Advertisements

Thursday, March 5, 2015

Bifu la Wema na Kajala Laibuka Upya!

Bifu la kati ya waigizaji marafiki wa zamani Wema Isaac Sepetu ‘Madam’ na Kajala Masanja ‘Kay’ inadaiwa kuwa limeibuka tena upya mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya Madam kuanika ubaya aliotendewa na Kajala aliyewahi kumlipia faini ya shilingi milioni 13 na kumuepusha na kifungo cha miaka 7 jela, Machi 25, 2013, kupitia kipindi chake cha In My Shoes kinachorushwa na kituo cha televisheni cha EATV.
Wafuasi na mashabiki wa Kajala hawakufurahishwa na maneno ya Wema ambayo walidai yalikuwa na lengo la kumvua nguo mwenzake, yale matumaini ya kusameheana hayapo tena.

“Wema hana busara, mtu mwenye busara zake hawezi kuzungumza hadharani mambo ya kuibiana mabwana, ni ujinga tu. Unazungumza ili iweje?” aliandika mfuasi wa Kajala mtandaoni.

Kwenye kipindi hicho, mbali na mambo mengine, Wema alieleza kuwa Kajala hakuwahi kuwa rafiki yake lakini alijitolea kumlipia faini kumuepusha na kifungo kutokana na kuguswa na kuingiwa na moyo wa huruma kama msanii mwenzake.

“Sikuwahi kuwa na urafiki na Kajala, kilichonifanya niwe karibu naye ni mwanaye ambaye alikuwa akinipenda na kutaka kukutana na mimi...,” alisema Madam.

Kupitia kipindi hicho, Wema pia alizungumzia kiini cha ugomvi wao ambapo alianika kinagaubaga kwamba alichukizwa na suala la Kajala kumsaliti kwa kutembea na mchumba wake aitwaye CK (yule kigogo aliyesumbua mjini kwa kutapanya fedha).“Kajala hana fadhila, huwezi amini mtu ambaye niliamua kujitolea kwa moyo wangu kumlipia Sh. milioni 13 huyohuyo aje kutembea na mchumba wangu, huku ni kukosa ubinadamu kulikopitiliza,” alisema Wema.

Jitihada za kumpata Kajala aweze kuzungumzia mashambulizi hayo ya Wema hazikuzaa matunda baada ya simu yake kuita bila kupokelewa lakini shosti yake wa karibu alisema Kajala amechukizwa na maneno hayo ya Wema na kamwe hatakuja kukaa naye meza moja, achilia mbali kumzika.

“Kajala hakufurahishwa na maneno ya Wema, hali ni mbaya, amesema kamwe hawezi kukaa na Wema meza moja maana amekuwa mtu wa kumdhalilisha kila kukicha, alianza kwa kumwambia ana nuksi na sasa amemdhalilisha katika kipindi chake, kamwe hatamsamehe na hayuko tayari kumzika wala kuzikwa na Wema,” alisema shosti huyo.

GPL

No comments: