
Mkutano Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) ambao hukutanisha viongozi wa Klabu za Ligi Kuu ya Soka Bara na Ligi Daraja la Kwanza, uliofanyika Februari 28 mwaka huu, umejadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja kujulishwa taarifa za kupatikana kwa mdhamini wa Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao, ambaye ni Azam Media.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kaimu Mtendaji wa Bodi hiyo, Fatma Shibo, alisema kuwa katika mkutano huo pia wajumbe walijadili utendaji wa kazi za kila siku za bodi hiyo na mfumo wa tiketi za kieletroniki ambazo zinatumika.
Shibo alisema kuwa wajumbe wa bodi hiyo pia walizungumzia matukio ya vurugu zinazotokea kwenye viwanja ambavyo ligi hizo huchezwa na kuahidi kuyafanyia kazi maoni ya viongozi wa klabu.
"Viongozi wa klabu wamelalamikia pia mfumo wa tiketi za kieletroniki na kuweka wazi kwamba mapato yao yameshuka na kufikia asilimia 40," alisema Shibo.
Alisema kuwa Bodi ya Ligi imelichukua hilo na kulifanyia kazi na kueleza kwamba tayari wako katika mazungumzo na kampuni inayohusika na utengezaji wa tiketi hizo ambao ni benki ya CRDB kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Kiongozi huyo alimtaja mdhamini ambaye amepatikana kwenye Ligi Daraja la Kwanza kuwa ni Azam Media ambao pia wanaidhamini Ligi Kuu.
Katika suala la malalamiko kuhusiana na waamuzi, tayari Kamati ya Utendaji ya TFF, imeteua kamati maalum ambayo itafuatilia suala hilo na kutoa maamuzi ndani ya saa 75 baada ya mechi kuchezwa.
Shibo alisema kuwa kamati hiyo itaongozwa na Said Mohamed na Makamu wake Geofrey Nyange 'Kaburu' huku wajumbe ni Charles Ndagala na Steven Mguto.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment