ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 7, 2015

Chadema chasema CCM kinatapatapa

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Chadema, Tumaini Makene

Wakati Katibu wa Itikadi na Uenezi (CCM), Nape Nnauye, akikishutumu Chadema kuwa vijana wa Red Brigade wanaowapa mafunzo ni kwa ajili ya shughuli za kigaidi, wenyewe wamejibu kuwa CCM hakina hoja.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Chadema, Tumaini Makene, akijibu hoja hiyo jana alisema kuwa, adui wa CCM siyo Red Brigade bali ni kushindwa kwake na kubaki kutapatapa.

Makene alisema tishio la kwanza litaloiangusha CCM kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu ni kupoteza ushawishi na uhalali wa kisiasa kwa Watanzania.

“Kushindwa kwa sera za chama hichi kuwapatia Watanzania haki na matumaini katika nchi yao, kwa ajili ya amani na utulivu wa kweli ni moja ya sababu ambayo wananchi wataiondosha CCM madarakani,” alisema na kuongeza:
Alisema kuwa katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichofanyika hivi karibuni, moja ya mambo waliyokubaliana ni kutumia mikakati mbalimbali ya propaganda kupitia mikutano ya hadhara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Nape kuwatia hofu Watanzania.

Alisema kikao hicho walikubaliana kuibua mijadala mingine ili kuwasahaulisha Watanzania kujadili masuala ya msingi yanayoamua hatma ya taifa.

“Ushahidi wa hili ni namna CCM kilivyotumia njia haramu na kufanya uharamia kuharibu mchakato wa kuwapatia Watanzania Katiba Mpya na bora kwa ajili ya mstakabali mweka wa taifa letu,” alisema.

Alisema CCM kimekuwa hakipendi kuona Watanzania wakihoji udhaifu unaoendelea katika uandikishaji wa daftari la wapiga kura.
Aliongeza kuwa, ili kuwafanya wananchi wasijadili mambo ya msingi ambayo CCM haina majibu chama hicho kimeamua kurudi na propaganda dhidi ya mafunzo ya vijana wa Chadema.

Makene alidai kuwa CCM kilipaswa kuwa cha kwanza kuacha kuwafundisha kwa siri mafunzo ya namna ya kuteka, kutesa na kuua.

“Green Guard ni kikosi pekee cha ulinzi kinachotokana na chama cha siasa ambacho kimekuwa kikifanya matukio ya kushambulia, kuteka na kutesa wakati mwingine mbele ya Askari wa Jeshi la Polisi,” alisema na kuongeza
“Kimefanya hivyo mara nyingi hususan wakati wa uchaguzi, ushahidi wa matukio upo, hakuna hatua yoyote imewahi kuchukuliwa,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

No comments: