ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 28, 2015

UNESCO YATAKA UBIA NA MWEDO

DSC_0005
Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya Maendeleo ya wanawake wa Kimasai (MWEDO), Ndinini Kimesera (kushoto) akimkaribisha Mkurugenzi Mkazi wa Unesco nchini, Zulmira Rodrigues kwenye ofisi za asasi hiyo kwa ajili ya mazungumzo jijini Arusha.

Na Mwandishi Wetu, Arusha
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, limesema kwamba litaingia ubia na asasi ya Maendeleo ya wanawake wa Kimasai (MWEDO) ili kuimarisha mradi wa kijiji cha digitali cha Ololosokwan.
Mradi huo mkubwa unaoendeshwa na Unesco kwa kushirikiana na Samsung umelenga kuinua maisha ya jamii ya wafugaji wa kimasai kwa kuwawezesha kielimu, kitamaduni na kiujasirimali.
Kauli ya kutaka kuingia ubia imetolewa na Mkurugenzi Mkazi wa Unesco nchini, Zulmira Rodrigues wakati alipokutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwedo, Ndinini Kimesera katika ofisi za Mwedo mkoani Arusha.
Alisema Unesco inataka kutumia uzoefu wa Mwedo katika ushirikishaji wananchi hasa katika uwezeshaji ujasirimali na elimu kufanikisha moja ya miradi mikubwa ya kisayansi katika kijiji cha Ololosokwan.
DSC_0031
Mkurugenzi Mkazi wa Unesco nchini, Zulmira Rodrigues (kushoto) akiwa kwenye mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya Maendeleo ya wanawake wa Kimasai (MWEDO), Ndinini Kimesera (katikati) alipotembelea ofisi hizo jijini Arusha. Kulia ni Mshauri wa kiufundi, usimamizi na tathmini wa MWEDO, Bw. Paul Wilson.

Alisema Rodrigues katika mazungumzo na Mtendaji wa Mwedo kwamba Unesco imetambua haja ya kushirikisha wabia wengi katika maendeleo ili kufanikisha mradi huo mkubwa unaotaka kutoa huduma za afya, elimu na kuleta mabadiliko chanya katika jamii ya wafugaji wa kimasai ili kuweza kutumia raslimali zao walizonazo kupata maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Alisema vifaa kwa ajili ya mradi wa kubadili kijiji cha Ololosokwan kuwa kijiji cha digitali vimeshafika katika bandari ya Dar es salaam na wakati wowote kuanzia wiki zijazo vitasafirishwa kuelekea kijiji hicho tayari kwa utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa aina yake nchini ambao umelenga moja kwa moja wahusika.
Alisema mradi huo unataka kutumia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano kuwawezesha wananchi wa kijiji hicho kupata mabdiliko makubwa ya kimaisha.
DSC_0019
Mkurugenzi Mkazi wa Unesco nchini, Zulmira Rodrigues akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya Maendeleo ya wanawake wa Kimasai (MWEDO), Ndinini Kimesera.

“Tumefika kwenu kuona ni namna gani tutasaidiana kuimarisha mradi huu hasa utoaji wa elimu na ujasirimali na utafutaji masoko” alisema.
Alisema mradi huo umetaka kuhakikisha watoto wa wafugaji waume kwa wake wanapata elimu kwa kupitia teknolojia ya kisasa, huku ujasirimali kama utengenezaji wa shanga ukiwa katika soko na kuboreshwa zaidi.
Alisema kwa watu wazima wanataka kuwapa uelewa ili kuboresha maisha yao kiujasiriamali, kiafya na kiuchumi.
Alisema soko la bidhaa za wanakijiji wa Ololosokwan kama urembo wa shanga na mashuka zinazouzwa kwa watalii, zinaweza kupata soko zaidi kwa kuboreshwa.

DSC_0051
Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) Bw. Al Amin Yusuph (kulia) akifafanua jambo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya Maendeleo ya wanawake wa Kimasai (MWEDO), Ndinini Kimesera (hayupo pichani). Kulia ni Mshauri wa kiufundi, usimamizi na tathmini wa MWEDO, Bw. Paul Wilson.

Alisema ameridhika na uhodari uliooneshwa na Mwedo katika ujasiriamali na hivyo wanataka kuimarisha uhusiano huo kwa kuhakikisha inawaleta watu wa kusaidia kuboresha elimu ya utengenezaji wa vifaa hivyo kwa soko la mataifa.
Alisema kwamba pamoja na kuwataka Mwedo kutafuta hosteli kwa ajili ya wabunifu hao ili kuziongeza thamani bidhaa kwa soko la kimataifa.
Naye Mtendaji wa Mwedo amesema kwamba wapo tayari kushirikiana na Unesco katika miradi ya wananchi wa jamii ya wafugaji.
DSC_0057
Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya Maendeleo ya wanawake wa Kimasai (MWEDO), Ndinini Kimesera akielezea shughuli mbalimbali zilizofanywa na asasi yake ikiwemo ujenzi wa shule ya sekondari MWEDO ikiwashirikisha wasichana wa kimasai wanaoishi katika mazingira magumu wakiwa ni wanafunzi waliokosa nafasi ya kupata elimu kwa kuwachukua wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali kwenye jamii ya kifugaji, masuala ya ujasiriamali kwa wanawake wa kimasai pamoja na mambo mengine mengi yanayoendelea kufanywa na asasi hiyo kwa Mkurugenzi Mkazi wa Unesco nchini, Zulmira Rodrigues (kushoto). Kulia ni Mshauri wa kiufundi, usimamizi na tathmini wa MWEDO, Bw. Paul Wilson.
DSC_0044
Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO aliambatana na Afisa mipango ya Elimu wa Shirika la UNESCO, Bi. Jennifer Kotta (kulia) pamoja na Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph (kushoto). Katikati ni Afisa Mradi wa MWEDO, Martha Sengeruan.
DSC_0079
Mkurugenzi Mkazi wa Unesco nchini, Zulmira Rodrigues akiangalia bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na wakinamama wa kimasai kwenye duka la MWEDO mara baada ya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya Maendeleo ya wanawake wa Kimasai (MWEDO), Ndinini Kimesera (kulia). Katikati ni Afisa mipango ya Elimu wa Shirika la UNESCO, Bi. Jennifer Kotta.
DSC_0094
Mkurugenzi Mkazi wa Unesco nchini, Zulmira Rodrigues (kulia) akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya Maendeleo ya wanawake wa Kimasai (MWEDO), Ndinini Kimesera mara baada ya mazungumzo.

No comments: