Lakini hebu mpe huo ukubwa uone. Hapo ndipo utakapotambua uhalisia wake, kwa sababu utajua jinsi gani alivyo na utu, jeuri, tamaa, mzinzi, busara, fisadi na kila jambo. Kifupi, madaraka yanayoambatana na mamlaka ya kuamua hukupa picha halisi ya mtu.
Na kwa namna ambayo hukutegemea, mtu ambaye ulimuona mwingi wa busara, unaweza kujikuta ukishangazwa na ukatili wake, kama ambavyo mtu uliyeamini ni wa ovyo, anavyoweza kukushangaza kwa maamuzi na matendo yake yenye hekima na weledi uliotukuka.
Mimi ni miongoni mwa watu, nadhani wengi, walioshangazwa sana na uteuzi wa Paul Makonda, kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, wakati Rais Kikwete alipofanya uteuzi wake, unaodhaniwa kuwa wa mwisho wa wakuu wa wilaya.
Nilishangazwa kwa sababu kubwa mbili. Kwanza ni udogo wake kwa umri, ambao una tofauti kubwa na majukumu mazito anayokwenda kukabiliana nayo. Maana haipendezi mtoto mdogo akapewa jambo lililostahili mtu mzima, asije akaleta mambo ya disko wakati watu wanahitaji hekima.
Jambo la pili lililonifanya nishangazwe na JK kumpa dhamana kubwa kama ile, ni kile ambacho binafsi hukiamini kuwa Makonda hana busara. Kwa jinsi ambavyo amekuwa akitoa maneno kumhusu waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa hayaonyeshi kama ni kijana aliyekulia kwenye utamaduni wa kuheshimu wakubwa, kwani licha ya mbunge huyo wa Monduli kumzidi sana umri, pia kwa wadhifa wake, anastahili heshima, hasa kutoka kwa chipukizi wa chama chake, akiwemo Makonda.
Lakini kitu kimoja tu alichokifanya, kimenifanya nione afadhali ya akina Makonda kumi wangepewa Ukuu wa Mikoa wangekuwa na msaada kwa watu, kuliko waheshimiwa wengi wanaoishi kwa kudhani wako peponi na kusahau kabisa maisha halisi ya Watanzania.
Mwanzoni mwa wiki hii, Makonda alitoa agizo (kazi ipo katika utekelezaji wake) kwamba polisi wanapaswa kuwekwa katika hospitali mbili za Palestina iliyopo Sinza na Mwananyamala, zote katika Wilaya ya Kinondoni, ili kutoa unafuu kwa wananchi kupata Hati ya Matibabu (PF3).
Nadhani suala hili limechelewa mno na kwa kiasi kikubwa, linachangia sana kuwepo kwa vifo ambavyo vingeweza kuzuilika. Mtu amepigwa kisu na vibaka nje ya hospitali, ameporwa kila kitu na damu nyingi zinamtoka, lakini sheria zinataka kabla ya kutibiwa, lazima kwanza apate fomu ya matibabu kutoka polisi!
Kama ni lazima kwa matakwa haya ya sheria kutimizwa, kwa nini kusiwe na utaratibu wa kuwaweka polisi katika hospitali zote ili kuwanusuru watu wanaoshambuliwa na wezi, majambazi au wanaopata ajali?
Chukulia mfano wa mtu aliyeshambuliwa na vibaka, amepigwa, ameporwa na hana kitu, anatokea msamaria, badala ya kukimbizwa hospitalini, anapelekwa kwanza polisi, ambako nako kuna urasimu wa kupitiliza.
Mtu anayevuja damu anaweza kukaa kituo cha polisi zaidi hata ya nusu saa pasipo kuhudumiwa na anapoanza kuulizwa maswali, saa nzima inaweza kupita kabla ya kupewa PF3 na kuondoka. Kwa majeruhi, saa moja ni muda mrefu sana wa kuvuja damu.
Kwa hiyo wakati ninatoa pongezi za dhati kwa Makonda kwa agizo lake lenye akili, ninawataka watu wazima wengi walioshika nafasi za umma kuwa na wepesi wa utambuzi kama huu, wa kuelewa nini hasa watu wanahitaji na kwa wakati gani.Nimuombe Rais Kikwete kulipokea suala hili kwa umakini mkubwa na asimamie utekelezaji wake kwa faida ya Watanzania wenye kero nyingi.
GPL
2 comments:
Hiyo si sababu yakuficha mabaya yake yakutaka kumdhuru mzee wetu kwa uchu wa madaraka.
Hivi kweli kuna umuhimu gani wa mgonjwa aliyejeruhiwa au aliyepata ajali aende kwanza polisi akachukue PF 3? Sijaelewa hadi leo kwa nini wagonjwa waende polisi kuchukua PF 3......ni muhimu kuokoa maisha ya watanzania wote kwani kila mtu anayo haki ya kuisha awe jambazi au nani. Kwani polisi wanashindwa kwenda kuchukua maelezo yao wagonjwa wakiwa hospitali wakiwa na unafuu? Bado serikali yetu inafanya mambo ya enzi za mawe (stone age) haijali maisha ya wananchi wake kwa sababu wao na familia zao wakipata tatizo ndege zipo tayari tayari kuwapeleka Afrika kusini na Nairobi au India.
Post a Comment