Advertisements

Saturday, February 28, 2015

Mtoto wa Sokoine ataka Jimbo la Lowassa

Namelock Sokoine.

Monduli. Viongozi wa Mila ya kimasai, maarufu kama Laigwanani wa Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha wamesema wanamruhusu kuwania ubunge wa Jimbo la Monduli, mtoto wa kike wa Waziri Mkuu wa zamani, hayati Edward Moringe Sokoine, Namelock Sokoine.
Mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ametangaza nia ya kutogombea tena jimbo hilo, hali ambayo imeibua mvutano kwa makada kadhaa wa CCM wilayani Monduli. Namelock alikuwa mmoja wa watoto kipenzi cha hayati Sokoine,
Katibu wa viongozi hao wa kimasai, Buluka Ngaimeria na Makamu Mwenyekiti wake, Mepukori Mberekeri, kwa nyakati tofauti alisema wao kama viongozi wa mila, hawajatoa msimamo wa kumkataa Namelock kwa kuwa ni mwanamke.
Ngaimeria alisema, hivi karibuni walikutana katika Kata ya Makuyuni, lakini hakukupitishwa azimio la kumkataa Namelock kwa kuwa ni mwanamke.
“Mimi kama Katibu wa viongozi wenzangu, hatukufikia maamuzi ya kumkataa mtu, kile kikao kilikuwa cha kujadili mambo yetu ikiwepo kutokuwa na ofisi na masuala ya siasa haikuwa hoja kuu,” alisema.
Naye Makamu Mwenyekiti wa viongozi hao, Mepukori Mberekeri alisema, yeye ndiye alitoa taarifa kwenye kikao hicho, juu ya tangazo la Namelock kuwania ubunge alilotoa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Monduli.
“Baada ya kuwapa taarifa mjumbe mwingine alisema pia kuna mgombea mwingine, Loota Sanare na baada ya majadiliano suala hilo liliachwa lije kuamuliwa na wananchi,” alisema.
Alisema sio kweli kuwa wao, wametangaza kupinga kuongozwa na Mbunge mwanamke na sio kweli kuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Edward Lowassa anawashinikiza kumtaka Sokoine.
Uchaguzi wa ubunge katika jimbo la Monduli, umeibua gumzo kubwa hasa kutokana na uamuzi wa Lowassa kutajwa kuutaka urais.
MWANANCHI

No comments: