Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imesema imemhoji na inaendelea kumchunguza mmiliki mwenza wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL), James Rugemalira.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alisema vigogo wote waliohusika na sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow, ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wanachunguzwa akiwamo Rugemalira.
“Tunawachunguza wote, hatuwezi kufanya kazi harakaharaka kama zimamoto, tunakwenda hatua kwa hatua, uchunguzi ukikamilika wote watakaopatikana na hatia watapelekwa mahakamani,” alisema Dk Hoseah.
Rugemalira akiwa mbia wa IPTL chini ya Kampuni ya VIP Engineering and Management (VIPEM), ndiye kiini cha vigogo wengi wa Serikali kupewa mgawo wa fedha kupitia Benki ya Mkombozi.
Akizungumzia suala hilo, Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwani alisema Rugemalira anachunguzwa na kueleza kuwa taratibu zote za uchunguzi ikiwamo mahojiano zimeshaanza kufanyika... “Tumeshamuhoji na tunaendelea kumchunguza, hilo linaeleweka.”
Walioburuzwa kortini na Takukuru
Mpaka sasa Takukuru imeshapeleka watuhumiwa kadhaa mahakamani wakiwamo maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Miongoni mwao ni Meneja Misamaha ya Kodi TRA, Kyabukoba Leonard Mutabingwa, Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco, Steven Roman Urassa na Mkurugenzi wa Fedha BoT, Julius Rutta Angello ambao wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya kuomba na kupokea rushwa ya mamilioni ya fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Wengine waliofikishwa mahakamani hapo ni Mhandisi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Theophillo Bwakea anayedaiwa kupokea Sh161,700,00. Mwingine ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma ambaye anadaiwa kuwekewa kiasi cha Sh323 milioni.
Waliosombwa na escrow bungeni
Viongozi wengine Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja aliyekuwa akiongoza Kamati ya Sheria na Utawala na Mbunge wa Chunya (CCM), Victor Mwambalaswa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini walijiuzulu nafasi zao hizo kutokana na kashfa hiyo.
Chenge anadaiwa kupokea Sh 1.6 bilioni na Ngeleja Sh40 milioni na Mwambalaswa alikuwa katika Bodi ya Tanesco ambayo Bunge liliazimia ivunjwe.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, aliwajibishwa na Rais Jakaya Kikwete Desemba mwaka jana katika mkutano wake na wazee wa Dar es Salaam. Profesa Tibaijuka anadaiwa kupokea mgawo wa Sh1.6 bilioni.
Awali, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alijiuzulu wadhifa wake baada ya Bunge kushinikiza awajibishwe kwa mujibu wa sheria kwa kuipotosha Serikali kuhusu suala hilo.
Mbali na viongozi hao, Serikali pia imemsimamisha kazi Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Eliakim Maswi kupisha uchunguzi dhidi yake katika kashfa hiyo.
Januari, 23, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospter Muhongo alijiuzulu wadhifa wake huku akisisitiza kuwa ni msafi na hawezi kuuza utu wake kwa kupokea rushwa ili kuwakandamiza Watanzania.
Kuhusu kufilisiwa mali wale waliohusika katika sakata hilo, Dk Hosea alisema hiyo ni kazi ya Mahakama kwani Takukuru kazi yake ni kuchunguza na kuwafikisha watuhumiwa sehemu husika.
Wanaodaiwa kupata mgawo wa escrow
Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali iliyowasilishwa bungeni ilitoa orodha ya watu waliopokea mgawo wa fedha za akaunti hiyo kuwa ni pamoja na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh40.4 milioni), aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk Enos Bukuku (Sh161.7 milioni).
Wengine ni Majaji wa Mahakama Kuu, Profesa Eudes Ruhangisa (Sh404.25 milioni) na Jaji Aloysius K. Mujulizi (Sh40.4 milioni) pamoja na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko (Sh40.4 milioni).
Pia, wamo aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Emmanuel Ole Naiko (Sh40.4 milioni), Ofisa wa TRA, Lucy Appollo (Sh80.8 milioni), Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini (Sh80.9 milioni), Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius Nzigirwa (Sh40.4 milioni) na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh40.4 milioni).
Ripoti ya PAC kuhusu kashfa ya Tegeta Escrow inatokana na uchunguzi maalumu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu fedha hizo zilizochotwa ndani ya BoT, zilipokuwa zinatunzwa zikiwa gharama za uwekezaji (capacity charge) kwa IPTL baada ya kutokea mgogoro wa kibiashara baina yake na Tanesco.
Tanesco ililalamika kuwa ilikuwa inailipa zaidi IPTL kinyume na gharama za uwekezaji, hivyo kuamuliwa na Mahakama kuwa fedha ilizokuwa inatakiwa kulipa ziwekwe katika escrow hadi upatikane ufumbuzi wa mgogoro huo.
Hata hivyo, kesi hiyo ilipohukumiwa Februari 12 mwaka jana, ikibainisha kweli Tanesco ilikuwa inailipa zaidi IPTL, tayari fedha zilizokuwa katika akaunti hiyo zilishachotwa na IPTL kwa ruksa ya baadhi ya viongozi wa Serikali.
MWANANCHI
1 comment:
Mheshimiwa Hosia, kama kazi yako ni kuchunguza wenye HATIA kabla ya kuwapeleka mahakamani, then kazi ya mahakama ni nini? Labda nikukumbushe tu kwamba kazi ya chombo unachokiongoza ni kuchunguza kama mtuhiwa ANA KESI YA KUJIBU and then MAHAKAMA ndiyo itakayoamua kama huyo mtuhumiwa ana HATIA au LA.
Post a Comment