto katika Hospitali ya Mwanyamala pamoja na kutoa misaada katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Chakuama na kushiriki zoezi la kuchangia damu salama, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 40 ya kuzaliwa kwake.


Akijibu swali aliloulizwa na waandishi wa habari kuhusu agizo la serikali kupitia wizara yake kuwa watu hao ambao walipata fedha kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd, James Rugemalira, wanapaswa kulipa kodi tangu Desemba 31, Mwigulu alisema tayari taratibu zote zimefanyika na walikabidhiwa hati za malipo tangu Januari Mosi, mwaka huu.

“Mamlaka ya Mapato nchini, tayari imeshawaandikia mahesabu yao na wamepewa mwezi mmoja wa kuhakiki madeni yao kupitia wakaguzi wao wa mahesabu, kama mahesabu yako sawa ama la baada ya hapo wanapaswa kulipa deni hilo ambalo ni kodi inayopaswa kuingia serikalini ikahudumie jamii,“ alisema Nchemba.

Alifafanua kuwa malipo ya mahesabu yao yanatokana asilimia ya faida walizopata kutokana na mgawo wa fedha walizopata.
“Wote hawa watatakiwa kulipa kodi hizi kulingana na faida walizozipata katika matumizi ya fedha hizo,” alisema Nchemba.

Kuhusu serikali kulinda watendaji wabovu na wabadhirifu wa fedha za umma na wakwepa kodi, Nchemba alisema kupitia sera ya Katiba mpya, watu kama hao wanapaswa kuadhibiwa kwa kufukuzwa kazi, kufilisiwa mali zao na kufungwa jela.

Alisema zamani watendaji wa serikalini waliokuwa wanafanya makosa walihamishwa vituo vya kazi kutokana na uhaba wa wasomi, lakini sasa waliosoma ni wengi na wamekosa ajira, hivyo hakuna sababu ya kuendelea na sera hiyo.

“Hatuwezi kuendelea kulea sheria za zamani, watendaji wabovu na wakwepa kodi. Lazima watu kama hawa wanaowanyima Watanzania haki zao ambazo zinatokana na kulipa kodi, hapa hospitali kuna watoto wanakufa kwa kukosa dawa ambazo zingenunuliwa na kodi za Watanzania, sasa hatuwezi kulea wanaokwepa kulipa kodi,” alisema Nchemba.

Alifafanua kuwa lengo la kupita katika hospitali hiyo, ni kujionea hali halisi ya sekta ya afya na adha wanayoipata wagonjwa pamoja na wahudumu wa afya.

“Mimi kama Naibu Waziri wa Fedha, kupita kwangu hapa kunanipa mafunzo na uzito wa jambo wakati wa kutenga bajeti ya Wizara ya Afya ninafahamu hali halisi na mahitaji husika,” alisema Nchemba.

Alisema pia zoezi hilo litamsaidia kuongeza kasi ya kupambana na walipa kodi na kuhakikisha wanaotakiwa kulipa kodi wanalipa ili fedha hizo ziwafikie Watanzania kwa usawa.

Novemba 26, mwaka jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) , Zitto Kabwe, aliwasilisha bungeni ripoti ya kamati hiyo baada ya kupitia taarifa ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Akaunti ya Tegeta Escrow na kuwataja watu mbalimbali waliopokea mgawo kutoka kwa Rugemalira ambao wanapaswa kuulipia kodi.

Aliwataja kuwa ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (Sh. bilioni 1.6); Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (Sh. milioni 40.4); Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh. milioni 40.4); Mbunge mstaafu Paul Kimiti (Sh. milioni 40.4); Msajili wa zamani wa Hazina na Mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk. Enos Bukuku (Sh. milioni 161.7).

Wengine ni Jaji Profesa Eudes John Ruhangisa (Sh. milioni 404.25) na Jaji Aloysius Mujulizi (Sh. milioni 40.4).

Kamati iliwataja wengine kuwa ni watumishi wa umma ambao ni Mtendaji Mkuu wa wa Rita, Philip Saliboko (Sh. milioni 40.4); aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Emmanuel Ole Naiko (Sh. milioni 40.4) na Mtumishi wa TRA, Lucy Appolo (Sh. milioni 80.8).

Wapo pia viongozi wa dini waliotajwa na Zitto na kiasi cha fedha walichopokea ambao ni Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini (Sh. milioni 80) Askofu Eusebius Nzigilwa (Sh. milioni 40.4) na Padri Alphonce Twimanye Simon (Sh. milioni 40.4), ambao walipewa fedha hizo kupitia Benki ya Mkombozi.

 
CHANZO: NIPASHE

3 comments:

Anonymous said...

Dear Minister, is that the final outcome of the matter. To knowingly or unknowingly take stolen funds is a criminal offence. So mpya hiyo, kumbe if you pay tax on it then it is all yours? Is that the case Hon Minister?

And how come there is no code of conduct for MPs, they just resign as Ministers and continure being MPs. What message does this send to the public?

Anonymous said...

ukoo wa panya wanajuana wenyewe mwisho wasiku wanakuwa panya buku. hakuna kitu katika ccm wote si wasafi wanabaki kusafishana na pia kubomoana.hakuna kitu hapo.

siku tukiacha kuwashabikia wanasiasa ndo siku itayokuwa ukombozi wetu sisi wananchi wanyonge tusio na mbele wala nyuma.

kata kuwashabikia wana siasa na vyama vyao kata kata ewe mnyonge mwenzangu,tafuta ugari wako ule na ushibe na watoto wako ukibakisha mpe na jirani yako mmonge mwenzako.

Anonymous said...

nasikia anajiita sokoine wa 2,my goodness lord mmmh.kazi kweli ipo.Watu wanapenda kujifananisha sehemu ambazo hata hawafanani napo!!!!

vijimambo team please msibaniye hii comment ahsanteni