ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 26, 2015

UNAMPENDA, UNATAKA NDOA

Ni wiki nyingine ambapo Mwenyezi Mungu ametujaalia kukutana katika busati letu la mahaba kujadiliana mambo mbalimbali yanayohusu uhusiano wa kimapenzi. Ni matumaini yangu kuwa mada ya wiki iliyopita ilikuingia vizuri na sasa unayafanyia kazi yale tuliyojadiliana.

Karibu tena tujadiliane kuhusu mada ya leo kama inavyojieleza; unampenda na unataka kumuoa lakini hujui pa kuanzia, unapaswa kufanya nini?

Maendeleo ya teknolojia yamebadilisha mambo mengi katika maisha yetu ya kila siku. Zamani ilikuwa kama kuna mwanamke au mwanaume unampenda, basi lazima uhangaike sana mpaka utakapopata nafasi ya kuzungumza naye, na kama huna ujasiri wa kumtongoza ana kwa ana basi ndiyo umemkosa.
Siku hizi mambo yamebadilika sana. Ukitokea kumpenda mtu fulani kama kweli nia yako ni kuingia naye kwenye ndoa na siyo kukidhi matamanio ya siku moja, zipo mbinu nyingi zinazoweza kukurahishia kazi yako. Kuna simu za mikononi, kuna mitandao ya kijamii na njia chungu nzima hivyo huna haja ya kuendelea kuumia na upweke.


Kumbuka kuwa penzi bora ni lile ambalo wawili huanza kwa kuwa marafiki, ni makosa kukurupuka kumtongoza mtu kwenye simu au kwenye mitandao ya kijamii bila kumvuta kwanza karibu yako na kumfanya kuwa rafiki yako.

Hatua ya kwanza, kama nilivyosema hapo juu ni kujitahidi kujenga ukaribu naye. Kama unadhani ni vigumu kwa wewe na yeye kukutana ana kwa ana, unaweza kutafuta namba yake ya simu. Ukishapata namba ya simu ya huyo umpendaye, tafuta muda ambao utakuwa umetulia kisha mpigie na jitambulishe.
Mweleze kwamba umempigia simu kumjulia hali, kama akikuuliza mahali ulikoipata namba yake, unaweza kumjibu vyovyote lakini inashauriwa kuwa siyo vizuri kumtajia aliyekupa namba yake kwa sababu unaweza kuwagombanisha.
Usiwe na papara, mtakie siku njema na endelea na shughuli zako nyingine. Unaweza pia kuendelea kumtumia meseji za kawaida (siyo za mapenzi), ukimjulia hali, ukimuuliza kama ameshakula au amekula chakula gani, anafanya nini kwa muda huo na vitu anavyovipenda sambamba na vile asivyovipenda.

Endelea hivyo kwa muda, siri kubwa ambayo huijui ni kwamba watu wengi, hasa wanawake huwa wanapenda kujua kuwa mtu fulani anamjali kwa kumuuliza mambo mbalimbali yanayohusu maisha yake ya kawaida. Jitahidi kuwa mcheshi lakini usizidishe masihara. Ukishafanikiwa kumvuta karibu yako na kumfanya aamini kwamba huwa unamfikiria mara kwa mara, sasa unaweza kupiga hatua moja mbele kwa kufanya yafuatayo:

Tumia sauti ya utulivu yenye hisia ndani yake, utazidi kumvuta karibu yako. Usipende kuzungumza kwa sauti ya juu au kupayuka au kupiga simu ukiwa kwenye kelele. Akipokea tu simu yako, mjulie hali yake kisha msifie kidogo kuhusu sauti yake na namna anavyozungumza.
Msimulie kidogo kuhusu siku yako inavyokwenda, tumia maneno machache lakini yatakayomfanya asiboreke kukusikiliza. Ifanye stori yako iwe ya kuvutia kwa kutumia maneno matamu yatakayomfurahisha na kumfanya aache kila anachokifanya na kukusikiliza.

Badili mazungumzo, muulize kama anajua kwamba yeye ni mzuri sana na hujawahi kukutana na mtu anayevutia kama yeye. Kama wewe ni mwanaume na unayezungumza naye ni mwanamke, utakuwa katika nafasi nzuri ya ‘kum-win’ kwa sababu wanawake wengi wanapenda sana kusifiwa.

Akiwa amekolea na sifa unazommwagia, mweleze kwamba unavutiwa naye na unatamani kuwa na mpenzi anayefanana naye. Zungumza naye kwamba atakapokubali kuwa na wewe, utamtunza na kumlea kama malkia, mweleze malengo yako ya baadaye katika uhusiano wenu endapo atakukubalia.

Usimpe nafasi ya kukwambia kama amekubali au amekataa bali hitimisha mazungumzo yenu kwa kumtakia siku njema au kazi njema. Bila shaka utamuacha akiwa na shauku kubwa ya kuendelea kusikiliza ‘mistari’ yako.
Endelea kuwasiliana naye kwa mambo ya kawaida huku ukimpima kama yale uliyomwambia anayachukuliaje. Kama naye amekupenda, utaanza kuona mabadiliko kuanzia meseji atakazokuwa anakutumia.

Itaendelea wiki ijayo.

GPL

No comments: