ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 13, 2015

SERIKALI NA WADAU BINAFSI WASHAURIWA KUWASAIDIA WAJASIRIAMALI WA KITANZANIA

Balozi wa Tanzania nchini Oman Ali Ahmed Saleh kushoto Aliyekaa kwenye kiti akipata burudani ya Msewe iliyoandaliwa kwa ajili yake na Kikundi cha Sanaa cha Zanzibar mara baada ya Balozi huyo kumaliza ziara yake ya kuwatembelea Watanzania na kushauriana nao mambo mbalimbali ya kukuza soko katika Maonesho ya Kimataifa ya Sanaa Ubunifu na Utamaduni yanayoendelea Mjini Mascut nchini humo. Picha na Faki Mjaka.
Wasanii wa Kikundi cha Sanaa cha Zanzibar wakicheza Ngoma aina ya Uringe kwa Balozi wa Tanzania nchini Oman (hayupo pichani) mara baada ya Balozi huyo kuwatembelea Watanzania na kushauriana nao mambo mbalimbali ya kukuza soko katika Maonesho ya Kimataifa ya Sanaa Ubunifu na Utamaduni yanayoendelea Mjini Mascut nchini humo.
Mjasiriamali wa Mavazi mbalimbali ikiwemo ya Kimasai Bi Anna Matinde akitoa ufafanuzi wa bidhaa zake kwa Balozi wa Tanzania Nchini Oman Bw. Ali Ahmed Saleh kulia.Balozi Saleh alifanya ziara ya kuwatembelea Watanzania hao na kushauriana mambo mbalimbali ya kukuza soko katika Maonesho ya Kimataifa ya Sanaa Ubunifu na Utamaduni yanayoendelea Mjini Mascut nchini humo. Picha na Faki Mjaka-Mascut Oman.

Na Faki Mjaka, Muscat, Oman 

Serikali na Wadau binafsi wameshauriwa kuwasaidia Wajasiriamali wa Kitanzania ili waweze kuziweka bidhaa zao katika Vifungashio (Package) vyenye mvuto na kiwango cha ubora wa kimataifa.

Kufanya hivyo kutawawezesha Wajasiriamali hao kupata soko la Bidhaa zao kwa Wateja wadogo na wakubwa katika nchi mbalimbali duniani.

Ushauri huo umetolewa na Balozi wa Tanzania nchini Oman Bw. Ali Ahmed Saleh alipowatembelea Wajasiriamali wanaoshiriki katika Maeonesho ya Kimataifa ya Sanaa,Ubunifu na Utamaduni yanayoendelea katika Mji wa Muscat nchini Oman.

Amesema licha ya Tanzania kufanya vyema katika Maonesho hayo kuna baadhi ya changamoto ambazo zinahitaji kupatiwa ufumbuzi ili Tanzania izidi kupata sifa ya bidhaa zake kimataifa.

Changamoto hizo ni pamoja na uwezo mdogo wa kuziweka bidhaa wanazozitengeneza katika Vifungashio (Package) ambavyo ubora wake haujafikia kiwango kinachotakiwa cha kimataifa.

Balozi Saleh amefahamisha kuwa mbali na bidhaa hizo ikiwemo zile za Viungo kupata Soko kutoka kwa Wakaazi wa Oman lakini inakuwa ngumu kupata Soko kwa Wateja wa Maduka Makubwa (Supermarkets) ambao wangenunua bidhaa hizo kwa ujumla.

Ameongeza kuwa Wateja wa Maduka Makubwa wanahitaji bidhaa zilizowekwa katika Package ambazo zinaonesha kuwa zimepitia katika maabara ya kisayansi na kupata vigezo vyote vinavyohitajika kimatumizi.

“Naamini tukiwa na Package zenye ubora wa kimataifa zinazoonesha Warrant, muda wa matumizi basi hata Order za Wateja wa Supermarkets tungepata za kutosha ” Alisema Balozi Saleh

Aidha Balozi Saleh amewashauri Wajasiriamali hao kuziweka bidhaa zao katika Vifungashio (Package) hata zile ambazo bado hawajafikiria kuziweka ikiwemo zile za Vinyago na Viatu ili kuvutia zaidi Wateja.

“Tumezoea kwetu kuwa Vinyago haviwekwi kwenye Package ila navyo vinatakiwa viwekwe pamoja na vitu vingine ili wateja wahamasike na Ubora wa Bidhaa zetu” Alishauri Balozi Saleh

Hata hivyo Balozi Saleh ameishukuru Serikali ya Oman kwa mashirikiao yake makubwa na Tanzania na kwamba fursa hiyo iliyopatikana itakuwa na Matunda mazuri kwa Tanzania kutokana na kujitangaza vyema kwa Wageni na Wenyeji wa Oman.

Kwa upande wao Wajasiriamali hao Walimshukuru Balozi Saleh na Ofisi yake kwa kuwa karibu nao na kushauriana nao kila muda jambo ambalo linawapa faraja kubwa.

No comments: