ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 16, 2015

MWANAMKE MZURI ANAPASWA KUWA NA VIGEZO GANI?- 2

U hali gani msomaji wangu? Ni matumaini kwamba uliifurahia siku ya wapendanao (Valentines Day) kwa kufanya yale yanayostahili kufanywa kwenye siku hiyo. Nakukaribisha tena tuendelee na mada yetu tuliyoianza wiki iliyopita kama inavyojieleza hapo juu.

Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitakushukuru wewe msomaji wangu ambaye ulituma ujumbe mfupi (sms), kuchangia mada hii kama nilivyokuomba. Ushauri au mawazo yako uliyoyatoa ni ya msingi sana.
Leo tunaendelea kujadili sifa au vigezo anavyopaswa kuwa navyo mwanamke ili aitwe mzuri. Katika wengi waliochangia, walijikita kueleza sifa anazopaswa kuwa nazo mwanamke huku wengine wakitoa ushuhuda wa jinsi kudanganyika kwao na sura au umbo, kulivyowasababishia maumivu makali kwenye mioyo yao.

MFANO HALISI
Mama Karim, mkazi wa Tabata jijini Dar ni msomaji mzuri wa kona hii. Katika kuchangia mawazo yake, alinitumia ujumbe ufuatao:

“Kaka ni kweli kabisa uzuri wa mwanamke siyo sura wala umbo. Mimi binafsi Mungu amenijaalia sura nzuri na umbo mashalaah, sijisifu lakini nimeumbika. Nilipokuwa msichana mbichi, nilitingisha sana kiukweli. Ilikuwa mwanaume hawezi kunisumbua kwa chochote, akileta za kuleta naachana naye kwani ni wengi waliokuwa wananipenda na kunihitaji. Nilidanganyika na uzuri wa sura na umbo bila kujua umri unaenda.

“Baada ya kuhangaika na wanaume wa kila aina, nilichoambulia ni kuzalishwa mtoto mmoja ambaye hana baba, sikupata bahati ya kuolewa na mpaka sasa nakaribia kufikisha miaka 35, nipo tu nahangaika na maisha, uzuri umeshaisha kwani umri nao unaenda. Najutia sana bahati nilizozichezea wakati wa usichana wangu. Uzuri siyo sura wala umbo jamani.”

JAMBO LA KUJIFUNZA
Hili liwe somo kwa wanawake wote na wanaume pia kwamba uzuri wa mwanamke siyo sura wala umbo bali ni zaidi ya hapo. Kwa mfano wa hapo juu, utakuwa umeelewa vizuri alichokieleza mama Karim. Huyu ni miongoni mwa wanawake wengi ambao kwa kutojua thamani yao, wamejikuta wakiishi maisha ya taabu licha ya kujaliwa uzuri wa sura na umbo.

Kama ni mwanamke na upo ndani ya ndoa au unatarajia kuingia ndani ya ndoa, fahamu kwamba uzuri wako siyo sura wala umbo lako. Ukishalijua hili, utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kudumu kwenye ndoa kwa sababu wanaume wengi hawapendi wanawake ‘pasua kichwa’.

Na wewe kama ni mwanaume na unatarajia kuingia kwenye ndoa, kamwe usidanganyike na sifa za nje za mwanamke. Anaweza kuwa mzuri sana kwa kumtazama lakini utakapoingia naye kwenye ndoa akageuka na kuwa mwiba mkali kwenye mtima wako.

Sikatai kwamba wapo ambao wamejaliwa sura nzuri, umbo zuri na tabia njema pia ingawa wapo wachache sana lakini wengi akishakuwa na sura au umbo zuri, anajiona yupo tofauti na watu wengine na matokeo yake anaendekeza kiburi, jeuri na tabia zisizofaa katika jamii kwa sababu anajua ukimuacha wewe, wapo wengi wanaomsubiri na hatakosa tena mtu wa kumuoa.

Matokeo yake, wanashindwa kufahamu thamani ya mwanamke ni ipi na wengi wao wanaishia kuchezewa na kuhangaika na dunia. Jiongeze.

THAMANI HALISI YA MWANAMKE
Upo msemo ambao unatumika tangu enzi za mababu zetu kwamba uzuri wa mwanamke siyo sura bali ni tabia. Mwanamke anapaswa kuwa na tabia nzuri, aielewe thamani yake, ajue namna ya kuishi na mumewe, ajue kutunza familia, kuishi na ndugu, majirani na watu wanaomzunguka.

Amheshimu mumewe na kumpenda hata katika wakati mgumu, asiwe mwepesi wa kushawishika na vitu vidogo kama pesa, magari au nyumba kwani hivyo vyote ni vitu vya kupita. Awe na kauli nzuri, ajue namna ya kuzungumza na mumewe hata katika wakati ambao hayupo sawa, awaheshimu watu wote, bila kujali mkubwa au mdogo, tajiri au maskini.

Mwanamke mwenye sifa hizi, hata awe na sura mbaya kiasi ataolewa na kuwdumu kwenye ndoa yake.

GPL

No comments: