Mkazi wa Kijiji cha Mwakata akizungumza na simu alipokuwa akitoa taarifa kwa jamaa zake baada ya nyumba yake kubomoka kutokana na mvua ya mawe iliyonyesha kijijini hapo wilayani Kahama.
Kahama. Mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha juzi usiku imesababisha maafa katika kijiji cha Mwakata wilayani Kahama mkoani Shinyanga ambako zaidi ya watu 42 wameuawa, wakiwamo saba wa familia moja na wengine 91 kujeruhiwa vibaya.
Mvua hiyo ya aina yake ilisababisha nyumba 160 kuanguka na nyingine kuezuliwa paa kutokana na upepo mkali na watu wengine 900 wameripotiwa kukosa makazi.
Watu wengi walifariki kutokana na kuangukiwa na kuta za udongo za nyumba za wanakijiji hao na wengine kuuawa kutokana na kuangukiwa na mawe makubwa ya barafu wakati walipokuwa wakijaribu kutafuta hifadhi baada ya mapaa kutobolewa.
Mashuhuda wa tukio hilo waliliambia gazeti hili kuwa mawe makubwa ya barafu yalikuwa yakidondoka usiku na kuvunja nyumba za wakazi wa kijiji hicho ambazo nyingi ni za udongo.
Waokoaji walilazimika kufumua mabati yaliyoanguka na kufukua vifusi kwa ajili ya kutoa miili ya watu waliofariki na kuokoa walionusurika na baadaye kuwapakia kwenye malori ili kuwapeleka hospitalini.
“Mimi tangu nianze uongozi wa umma sijawahi kukutana na tukio la aina hii,” alisema Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya.
“Nashindwa kulizungumzia (suala hili). Hili ni tukio kubwa ambalo limepoteza uhai wa maisha ya watu hivyo nashindwa nianzie wapi lakini kifupi wananchi wa Mwakata wamekumbwa na msiba mzito,” alisema Mpesya, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Wilaya.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Ezekiel Sanane alisema wakati mvua hiyo inanyesha ilikuwa na upepo mkali na mawe makubwa ambayo yalikuwa yakitoboa nyumba na kutumbukia ndani na kuponda watu, hali ambayo iliwafanya wengine kukimbilia nje ambako pia walipigwa na mawe ya barafu na kufariki.
Sanane alisema wapo wengine walifunikwa kabisa na ukuta wa nyumba na kufariki, lakini wengine wamekufa wakiwa nje ya nyumba zao.
Hata hivyo mkazi wa kijiji hicho, Paulina Nyalulu alisema alinusurika kifo baada ya kukimbilia barabarani. Alisema baada ya kuona nyumba imejaa maji, yeye na familia yake walikimbilia barabarani ambako walishuhudia nyumba zao zikianguka, ingawa hakuna mtu aliyekufa.
“Tunamshukuru Mungu hakuna aliyekufa kwenye familia hii lakini kama unavyoona vitu vyote, vikiwemo vyombo pamoja na vyakula vimezolewa vyote maana maji yalijaa nyumba yote na sisi tulikimbia na ndiyo ilikuwa usalama wetu,” alisema Nyalulu.
Taarifa za awali zilizotolewa na kamanda wa polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Jastus Kamugisha zilieleza kuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka kutokana na kazi ya kufukua miili kutoka kwenye vifusi vya nyumba kuendelea hadi jana mchana.
Kamugisha alisema mvua hiyo ilikuwa ya upepo mkali na mawe makubwa ya barafu ambayo ndiyo chanzo kikubwa cha watu hao kufariki.
Alisema watu hao walifariki kwa kuangukiwa na nyumba na wengine walifariki kutokana na kupondwa mawe hayo mazito ya barafu wakati wakikimbia kutoka kwenye nyumba zao.
Madhara mengine yaliyosababishwa na mvua hiyo ni pamoja na kuharibika kwa mazao, mifugo kufariki na kubomoka kwa makanisa. Karibu asilimia 80 ya nyumba za wananchi wa kijiji hicho zimeangushwa na kusababisha wananchi wengi kukosa mahali pa kuishi.
Akizungumzia maafa hayo mapema jana, Mpesya alisema idadi ya watu waliokufa inaweza kuongezeka kutoka 42 baada ya kukamilika na kwamba kazi ya kuwatambua inaendelea.
Kamati yangu ya maafa leo (jana) baada ya tathmini ya hasara iliyojitokeza itakaa kujadili maafa hayo na baada ya kamati hiyo, kamati ya maafa ya mkoa itakaa jioni kutathmini hasara yote na namna ya watu hao watakavyoishi,” alisema Mpesya.
Aliwataka wananchi wa Mwakata kutohusisha tukio hilo na imani yoyote na tayari amewaagiza viongozi wa serikali wa eneo hilo kuendelea na taratibu za mazishi ya watu waliofariki wakati kazi ya kuwatafuta wengine ikiendelea.
“Ndugu zangu ambao tumesalimika kwenye tukio hili naomba tuendelee na kuwasitiri wenzetu waliokumbwa na maafa na wengine tuendelee kufanya tathmini pamoja na kuangalia maeneo mengine ambayo nyumba zimenguka,” alisema Mpesya.
Kwa upande wake, Daudi Maganga, ofisa tarafa mstaafu wilayani Kahama ambaye naye nyumba zake zilibomolewa pamoja na za familia ya watoto wake, alisema hivi sasa hali ya wananchi katika kijiji hicho ni mbaya.
“Hivi ikinyesha mvua sasa hivi hawa watu watakuwa wapi maana karibu kijiji kizima nyumba zake zimebomolewa na mvua hiyo pia idadi kubwa ya watu wanaishi shuleni wakati pia wale waliokimbilia makanisani nako majengo yameanguka na kubaki kanisa moja tu la AICT,”alisema Maganga.
Jana kamati zote mbili za ulinzi na usalama za mkoa wa Shinyanga na ile ya Wilaya ya Kahama zilikesha kwenye tukio hilo na hadi mchana zilikuwa zikiendelea na kutathmini ya madhara hayo ambayo Mpesya aliwaambia waandishi wa habari taarifa kamili juu ya tukio hilo itapatikana leo baada ya majumuisho yote kukamilika.
…yafanya uharibifu Moshi, Rufiji, Morogoro na Katavi
Moshi
Zaidi ya familia 10 za Kijiji cha Kiriwa wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro hazina makazi baada ya nyumba zao kuezuliwa na upepo mkali ulioambatana na mvua zilizonyesha kwa muda mfupi juzi.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Pius Shio alisema hayo juzi wakati akipokea msaada ya mabati 20 yaliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Lucy Owenye alipotembelea wananchi hao na kuwapa pole.
Shio alisema mvua na upepo mkali zilizonyesha kuanzia saa 8:00 mchana ziliezua nyumba kumi pamoja na kuharibu migomba.
Alisema kijiji hicho kitakumbwa na njaa baada ya migomba kuvunjika kutokana na upepo huo mkali ambao pia ulivunja miti mikubwa. Alisema miti hiyo pia iliangukia nyumba na kuzibomoa.
Kwa upande wake Owenya aliwataka wadua mbalimbali kuwasaidia wanachi hao kwa chakula kutokana na migomba ya kijiji hicho kuharibiwa.
Katavi
Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali imesababisha hasara baada ya kuezua paa la bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari ya Ikola wilayani Mpanda.
Mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo, Godfrey Mwale aliieleza timu ya kutathimini maafa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda kwamba uharibifu huo ulijitokeza kutokana na mvua hiyo iliyoambatana na upepo mkali.
Mwale alieleza kuwa tukio hilo lilitokea kati ya saa 8:00 na 9:00 usiku wakati mvua iliyoambatana na upepo mkali ilipoezua paa hilo na kulitupa umbali wa kama mita 15 kutoka kwenye bweni hilo.
Hata hivyo, kutokana na tukio hilo hakuna mwanafunzi yeyote aliyejeruhiwa kwa kuwa katika bweni hilo kulikuwa hakuna mwanafunzi anayelala kwa kuwa lilikuwa katika shughuli za ukarabati. Mwaka jana, bweni hilo pia liliezuliwa kwa upepo.
Kwa Upande wake mwenyekiti wa bodi ya shule, Antony Namayala alieleza kuwa mvua ilisababisha hasara na kuwarudisha nyuma kimaendeleo wananchi kutokana na kufanya uharibifu mkubwa.
Namayala alisema jumla ya mabati 60 yameezuliwa na kuisababishia hasara shule hiyo, ambayo iko katika harakati za kukamilisha ujenzi wa maabara za sayansi.
Morogoro
Mvua zilizonyesha juzi jioni mkoani Morogoro zimesababisha zaidi ya nyumba nne kuezuliwa paa maeneo ya Kijiji cha Doma wilayani Mvomero na kuharibu mabanda ya maonyesho yaliyokuwa yamejengwa kwenye Uwanja wa Jamhuri kwa ajili ya siku ya wanawake duniani ambayo kitaifa inafanyika mkoani hapa.
Mvua hizo ziliambatana na upepo mkali na kuacha familia hizo wilayani Mvomero kutokuwa na makazi kwa sasa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Doma kilicho wilayani Mvomero, Adam Said alisema kuwa mvua hizo zilinyesha zikiambatana na upepo mkali uliosababisha nyumba kuezuliwa paa, ikiwamo ya mganga wa zahanati ya kijiji hicho.
Mwenyekiti huyo wa kijiji aliuomba uongozi wa Wilaya ya Mvomero kufika kijijini hapo kuona hali halisi ya wananchi hao na jinsi gani watakavyoweza kuwasaidia wananchi.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba aliyefika eneo hilo, alisema atashirikiana na kamati ya mkoa kuona ni jinsi gani watafanya ili maonyesho hayo yaweze kuzinduliwa rasmi na kuendelea kama yalivyopangwa.
Waziri Simba alikagua mabanda yaliyoharibika pamoja na bidhaa na hivyo kuwatia moyo washiriki wa maonyesho hayo kutokana na hasara waliyoipata.
Kaya 60 hazina mahali pa kuishi wilayani hapa baada ya nyumba zao kuezuliwa na upepo mkali ulioambatana na mvua ya mawe iliyonyesha usiku wa kuamkia juzi katika Kijiji cha Mchukwi wilayani hapa.
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu alisema watu walioathirika na mvua katika eneo hilo ni mbaya na wanahitaji msaada wa haraka.
Alisema katika tukio hilo paa za msikiti, kanisa pamoja na Chuo cha Ufundi cha Mchukwi zimeezuliwa, wakati nyumba sita zimebomoka kabisa na gharama ya uharibifu huo unakadiriwa kuwa Sh45 milioni.
Tayari ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa wilaya na kamanda wa vijana wa CCM Rufiji, Ally Ungando alitoa viroba 60 vya unga kwa ajili ya wakazi hao.
Babu alisema ofisi ya mkuu wa wilaya imetoa mabati 60 kwa ajili ya kupaua upya majengo ya chuo cha ufundi yaliyoezuliwa na kutoa wito kwa wahisani wengine kuwasaidia wananchi hao.
Amini Yasini Fina Lyimo(Moshi), Kibada Ernest(Katavi) na Lilian Lucas(Morogoro) wa Mwananchi
No comments:
Post a Comment