ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, February 15, 2015

TBS yapiga ‘stop’ mabati ya Uni Metal

Dar es Salaam. Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limepiga marufuku usambazwaji wa mabati kutoka Kampuni ya Uni Metal East Africa Ltd baada ya kuthibitishwa kuwa hayajakidhi viwango.
Sambamba na kuzuiwa kuingia sokoni, TBS imelifungia ghala linalotumika kuhifadhi mabati hayo yanayoingizwa nchini kutoka India.
Ofisa viwango wa TBS, Cyrin Kimario alieleza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kupimwa kwa sampuli ya mabati hayo na kubainika kuwa hayajakidhi viwango licha ya kuwa na nyaraka zinazothibisha kukaguliwa na wakala aliyekuwa India.
“Pamoja na kukosa viwango vingine vya ubora haya mabati hayana chapa ya kiwanda yanapotengenezwa,” alisema Kimario.
Alisema kufuatia kasoro hizo bati hizo ambazo idadi yake zinafikia takriban 15,000 hazitaingizwa sokoni mpaka itakapopatikana taarifa kutoka India zilopokaguliwa kujua kwa nini ziliruhusiwa kuingia sokoni zikiwa chini ya kiwango.
Kimario alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania kuwa makini wakati wa kununua bidhaa ili kuhakikisha zina chapa inayoonyesha zimetengenezwa wapi.
“Bidhaa zikiwa zinaonyesha zimetengenezwa na nani ni rahisi hata sisi kuingilia kati na kumvaa mhusika endapo zitabainika kuwa chini ya kiwango,” alisisitiza Kimario.
Mkurugenzi wa Kiwanda hicho, Rohit Panjwan alieleza kushangazwa na taarifa hizo huku akisisitiza kuwa anazo nyaraka zote zinazothibitisha kuwa bati hizo zilikaguliwa.
“Nashangaa haya mambo yametokea wapi kwani tangu bati zimeanza kuingia sokoni ni mwaka sasa iweje leo ndiyo zionekane na upungufu,” alisema na kuongeza kuwa ametumia zaidi ya Sh5 bilioni kuagiza mzigo huu na kuahidi kumshtaki mkaguzi aliyenithibitishia bati hizo.
Mwananchi

No comments: