ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 20, 2015

WANAWAKE WASOMI WA SAYANSI WANAISHI KWA RAHA NA HAWAZEEKI

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (Must), Scholastica Loppa anasema asilimia kubwa ya wanawake au wasichana wanaosoma sayansi ni wazuri na hawazeeki.

Akiwa ndani ya mavazi ya kawaida, mweupe kwa rangi ya mwili huku kichwa chake kikiwa kimesheheni nywele nyeusi za asili zisizo na hata chembe ya kemikali, Loppa alikuwa na mengi ya kuwaeleza watu.
Masomo ya sayansi hayazeeshi si mnaniona mimi hapa? Napendeza, sipendezi? alihoji mhadhiri huyo mbele ya umati uliofika kwenye chuo hicho kushuhudia uzinduzi wa kampeni za kuhamasisha wasichana wasome masomo ya uhandisi na teknolojia (Wited).

Kampeni hiyo inaratibiwa na chuo hicho kupitia mpango maalumu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola Afrika wa kuhimiza wasichana wasome sayansi na ufundi.

Mhadhiri huyo aliwasihi wasichana wa sekondari na vyuo mbalimbali nchini kutosikiliza madai kuwa wanawake wanaosoma sayansi wanazeeka mapema, kwa sababu masomo hayo yanahusisha kufikiri kwa kiwango kikubwa.

Aungwa mkono

Kauli imepokelewa kwa mikono miwili na baadhi ya watu, akiwamo mkurugenzi msaidizi wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia, Margreth Komba anayesisitiza kwamba wanawake waliosoma sayansi wanaishi maisha ya raha zaidi kuliko wanaosoma fani nyingine.

Anaeleza kuwa masomo ya sayansi kwa wanawake yanawaongezea maarifa zaidi, kwani wao wamezaliwa kisayansi zaidi na ndio maana wanafanya kazi nyingi zikiwamo za kutumia moto jikoni.

Naye Mwenyekiti wa mpango huo chuoni hapo na mhadhiri wa sayansi na biashara, Albertina Leonard, anasema wanawake ni kila kitu katika maisha duniani.

Anasema uzinduzi wa mpango wa Wited ni ukurasa mpya kwa chuo hicho kuanzisha kampeni maalumu kuwahamaisha wanawake walio kazini na hata wanafunzi wa sekondari kujipanga kupenda masomo ya uhandisi na teknolojia.

No comments: