Advertisements

Saturday, January 24, 2015

YANGA SC YAFANYA KWELI MOROGORO

Na Bertha Lumala, Morogoro
Bao pekee la mshambuliaji Danny Mrwanda limeizindua Yanga SC na kuipa ushindi wa tano msimu huu katika mechi pekee ya leo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Polisi Moro iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.

Mrwanda alifunga bao hilo dakika ya 42 akimalizia mpira uliotemwa na kipa Tony Kavishe wa Polisi Moro kufuatia shuti kali la krosi ya beki wa pembeni kulia Juma Abdul.
Hilo ni bao la tano kwa Mrwanda baada ya kufunga pia mabao manne katika mechi saba alizokichezea kikosi cha Kocha Adolf Richard cha Polisi Moro mwanzoni mwa msimu huu kabla ya kujiunga na Yanga SC dirisha dogo.

Mrwanda, ambaye hakufunga katika mechi mbili zilizopita ambazpo Yanga SC ilitoka sare ya 2-2 dhidi ya Azam FC na 0-0 dhidi ya Ruvu Shooting, sasa yuko sawa na Ame Ally Amour wa Mtibwa Sugar FC na Rashid Mandawa wa Kagera Sugar wenye mabao matano pia.

Kwa ushindi huo, Yanga SC ambayo imeshinda mechi nyingine nne msimu huu dhidi ya Tanzania Prisons, JKT Ruvu, Stand United na Mgambo ikishikwa kwa sare na Simba SC, Azam FC na Ruvu Shooting Stars na kufungwa na wakatamiwa Mtibwa Sugar FC na Kagera Sugar FC, imefikisha pointi 18 baada ya kucheza mechi 10.

Kikosi hicho cha Pluijm sasa kiko kimepanda hadi nafasi ya pili ya msimamo wa VPL kikizidiwa pointi mbili na vinara Azam FC ambao pia wamecheza mechi 10 na kesho watakipiga dhidi ya Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Shambulizi kali zaidi la Yanga SC kipindi cha kwanza lilifanyika dakika nne kabla ya kufungwa kwa bao la Mrwanda, shuti la mshambuliaji Mliberia Kpah Sherman wa Yanga SC lilipogonga besela na mpira kutua kwenye guu la kulia la kiungo Salum Telela lakini akapaisha.

Yanga SC waliuanza kwa kasi mchezo huo wakilisakama muda wote lango la Polisi Moro kipindi cha kwanza kabla ya hali kugeuka kipindi cha pili baada ya kuingia kwa mfungaji bora wa Kombe la Kagame 2012, Said Bahanunzi kipindi cha pili.

Bahanunzi aliyejiunga na Yanga SC katikati ya mwaka 2012 akitokea Mtibwa Sugar SC, akaisaidia Yanga kutwaa taji la Kombe la Kagame wakiwafunga 2-0 wanafainali Azam FC huku akitwaa kiatu cha mfungaji bora. Aliifungia Yanga SC kwa penalti katika sare ya 1-1 dhidi ya Simba msimu wa 2012/13 kisha akafulia kabla ya kujiunga na Polisi Moro dirisha dogo msimu huu.

Kuingia kwake kipindi cha pili katika mechi ya leo kumeonekana kuipa uhai safu ya ushambuliaji ya Polisi huku Kocha Mkuu wa Yanga SC, Mholanzi Hans van Der Pluijm akimtoa beki wa kati Kelvin Yondani na kumuingiza Rajab Zahir baada ya kuingia kwa Bahanunzi.

Muda mwingi kipindi cha kwanza kabla ya kufungwa kwa bao, wachezaji wa Polisi Moro walikuwa wakianguka na kupoteza muda, hali ambayo pia iliigwa na wachezaji wa Yanga SC kipindi cha pili. Kipa Ali Mustafa ‘Barthez’, Mrwanda na winga Mbrazil Andrey Coutinho walitumia mbinu hiyo ya kuanguka na kugangwa uwanjani ili kupoteza muda.

Coutinho, aliyeletwa nchini na kocha wa zamani wa Taifa Stars na Yanga SC, Mbrazil Marcio Maximo, alionywa kwa kadi ya njano kwa kupoteza muda wakati akitolewa kumpisha Hussein Javu dakika 10 kabla ya mechi kumalizika.

Hadi kipyenga cha mwisho cha refa John Kanyenye kinapulizwa, Polisi Morogoro 0-1 Yanga SC.

Kulikuwa na idadi ndogo ya watazamaji waliojitokeza uwanjani kushuhudia mechi hiyo ikilinganisha na mechi zilizopita za Yanga SC kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa: Ali Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani/ Rajab Zahir (dk 58), Salum Telela, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/ Hassan Dilunga (dk 71), Danny Mrwanda, Kpah Sherman Andrey Coutinho/ Hussein Javu (dk 80).

Kikosi cha Polisi Moro FC: Tony Kavishe, Mohamed Mpopo, Simon Fanuel, Chacha Marwa, Laban Kambole, Nahoda Bakari, Said Mkwagu, Iman Mapunda, Six Mwasekaga/ Said Bahanunzi (dk 47), Kassim Selembe.
Credit:ShafiihDauda

No comments: