
Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP, Thobias Sedoyeka akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake.
Na Nathaniel Limu, Singida
MTOTO wa kike mwenye umri wa miaka sita mkazi wa kitongoji cha Maweni kijiji cha Mayaha kata ya Minyughe tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida,Samaka Matawa,amefariki dunia baada ya kubakwa na kisha kunyongwa shingo.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP,Thobias Sedoyeka, alisema tukio hilo la kusikitisha na la kinyama, limetokea majira ya jioni februari sita mwaka huu na mwili wa mtoto huyo uliokotwa na raia wema kesho yake saa 12 asubuhi ukiwa umetelekezwa hatua 150 na nyumbani kwao.
Alisema siku ya tukio, mtoto huyo Samaka alienda porini kwa lengo la kuchuma matunda pori.
“Mtoto huyo akiwa anaendelea na zoezi la kuchuma matunda pori akiwa peke yake, aliviziwa na Ramadhani Omari (28) na kukamatwa kwa nguvu na kisha alifanyiwa kitendo hicho bila huruma na mtuhumiwa Omari”,alifafanua.
Sedoyeka alisema mtuhumiwa Omari tayari ameishakamatwa na polisi na uchunguzi zaidi unaendelea na mara utakapokamilika, atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili.
Kamanda huyo alisema mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na daktari na wazazi na ndugu walikabidhiwa mwili huo kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Habari zaidi kutoka eno la tukio zinadai kuwa baada ya kuawa mtoto huyo,sehemu zake za siri zilinyofolewa.
No comments:
Post a Comment