ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 19, 2015

KUNA UBAYA GANI VALENTINE’S DAY KUWA KILA WIKI?

Niwiki nyingine tulivu tunakutana kupitia ukurasa huu nikiamini kwamba umzima na unaendelea nyema na majukumu yako ya kila siku. Mimi mzima wa afya na namshukuru Mungu kwa kila jambo ambalo amekuwa akinitendea katika kila siku ya maisha yangu.

Naomba tu niseme kwamba, kupitia safu hii unaweza kupata ushauri wa mambo mbalimbali ya kimapenzi hivyo kama una lolote ambalo linakukosesha amani, usikae nao! Wasiliana nami kwa namba za simu hapo juu naamini suluhisho litapatikana.

Mpenzi msomaji wangu. Wiki iliyopita tuliona nguo za rangi nyekundu na nyeusi zikipamba ulimwengu katika kusherehekea Sikukuu ya Wapendanao ‘Valentine’s Day’.Najua ilikuwa ni siku ya furaha kwa walio wengi hasa walio katika mapenzi ya kweli lakini usishangae kusikia wapo walioachana, waliogombana na waliofumaniana katika siku hiyo muhimu. Hawa ni wale walio kwenye mapenzi ya ubabaishaji ambayo mimi na wewe hatupaswi kuyapa nafasi.

Hata hivyo, yapo mambo ya kujifunza katika siku hii. Kusema ukweli nawashangaa sana wale ambao ikishafikia siku hii ndiyo wanahaha kutafuta zawadi na kadi kwa ajili ya wapenzi wao.Yaani wao kuonesha namna wanavyowapenda wapenzi wao ni mpaka siku hiyo ifike, kabla ya hapo mambo yanaenda kawaida tu. Hii siyo sawa kabisa.

Hivi ni kweli kuoneshana namna mnavyopendana ni mpaka siku hiyo ifike? Kama tuna dhana hiyo tutakuwa na ulimbukeni wa hali ya juu. Haya mambo yanatakiwa kila siku. Kununuliana kadi, kununuliana zawadi kunatakiwa kila kukicha ukiwa na uwezo wa kufanya hivyo, kwa nini? Kwa sababu mapenzi ya sasa usanii umekuwa mwingi.

Kumfanya mpenzi wako aamini kwamba unampenda kwa dhati si kazi rahisi. Yaani unatakiwa kila siku umwambie I Love You! Siku ikipita hujafanya hivyo, usishangae akahisi umzugaji.Katika mizunguko yako ukibahatika kupata kitu hata kama ni kidogo, mnununlie mpenzi wako kama zawaidi. Ukifanya hivyo utakuwa unapalilia penzi lenu kila siku.

Sasa cha kujiuliza ni kwamba, kwa nini hatufanyi hivyo? Ni kweli hatuna uwezo wa kufanya hivyo mpaka tufanye maandalizi kwa mwaka mzima kisha tuje tuwaoneshe upendo wale tunaowapenda Siku ya Wapendanao?

Mimi naamini uwezo wa kufanya hivyo tunao ila huwa tunajisahau na kuyaacha mambo yaende tu, kitu ambacho madhara yake ni makubwa hapo baadaye.

Ndiyo maana huwa najiuliza, kwani kuna ubaya gani endapo tutaamua kuwa kila siku ya wikiendi iwe Valentine’s Day? Kwamba kila ikifika Jumamosi, watu wanapendeza na nguo zao nyekundu kisha wanakwenda maeneo flani na wapenzi wao kula raha, wananunuliana zawadi, wanapeana kadi na maisha yanaendelea, kuna ubaya gani?

Sidhani kama kuna ubaya na kama unaona fedha za kusherehekea kila wikiendi huna, basi jenga tu utaratibu wa kumuonesha mpenzi wako kwamba unampenda kila siku na wala usisubiri hizo siku muhimu.

Ninachotaka kusema katika makala haya ya leo ni kwamba, mapenzi ya kuoneshwa siku ya Valentine’s hayawezi kuwa ya dhati, ya dhati ni yale ambayo kila siku yanapatikana.
Ukisubiri kwamba eti siku ya valentine ndiyo umnunulie mpenzi wako zawadi au umpe kadi, wewe utakuwa ni mshamba na utakuwa unaogelea kwenye penzi legelege ambalo wakati wowote linaweza kuvunjika.

GPL

No comments: