Advertisements

Friday, February 27, 2015

MAMA SALMA KIKWETE AKABIDHI MASHINE YA KUPIMIA SARATANI YA MATITI KWA AKINA MAMA HOSPITALI KUU YA JESHI LUGALO

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akimshauri Ndugu Peter Charles,28, baba mzazi wa binti Irene mwenye umri wa miezi 3 na mkazi wa Mikocheni kupunguza baadhi ya nguo alizomfunika mtoto wakati hali ya hewa ni ya joto. Mama Salma alimpongeza Ndugu Peter kwa kuambatana na mke wake kwenda kliniki.Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akisalimiana na Bibi Mariam Omar aliyemshika mtoto wake Jane Winston aliyekuwa akisubirim kupata huduma hospitalini hapo wakati Mama Salma alipotembelea sehemu mbalimbali za Kitengo cha Uzazi na Mtoto mara baada ya kukabidhi mashine ya kupimia saratani ya matiti kwa akina mama tarehe 27.2.2015.
Mke wa Rais na Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete akikabidhi mashine ya kupimia saratani ya matiti kwa akina mama kwa uongozi kwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Luteni Jenerali Samuel Ndomba (kulia). Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika kwenye Hospitani Kuu ya Jeshi Lugalo kwenye Kitengo cha Uzazi na Mtoto kilichoko Mwenge tarehe 27.2.2015. Aliyesimama pembeni kwa Mama Salma ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Donan Mmbando na aliyesimama kulia kwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi ni Mkuu wa Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugal Brigedia Jenerali Josia Mwita Makere.Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Luteni Jenerali Samuel Ndomba akimpongeza Mama Salma Kikwete kwa hotuba yake aliyoitoa kwenye hafla ya kukabidhi mashine ya kupimia saratani ya matiti kwa akina mama kwenye hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo tarehe 27.2.2015.Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo,WAMA, Mama Salma Kikwete akitoa hotuba yake muda mfupi kabla ya kukabidhi mashine ya kupimia saratani ta matiti kwa akina mama kwenye Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo. Hafala hiyo ilifanyika kwenye Kitengo cha Uzazi na mtoto cha hospitali hiyo kilichoko eneo la Mwenge hapa Dar tarehe 27.2.2015.Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Luteni Jenerali Samuel Ndomba akitoa hotuba wakati wa hafla ya kukabidhi mashine ya kupima saratani ya matiti kwa akina mama katika Hospitali ya Lugalo tarehe 27.5.2015.Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo,WAMA, Mama Salma Kikwete akiangalia ngoma za utamaduni mara baada ya kuwasili kwenye sherehe za kukabidhi mashine ya kupimia saratani ya matiti (Mammograph) kwa akinamama katika Hospitali ya Jeshi Lugalo kwenye kitengo cha Uzazi na mtoto kilichopo eneo la Mwenge hapa Dar tarehe 27.2.2015. Aliyesimama kushoto kwa Mama Salma ni Luteni Jenerali Samuel Ndomba, Mnadhmu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.Baadhi ya viongozi wa Jeshi la Ulinzi na wananchi waalikwa wakisikiliza kwa makini hotuba ya mgeni Rasmi Mama Salma Kikwete wakati wa hafla ya kukabidhi mashine ya kupimia saratani ya matiti kwa akina mama.Baadhi ya viongozi wa Jeshi la Ulinzi na wananchi waalikwa wakisikiliza kwa makini hotuba ya mgeni Rasmi Mama Salma Kikwete wakati wa hafla ya kukabidhi mashine ya kupimia saratani ya matiti kwa akina mama.

………………………………………………………..

Na Anna Nkinda – Maelezo

27/2/2015 Wanaume nchini wametakiwa kuwaunga mkono wake zao kupima saratani za matiti na shingo ya kizazi na pale watakapokutwa na maradhi hayo wasiwanyanyapae bali wawafariji kwani magonjwa hayo yanatibika kama yatagundulika mapema.

Rai hiyo imetolewa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya mashine ya kisasa ya upimaji wa saratani ya matiti (Mammography) katika Hospitali kuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo, kliniki ya Mama na Mtoto iliyopo Mwenge jijini Dar es Salaam.

Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema unyanyapaa wa wanaume huwakwaza wanawake na kuwafanya baadhi yao kusita kujitokeza kupima na kupata tiba dhidi ya saratani.

“Nanyi wanawake msisubiri mpaka msikie maumivu ndipo mkapime maana wakati huo saratani itakuwa imeenea, jengeni tabia ya kupima saratani za matiti na shingo ya kizazi mara kwa mara wataalamu wanasema unapima mara moja kila baada ya miaka mitatu”.

Bahati nzuri saratani ya shingo ya kizazi ina kinga kwa njia ya chanjo hivyo basi wazazi tuchangamkie kuwapeleka watoto wetu wa kike kupata chanjo hiyo, tutawapatia kinga ya kudumu ya maradhi haya hatari”, alisisitiza Mama Kikwete.

Alisema ugonjwa wa saratani ya matiti unaathiri wanawake wengi nchini na wataalam wa afya wanasema saratani ya matiti ni ya pili kwa ukubwa nchini ikifuatiwa na ya shingo ya kizazi.

Mama Kikwete alisema, “Niliamua kukabidhi mashine hii katika Hospitali hii baada ya kubaini kuwa wananchi wengi wanatibiwa hapa pia huduma ya mama na mtoto hutolewa hapa.Hospitali kuu ya Jeshi ya Lugalo ni Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mashariki hivyo inastahili kuwa na mashine ya aina hii ambayo itawanufaisha wanawake wengi wanaokuja hapa kuhudumiwa”.

Kwa upande wa saratani ya tezi dume aliwahimiza wanaume wenye umri wa zaidi ya miaka 45 wajitokeze kupima kwani ikigundulika mapema inatibika.

Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema, “Wanawake nasi tunao wajibu wa kuwahamasisha waume zetu kupima saratani ya tezi dume na kuwafariji wakiwa wakiwa kwenye tiba. Tushirikiane kwa pamoja kuleta mabadiliko”.

Naye Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Samuel Ndomba alimpongeza Mama Kikwete kwa kazi anayoifanya ya kuiongoza Taasisi ya WAMA yenye lengo la kuinua ustawi wa watoto na akina mama hususani katika nyanja za afya, elimu na huduma za maji safi na salama.

Alisema, “Juhudi kubwa unazozionyesha za kuboresha na kuendeleza huduma za afya ya mama na mtoto zinadhihirisha upendo wa dhati ulionao kwa umma wa watanzania”.

Luteni Jenerali Ndomba alisema tukio hilo la kukabidhiwa mashine ya kupimia saratani ya matiti kwa Jeshi hilo ni la kihistoria na la kipekee na kumshukuru Mama Kikwete kwa kutambua umuhimu, kujali na kuthamini afya za wanajeshi, familia zao na akina mama wote.

“Ni dhahiri kuwa ulinzi imara wa taifa letu unategemea wanajeshi na wananchi wenye afya nzuri. Tunakuhakikishia kuwa mashine hii haitatumika kwa wanajeshi na familia zao tu bali itatumika kutoa huduma kwa wananchi wa Tanzania kwa kufuata kanuni na taratibu za huduma ya tiba Jeshini”, alisema Luteni Jenerali Ndomba .

Alimalizia kwa kusema Jeshi hilo litaweka kipaumbele katika mafunzo kwa wataalam ambao wataweza kuitumia na kuitunza vizuri mashine hiyo ili utoaji wa huduma kwa akina mama uwe endelevu.

Mashine hiyo imetolewa na kikundi cha wanawake wajasiriamali wa Tanzania waishio nchini Washington, nchini Marekani cha Wanawake watano (Tano Ladies) kwa kushirikiana na Chama cha Wanawake wa Afrika na Uelewa wa Saratani (African Women Cancer Awareness Assossiation – AWCAA).

Wanawake hao walimkabidhi Mama Kikwete mashine hiyo ya kupimia saratani ya matiti mwishoni mwa mwaka jana alipokuwa nchini Marekani katika shughuli za kikazi ili iweze kusaidia na kuokoa maisha ya wanawake hapa nchini.
cedit:Full Shangwe.

No comments: